Surat Yuusuf Ukisoma Inaondosha Wivu? Na Zipi Surah Zilotajwa Fadhila Zake Katika Qur-aan

SWALI:

 

Assalam Alleikum Sheikh,

 

Ningependa kama utanielimisha kuhusu faida ya kila surah katika Quran,

nilipata forward inayosema faida ya kila surah k.m Surat Yusuf - kuondoa

wivu, Surat Anfaal - kutimiziwa haja zako n.k Pia inasema kusoma Surat Yasin ni kama kusoma Quran 12 na kufanya Hajj 20.

 

Tafadhali nielimishe. Shukran

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu fadhila za baadhi ya Surah.

Fadhila za Surah nyingi zimepatikana kutokana kwa Hadiyth dhaifu au maudhu’ (za kutungwa; za uongo), hivyo kutoweza kutegemewa.

 

Mfano wa fadhila zilizoenea kutajwa, ni za Surah Yaasin ambazo si sahihi.

 

Ama Surat Yuusuf, Ibn Kathiyr ametaja Hadiyth ya kutoka kwa Ubayy bin Ka’b (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambayo Ibn Kathiyr kaeleza kuwa ni dhaifu, nayo inasema:

“Wafundisheni wasichana wenu Surat Yuusuf, kwani hakuna Muislamu atakayeisoma au kumfundisha mkewe au aliyemmiliki kwa mkono wake wa kuume ila Allaah Humpunguzia machungu ya umauti na kumpatia nguvu ya kutomhusudu Muislamu yeyote”. Kisha akasema Ibn Kathiyr: “Na hii (Hadiyth) katika njia hii haisihi kwa sababu ya udhaifu kabisa wa Isnadi yake”.

 

Ama Suratul Anfaal hatukupata fadhila zake.

 

Zipo Surah zenye fadhila zinazofahamika kwa Hadiyth zilizo sahihi kama Suratul Ikhlaasw, ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ni thuluthi ya Qur-aan, kusomwa Suratul Kahf siku ya Ijumaa kunamuepusha mtu na fitnah za Dajjal n.k.

 

Soma ndani ya kiungo hichi kwa maelezo zaidi:

 

Fadhila Za Surat Yaasiyn Na Al-An'aam

 

Nataka kujua matumizi ya Surah Yaasiyn na Ayatul Kursiy

 

Surat Yaasiyn Inafaa Kumsomea Mtu Anayekata Roho

 

Vijitabu Vya Surat Yaasiyn Na Surah Maalum Za Kusomwa Na Yaasiyn, Vinafaa Kuvitumia?

 

Fadhila Za Suratul-Kahf Surah Namba: 18

 

Surah Saba Ziitwazo Sabaa Munjiyaat Ni Swahiyh Kuzisoma Kila Siku?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share