02-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Kuhukumu: Mlango Wa Madai na Ushahidi

 

 

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَاب اَلْقَضَاءِ

Kitabu Cha Kuhukumu

 

بَابُ اَلدَّعْوَى وَالْبَيِّنَاتِ

02-Mlango Wa Madai na Ushahidi[1]

 

 

 

 

1210.

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {"لَوْ يُعْطَى اَلنَّاسُ بِدَعْوَاهُمْ، لَادَّعَى نَاسٌ دِمَاءَ رِجَالٍ، وَأَمْوَالَهُمْ، وَلَكِنِ اَلْيَمِينُ عَلَى اَلْمُدَّعَى عَلَيْهِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ ‏ وَلِلْبَيْهَقِيِّ بِإِسْنَادٍ صَحِيحٍ: {"اَلْبَيِّنَةُ عَلَى اَلْمُدَّعِي، وَالْيَمِينُ عَلَى مَنْ أَنْكَرَ}

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Lau watu wangepewa kulingana na madai yao, basi watu wengine wangedai damu za watu na mali zao.[2] Lakini yamini ni juu ya mdaiwa.” [Bukhaariy, Muslim]

Na amepokea Al-Bayhaqiyy kwa isnaad sahihi: “Ushahidi ni juu ya mdai na yamini ni juu ya aliyekana.”

 

 

 

1211.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏عَرَضَ عَلَى قَوْمٍ اَلْيَمِينَ، فَأَسْرَعُوا، فَأَمَرَ أَنْ يُسْهَمَ بَيْنَهُمْ فِي اَلْيَمِينِ، أَيُّهُمْ يَحْلِفُ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Aliwaambia watu fulani waape, wakaharakisha. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaamrisha kupiga kura[3] baina yao nani kati yao aape.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

1212.

وَعَنْ أَبِي أُمَامَةَ اَلْحَارِثِيُّ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {" مَنْ اِقْتَطَعَ حَقَّ امْرِئٍ مُسْلِمٍ بِيَمِينِهِ، فَقَدْ أَوْجَبَ اَللَّهُ لَهُ اَلنَّارَ، وَحَرَّمَ عَلَيْهِ اَلْجَنَّةَ" .‏ فَقَالَ لَهُ رَجُلٌ: وَإِنْ كَانَ شَيْئًا يَسِيرًا يَا رَسُولَ اَللَّهِ؟ قَالَ: "وَإِنْ قَضِيبٌ مِنْ أَرَاكٍ"} رَوَاهُ مُسْلِم ٌ

Kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Haarithiy[4] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayejichukulia haki ya mtu Muislaam kwa kiapo chake, hakika Allaah Amekwishamuajibishia moto na Amemharamishia Jannah. Mtu mmoja akasema: ‘Ee Rasuli wa Allaah! Hata kama ni kitu kidogo? Akasema: hata kama ni kipande cha mswaki.”[5] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1213.

وَعَنِ الْأَشْعَثِ بْنِ قَيْسٍ رضى الله عنه‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {"مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ، يَقْتَطِعُ بِهَا مَالَ امْرِئٍ مُسْلِمٍ، هُوَ فِيهَا فَاجِرٌ، لَقِيَ اَللَّهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْبَانُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Al-Ash’ath bin Qays[6] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayeapa yamini ili ajikatie mali ya mtu Muislaam ilihali katika hilo ni muovu; atakutana na Allaah ilihali Amemghadhibikia.” [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1214.

وَعَنْ أَبَى مُوسَى اَلْأَشْعَرِيِّ رضى الله عنه‏ {أَنَّ رَجُلَيْنِ اِخْتَصَمَا إِلَى رَسُولِ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فِي دَابَّةٍ، لَيْسَ لِوَاحِدٍ مِنْهُمَا بَيِّنَةٌ، فَقَضَى بِهَا رَسُولُ اَللَّهِ‏ بَيْنَهُمَا نِصْفَيْنِ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ وَهَذَا لَفْظُهُ، وَقَالَ: إِسْنَادُهُ جَيِّدٌ

Kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Watu wawili waligombania mnyama, wala hakuna yeyote kati yao mwenye ushahidi. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akahukumu baina yao nusu mbili.”[7] [Imetolewa na Ahmad, Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy, Hadiyth hii ni tamshi lake na akasema: Isnaad yake ni nzuri]

 

 

 

1215.

