10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Kiwango Cha Zakaah Ya Noti (Bank Note)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

10-Kiwango Cha Zakaah Ya Noti (Bank Note)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kuna ‘Ulamaa wa enzi yetu ya leo ambao wanaona kuwa Zakaah ya “bank note” ikadiriwe kwa kiwango cha fedha, kwa kuwa ukadiriaji huu una manufaa zaidi kwa masikini.

 

Lakini wengine wanaona kuwa kiwango chake ni kiwango cha dhahabu, kwa kuwa thamani ya fedha ilibadilika baada ya enzi ya Nabiy na waliokuja baada yake mpaka ikapoteza thamani yake kabisa kinyume na dhahabu ambayo thamani yake kwa kiasi kikubwa inaonekana kutulia na kuimarika.

 

Halafu, kiwango cha dhahabu kiko karibu na viwango vyingine vya Zakaah kama ngamia watano, mbuzi au kondoo arobaini na kadhalika. Kwani vipi ikubalike na akili Uislamu usiwajibishe Zakaah kwa mwenye kumiliki ngamia wanne au kondoo 39 na kumzingatia kama masikini, halafu uje kuwajibisha Zakaah kwa mwenye kumiliki kiwango cha fedha ambacho hawezi hata kununulia mbuzi mmoja na kumzingatia kama tajiri?

 

Hakuna shaka kuwa madhehebu haya yako sawa zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Mfano bainishi:

 

Mtu mmoja ana pauni 2,000 na mwingine ana pauni 100,000. Ni kiasi gani cha Zakaah atatoa kila mmoja wao baada ya kupita mwaka?

 

Jibu:

 

Kwanza, tunahitaji kujua kiasi cha kiwango cha dhahabu kama ilivyotangulia ambazo ni gramu 85. Tukisema kwa mfano thamani ya gramu moja ya dhahabu ni sawa na pauni 30, kiwango kitakuwa: 85×30 = pauni 2,550. Na kwa kuwa anachokimiliki mtu wa kwanza ni chini ya kiwango, basi Zakaah si wajibu juu yake isipokuwa kama ataamua tu kutoa swadaqah.

 

Ama mtu wa pili, huyu anamiliki kiasi ambacho ni kikubwa kuliko kiwango. Huyu ni lazima atoe 2.5%. Zakaah yake itakuwa:

 

100,000 ÷ 40 = pauni 2,500  au 2.5 ÷ 100 × 100,000 = pauni 2,500

 

Hivyo atatoa pauni 2,500 kama Zakaah.

 

 

 

Share