Mzinifu Asiyeoa Alizini Zaidi Ya Mara Mia Na Akatubia Kikweli, Je, Atasamehewa Na Allaah? Na Je, Apigwe Fimbo Mia Kwa Kila Kosa?

SWALI:

Assallamu Allaikum warahmatul llwahi wabarakatu nini hukumu ya mzinifu aliekua hajaoa alizini kwa zaidi ya mara mia kisha akatubia akajuta akalia nakuacha kabisa tendo hilo pasi na kupigwa fimbo jee atapata msamaha wowote kwa Allaah na jee apigwe fimbo mia kwa kila tendo la zina.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu hukumu ya mzinifu ambaye bado hajaoa.

Hakika ni kuwa lau mzinifu atafanya madhambi yake kwa siri bila ya kujulikana na mtu hukmu yake inabakia baina yake na Allaah Aliyetukuka. Hata hivyo, Muumini wa kweli ni yule ambaye anaweza kujisalimisha pindi anapofanya kosa linalohitajia adhabu ili apate kusafishwa. Swali ni kuwa kwa sasa anaweza kujisalimisha kwa nani na dola zote hakuna shari’ah inayofuatwa?

Ikiwa hali ni hiyo basi itabidi awe na Niyah thabiti kuwa lau kungekuwa na dola ya Kiislamu yenye kuhukumu kwa shari’ah basi angejisalimisha kwa Kiongozi. Kwa kuwa sasa haipo itabidi afuate masharti ya kukubaliwa toba, kama:

1.     Kujiondoa katika makosa kwa kutorudia tena dhambi hilo.

2.     Kujuta kwa kufanya kosa hilo.

3.     Kuazimia kutorudia tena dhambi hilo.

 

Kwa kuwa Allaah Aliyetukuka Anasemehe madhambi yote (az-Zumar [39]: 53) hayo aliyofanya pia atasamehewa bila ya tatizo lolote na Mwenye Kusamehe makosa, Allaah Aliyetukuka.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

Mazuri hufuta mabaya” (at-Tirmidhiy). Kwa hiyo, afanye mazuri kwa wingi.

 Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

Nini Hukumu Ya Mwenye Kuzini Kwa Siri?

Binti Mwenye Kufanya Maasi Ya Zinaa

Duaa Gani Kuomba Ya Kujiokoa Na Zinaa

Mwenye Kufanya Maasi Ya Liwati Anaweza Kurudi Kwa Allah Kutubia?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share