وَعَنْ جَابِرٍ‏ رضى الله عنه أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {"مَنْ حَلَفَ عَلَى مِنْبَرِي هَذَا بِيَمِينٍ آثِمَةٍ، تَبَوَّأَ مَقْعَدَهُ مِنْ اَلنَّارِ"} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayeapa juu ya mimbari yangu hii kwa yamini ya dhambi, basi ameandaa makazi yake motoni.”[8] [Imetolewa na Ahmad, Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

1216.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{"ثَلَاثَةٌ لَا يُكَلِّمُهُمْ اَللَّهُ يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ، وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ، وَلَا يُزَكِّيهِمْ، وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ: رَجُلٌ عَلَى فَضْلِ مَاءٍ بِالْفَلَاةِ، يَمْنَعُهُ مِنْ اِبْنِ اَلسَّبِيلِ; وَرَجُلٌ بَايَعَ رَجُلاً بِسِلْعَةٍ بَعْدَ اَلْعَصْرِ، فَحَلَفَ لَهُ بِاَللَّهِ: لَأَخَذَهَا بِكَذَا وَكَذَا، فَصَدَّقَهُ، وَهُوَ عَلَى غَيْرِ ذَلِكَ; وَرَجُلٌ بَايَعَ إِمَامًا لَا يُبَايِعُهُ إِلَّا لِلدُّنْيَا، فَإِنْ أَعْطَاهُ مِنْهَا، وَفَى، وَإِنْ لَمْ يُعْطِهِ مِنْهَا، لَمْ يَفِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu watatu[9] Allaah Hatawasemesha Siku ya Qiyaamah wala Hatawatazama wala Hatawatakasa na wana adhabu kali: (a) mtu mwenye maji ya ziada jangwani na anamyima msafiri, (b)mtu aliyeuziana bidhaa na mtu baada ya Al-‘Aswr akaapa kwa kadha wa kadha, akamuamini na yeye si hivyo, (c) na mtu aliyembai kiongozi kwa ajili ya dunia tu akimpa kitu hutekeleza na asipompa kitu hatekelezi.” [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1217.

وَعَنْ جَابِرٍ رضى الله عنه {أَنَّ رَجُلَيْنِ اِخْتَصَمَا فِي نَاقَةٍ، فَقَالَ كُلُّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا‏ نُتِجَتْ عِنْدِي، وَأَقَامَا بَيِّنَةً، فَقَضَى بِهَا رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏لِمَنْ هِيَ فِي يَدِهِ}

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Watu wawili waligombania ngamia, kila mmojawapo akasema: ‘Ngamia huyu amezaliwa kwangu’ na wao wakaleta uthibitisho. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akahukumu ngamia huyo ni wa ambaye yuko mkononi mwake.”

 

 

 

1218.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا،{أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏رَدَّ اَلْيَمِينَ عَلَى طَالِبِ اَلْحَقِّ} رَوَاهُمَا اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَفِي إِسْنَادِهِمَا ضَعْفٌ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alirudisha yamini ya mwenye kutafuta haki.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy na katika isnaadi zake kuna udhaifu]

 

 

 

1219.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا {قَالَتْ: دَخَلَ عَلَيَّ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏ذَاتَ يَوْمٍ مَسْرُورًا، تَبْرُقُ أَسَارِيرُ وَجْهِهِ.‏ فَقَالَ: "أَلَمْ تَرَيْ إِلَى مُجَزِّزٍ اَلْمُدْلِجِيِّ ؟ نَظَرَ آنِفًا إِلَى زَيْدِ بْنِ حَارِثَةَ، وَأُسَامَةَ بْنِ زَيْدٍ، فَقَالَ: " هَذِهِ أَقْدَامٌ بَعْضُهَا مِنْ بَعْضٍ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliingia kwangu hali ni mwenye furaha, uso wake wameremeta. Akasema: “Je umemuona Mujazzizin Al-Mudlijiyy?[10] Muda mfupi amemtazama Zayd bin Haarithah na Usaamah bin Zayd akasema: “Hakika nyayo hizi baadhi yake zinatokana na baadhi nyingine.” [Bukhaariy, Muslim]

 

[1] Maana ya Da’waa (mashtaka au ulingano) ni kuweka madai ya mtu katika kitu kwa kusema: “Ni haki ya kitu kadha wa kadha.” Bila kujali madai hayo yaliyowekwa ni kweli au si kweli. Bayyinah ina maana ya jambo lililo wazi, bayana, maadamu inathibitisha haki ya kishariy’ah ya mmiliki katika kitu kinachogombewa.

