15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Ngamia

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

15-Zakaah Ya Ngamia

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Viwango Vya Zakaah Kwa Ngamia Na Kiasi Chake Cha Wajibu

 

Mwenye kumiliki chini  ya ngamia watano –madume au majike, wadogo au wakubwa– basi hana Zakaah. Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ليس فيما دون خمس ذود من الإبل صدقة))

((Hakuna chini ya ngamia watano Zakaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1447) na Muslim (979). Tushaitaja nyuma]

 

Ama waliozidi watano na kwenda mbele, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amebainisha kiasi cha uwajibu wa kutolewa Zakaah katika Hadiyth ya Anas katika barua ya Abu Bakr aliyomtumia. Barua hiyo ni hii hapa kwa maandishi yake kutokana na umuhimu wake mkubwa tokea hapo:

 

Toka kwa Anas kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimwandikia maelezo haya alipomtuma kwenda Bahrain:

“Bismil Laahi Ar-Rahmaan Ar-Rahiym. Hii ni fariydhwah ya Zakaah ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameifaradhisha kwa Waislamu wote na ambayo Allaah Amemwamuru kwayo Rasuli Wake. Atakayetakwa katika Waislamu kwa njia ya sawa basi atoe, na atakayetakwa zaidi ya inavyostahiki, basi asitoe. Katika ngamia 24 na chini ya idadi hiyo (hadi watano), atatoa toka “ghanam”, mbuzi mmoja (au kondoo mmoja) kwa kila ngamia watano. Wakifika ngamia 25 hadi 35, basi atolewe binti makhaadhw jike, wakifika 36 hadi 45, basi atolewe binti labuwn jike. Wakifikia 46 hadi 60, atatolewa hiqqat aliye tayari kupandwa na dume, wakifikia 61 hadi 75, basi atatolewa jadha’a, wakifikia -yaani 76 hadi 90– basi atatolewa binti labuwn wawili. Wakifikia 91 hadi 120, basi watatolewa hiqqah wawili wanaopandwa na madume. Wakizidi zaidi ya 120, basi katika kila 40 atatolewa binti labuwn, na katika kila 50 atatolewa hiqqah. Na ambaye hana isipokuwa ngamia wanne tu, basi hana Zakaah ila tu kama mmiliki wake atataka. Wakifikia ngamia watano, basi atatoa mbuzi mmoja (au kondoo). Na katika Zakaah ya mbuzi na kondoo (ghanam) waliochungwa na kulishwa kwenye malisho halali yasiyo na gharama, wakiwa 40 hadi 120, atatolewa mbuzi mmoja (au kondoo). Wakipindukia 120 hadi 200, watatolewa mbuzi wawili (au kondoo wawili). Wakizidi zaidi ya 200 hadi 300, watatolewa mbuzi watatu (au kondoo watatu). Wakizidi zaidi ya 300, basi katika kila 100 mbuzi mmoja (au kondoo). Na ikiwa mbuzi wa mtu (au kondoo) aliowachunga na kuwalisha katika malisho halali yasiyo na gharama amepungua mmoja katika mbuzi 40, basi hakuna Zakaah hapo isipokuwa kama mmiliki wake atataka. Na katika fedha (silver) ni robo ya kumi, na kama hakuna isipokuwa 190, basi hakuna kitu humo ila kama mmiliki wake atataka”. [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1454), Abu Daawuwd (1567) na An-Nasaaiy (5/18)]

 

Na kwa mujibu wa Hadiyth hii, Zakaah ya ngamia hutolewa kwa mujibu wa jedwali ifuatayo:

 

Idadi ya ngamia wanaomilikiwa

 

Kiasi cha wajibu kutolewa

Kuanzia

Hadi

1

4

Hakuna Zakaah

5

9

Mbuzi mmoja (au kondoo mmoja)

10

14

Mbuzi wawili (au kondoo wawaili)

15

19

Mbuzi watatu (au kondoo watatu)

20

24

Mbuzi wanne (au kondoo wanne)

25

35

Binti makhaadh mmoja. [Ni ngamia jike aliyetimiza mwaka mmoja na anaingia mwaka wa pili. Ameitwa hivi kwa kuwa mama yake amejiunga na makhaadh, nao ni ngamia wenye mimba]. Kama hakupatikana, itatosha kutoa ibni labuwn mmoja dume.

36

45

Binti labuwn mmoja. [Ni ngamia jike aliyetimiza miaka miwili na kuingia mwaka wa tatu. Ameitwa hivi kwa kuwa mama yake amezaa vitoto vingine na kuwa na maziwa]

46

60

Hiqqah mmoja. [Ni ngamia jike aliyetimiza miaka mitatu na kuingia mwaka wanne. Ameitwa hiqqah kwa kuwa anaweza kupandwa na dume]

61

75

Jadha’a mmoja. [Ni ngamia jike aliyetimiza miaka minne na kuingia mwaka wa tano]

76

90

Binti labuwn wawili

91

120

Hiqqah wawili

 

 

Ninasema: “Hii ndio idadi na kiasi kilichoelezewa katika Hadiyth ya Abu Bakr toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), na Ijma’a ya ‘Ulamaa imepitisha hilo”. [Al-Majmuw’u (5/400), Al-Amwaal cha Abiy Úbayd (uk.363) na Al-Mughniy (2/577)].

 

Ama idadi ya ngamia ikipita zaidi ya 120, linalofanywa na ‘Ulamaa wengi –kinyume na Hanafiy, An-Nakhíy na Ath-Thawriy– ni hili linalobainishwa na jedwali ifuatayo. [Hanafiy anasema kuwa faradhi inaanzia baada ya (120). Katika kila watano katika waliozidi, ni mbuzi mmoja kuongezea na hiqqah wawili].

