07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Aina Za Mali Ambazo Ni Waajib Kuzitolea Zakaah

 Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

07-Aina Za Mali Ambazo Ni Waajib Kuzitolea Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kwa mapana na marefu kuhusu aina za mali ambazo ni lazima zitolewe Zakaah. Kuna waliobana na kushikilia aina zile zile tu zilizotajwa bayana kwenye Aayaat na Ahaadiyth. [Ni kama Ibn Hazm, kisha Ash-Shawkaaniy na Swiddiyq Khaan (Rahimahumul Laah)]

 

Wengine wametanua wigo na kuingiza kila mali inayostawi hata pia kutoshurutisha kufikia kiwango cha Zakaah kwa baadhi ya mali hizo. [Ni kama Abu Haniyfah (Rahimahul Laah)]

 

Wabanaji wanasemaje kuhusu mwelekeo wao huo?   

 

Mwono wa Ibn Hazm na waliokubaliana na rai yake kuhusu wajibu wa Zakaah katika aina zile zile tu nane ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alichukua Zakaah, uko juu ya mambo mawili: [Angalia Fiqhu Az-Zakaah (1/165)]

 

1-  Uharamu uliothibiti kwa Hadiyth na Aayah juu ya mali ya Muislam. Haijuzu kuchukua chochote katika mali yake isipokuwa kwa maelekezo ya Aayah au Hadiyth.

 

 

2- Zakaah ni kalifisho la kisharia. Na dhima za watu kiasli hazina makalifisho isipokuwa yale tu yaliyokuja katika matini (Qur-aan au Hadiyth) ili tusije kuingiza sharia katika diyn ambayo Allaah Hakuiruhusu.

 

Ama Al-Qiyaas, hilo halijuzu kulitumia na hususan katika mlango wa Zakaah.

 

 

Waliotanua wigo wa mali za Zakaah wanasemaje kuhusu mwono wao?

Waliofungua milango zaidi ya aina za mali zinazolazimu kutolewa Zakaah, hawa njia yao imesimamia juu ya misingi ya uswuwl. Kati yake ni:

 

1- Kutoa dalili kwa kutumia ujumuishi wa Aayah za Qur-aan na Sunnah zinazosema kuwa kila mali ina haki ndani yake au swadaqah.

 

2- Matajiri wote na mali zao zote, wanahitajia kutakaswa na kutwaharishwa.

 

3- Kwa mazingatio ya ustawi na faida wamesema: “Mwenye kumiliki majengo na viwanda ambavyo vinamletea faida nyingi maradufu ya faida anayoipata kutokana na ardhi ya kilimo, ana haki zaidi ya kutoa Zakaah”.

 

4- Kuzingatia maslaha ya wote kwa kukidhi mahitaji ya masikini na fakiri na pia kuasisi maslaha jumuiya ya Waislamu wote.

 

Aina ambazo zimekubaliwa na wote kuwa ni lazima zitolewe Zakaah

 

‘Ulamaa kwa Ijma’a wamekubaliana kuwa ni waajib kuzitolea Zakaah aina tisa za mali:

 

1,2- Dhahabu na fedha (silver) [An-Naqdayn]

 

3,4,5- Ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo (mifugo).

 

6,7,8,9- Ngano, shayiri (barley), tende na zabibu kavu (mazao na matunda). [Haikuthibiti Ibn Hazm kuzungumzia zabibu kavu, hakugusia, bali amezizungumzia sampuli nane nyingine. Angalia Al-Muhallaa (5/209)]

 

 

 

Share