 

[2] Moja katika kanuni za msingi za shariy’ah ni kuwa mdai ni lazima athibitishe ukweli wa madai yake kwa kuleta vithibitisho, kuleta mashahidi n.k. mdaiwa au mshtakiwa ni lazima athibitishe ukweli wa madai yake kwa kuthibitisha au kwa kukana. Kama hili halijafanyika, mdaiwa anatakiwa alete ushahidi wa kukana madai au aape. Katika kesi ya mtuhumiwa mauaji ni kuwa mdaiwa (kama hali itaruhusu) anatakiwa alete mashahidi 50 watakaotoa kiapo. Akishindwa mdaiwa kufanya hivyo, au mdai kutoamini viapo vile, basi wakati huo anaweza kuleta viapo kama vile na kutaka alipwe fidia.

 

[3] Ikiwa mazingira ya madai ni imetokea kuwa makundi yote hasimu kila kimoja ni mdai na mdaiwa kwa wakati huo mmoja, basi makundi yote yanawajibika kutoa kiapo. Ikiwa kundi moja limekataa kutoa kiapo, kundi hasimu linatakiwa lifanye hivyo na kuchukua kinachogombaniwa. Kama hali itakuwa ni kwa makundi yote kuwa tayari kutoa viapo, mwenye kustahiki ataamuliwa kwa kura. Jina lolote litakalotokeza katika utaratibu huo atachukua kiapo kisha atachukuwa kitu kinachogombewa.

[4] Huyu ni Abuu Umaamah Iyaas bin Tha’labah Al-Answaar Al-Haarith Al-Khazraji. Inasemekana ni katika kabila la Balawi lililokuwa mshirika na Answaar. Alikuwa ni Swahaba wa kitambo, hakushiriki Badr kwa kuwa alikuwa akimuuguza mama yake.

 

[5] Hadiyth hii inathibitisha kuwa mtu akitoa kiapo cha uongo na kuchukua kitu cha mtu (hata kikiwa ni kidogo kiasi gani) au akamkosesha mtu mwenye haki na kitu chake, mtu huyo ataharamishiwa Jannah.

[6] Al-Ash’ath bin Qays bin Ma’dikarib Al-Kindi, Abuu Muhammad kwa jina lingine alikuwa ni Swahaba aliyeishi katika mji wa Kufa ‘Iraq. Alipoteza macho yake mawili katika vita vya Yarmuk. Alikuwa ni mtu karimu na mwema. Alichaguliwa kuwa ni gavana wa Azerbaijan na alihudhuria Siffin akiwa na ‘Aliy. Alifariki baada ya siku arubaini ya kifo cha ‘Aliy katika mwaka 40 Hijriyyah akiwa na umri wa miaka 63.

[7] Hii ni hali ambayo makundi yote mawili yanadai kitu kimoja. Ima hawakuwa tayari kuapa, au hawakuwa na mashahidi wa kuthibitisha madai yao. Hii ina maana walikuwa katika hadhi moja kuhusu madai yao. Ikiwa jambo katika mazingira kama haya litatokea, basi kitu kinachogombewa kitabaki kwa aliye nacho. Ikiwa hakuna aliyekuwa nacho, au kitu hicho kipo katika umiliki wa nusu kwa nusu, basi hukumu ni kukigawa kitu kinachogombewa mara mbili na kila mmoja kupata nusu yake.

 

[8] Hadiyth hii inaonesha kuwa uzito wa dhambi unategemea ni sehemu mtu aliyefanyia kitu kile na wakati alioufanya.

[9] Hadiyth hii inalinganisha watu wenye madhambi, kuwa hali zao zitakuwa mbaya sana, na wanastahiki ghadhabu za Allaah.

[10] Imepokelewa kuwa Zayd bin Haarith muachwa huru wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alielekea kuwa mweupe zaidi ilihali mwanae Usaamah alikuwa mweusi. Kwa ajili ya hili baadhi ya makafiri wakashuku nasaba ile. Mujazzizin Al-Mudlijiyy aliwaona wakiwa wamelala, wamejifunika nyuso zao na miguu yao ikiwa wazi. Alipoona miguu yao alisema maneno hayo ambayo yalimfurahisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Hii ni dalili ya kuwa mtu anapopata mashaka na kitu ni bora akapata ushauri wa wataalamu kama huyo bwana mtaalamu wa nasaba alivyofanya.

Share