 

Na ujumla wake ni kuwa kwa kila ngamia 50, atatolewa hiqqah, kwa kila 40, atatolewa binti labuwn, na hili limetajwa katika Hadiyth (ya Abu Bakri) iliyotangulia.

 

Idadi ya ngamia wanaomilikiwa

 

Kiasi kilicho wajibu kutolewa

Kuanzia

Hadi

121

129

Binti labuwn watatu

130

139

Hiqqah mmoja + binti labuwn wawili

140

149

Hiqqah wawili + binti labuwn mmoja

150

159

Hiqqah watatu

160

169

Binti labuwn wanne

170

179

Binti labuwn watatu + hiqqah mmoja

180

189

Binti labuwn wawili + hiqqah wawili

190

199

Hiqqah watatu + binti labuwn mmoja

200

209

Hiqqah wanne + binti labuwn watano

 

 

Na hivi hivi kuendelea: Walio chini ya kumi msamaha (hakuna kitu). Na wakikamilika kumi, ufaradhi unahamia kati ya mahiqqah na mabinti labuwn juu ya msingi wa tuliyoyaeleza kuwa katika kila 50 hiqqah, na kila 40 binti labuwn. [Angalia Fiqhu Az Zakaah cha Dk. Yuwsuf Al-Qaradhwaawiy (1/195)]

 

Angalizo

 

Nambari zilizotajwa kwenye jedwali, zinakusanya aina zote za ngamia; “bukht” (wenye nundu mbili), “’iraab”wenye nundu moja na wengineo. Jina “Al-Ibil” linawahusu ngamia wote.

 

 

Aliyewajibikiwa kutoa ngamia wa umri fulani kwa mujibu wa ilivyobainishwa na asiwe naye, nini afanye?

 

Aliyewajibikiwa na umri fulani na asiwe naye kati ya ngamia wake, huyo anaweza kutoa ngamia mwenye umri wa chini yake anayefaa na kutosheleza kwa Zakaah. [Ni kwa mpangilio huu: binti makhaadh, kisha binti labuwn, kisha al-hiqqah, halafu jadha‘a]

 

Na kujazilia upungufu huo, atampa mkusanyaji Zakaah mbuzi wawili au dirhamu 20. Makusudio ya dirhamu hizi ni kujazilia thamani ya mbuzi wawili.

 

Au anaweza kutoa umri wa juu zaidi lakini atachukua kutoka kwa mkusanyaji Zakaah mbuzi wawili au dirhamu 20. Hii ni kwa kila mmoja aliyewajibikiwa na Zakaah.

 

Toka kwa Anas kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘anhu) alimwandikia fariydhwah ya Zakaah ambayo Allaah Alimwamuru Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Aliyefikiwa na Zakaah ya kutoa jadha‘a katika ngamia wake, naye hana jadha‘a bali hiqqah, basi itakubaliwa atoe hiqqah, na watatolewa pamoja naye mbuzi wawili kama itakuwa wepesi kwake au dirhamu 20. Na aliyefikiwa na Zakaah ya kutoa hiqqah, naye hana hiqqah bali jadha‘a, basi itakubaliwa atoe jadha‘a lakini mkusanyaji Zakaah atampa dirhamu 20 au mbuzi wawili. Na aliyefikiwa na Zakaah ya kutoa hiqqah, naye hana bali binti labuwn, basi itakubaliwa atoe binti labuwn na atatoa juu yake mbuzi wawili au dirhamu 20. Na ambaye Zakaah yake imefikia binti labuwn naye hana, bali ana binti makhaadh, basi itakubaliwa atoe binti makhaadh na hutolewa pamoja naye dirhamu 20 au mbuzi wawili)). [Al-Bukhaariy (1453) na Ibn Maajah (1800)]

 

Inatoholewa kutokana na Hadiyth hii vile vile kuwa kama hakupata ngamia mwenye umri uliowajibikiwa Zakaah na badala yake akapata mkubwa zaidi kwa daraja mbili au mdogo zaidi kwa daraja mbili basi atamtoa, na tofauti ya ujazilio itakuwa dirhamu 40 na mbuzi wanne, na kuendelea.

 

Lakini inatolewa nje ya wigo wa qaaidah iliyotangulia katika hali hii: Ikiwa amewajibikiwa kumtoa binti makhaadh, na hakuwa na ibnati labuwn bali ana ibn labuwn dume, basi itamtosheleza kutoa binti makhaadh bila ya kutoa cha ziada au yeye kuchukua kitu. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Anas pia katika barua ya Abu Bakr kwa amri ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na Zakaah. Inasema:

((فإن لم يكن عنده بنت مخاض على وجهها، وعنده ابن لبون، فإنه يقبل منه وليس معه شيء))

((Kama hana binti makhaadh mwenye umri mwafaka lakini ana ibn labuwn, basi hukubaliwa na yeye hana chochote)). [Al-Bukhaariy (1448) na An-Nasaaiy (2447).

 

Je, itamtosheleza kutoa zaidi ya inavyomwajibikia?

 

Kutoa zaidi ya cha waajib kuna hali mbili:

 

Ya kwanza: Ni mtoaji Zakaah kujitolea tu kwa khiyari yake, akatoa ngamia mwenye umri mkubwa zaidi ya umri wa waajib. Ni kama kumtoa binti labuwn, au hiqqah, au jadha‘a badala ya binti makhaadh. Hili linajuzu bila mvutano wowote. [Al-Mughniy (2/582) na Naylul Awtwaar (4/161)]

 

Dalili yake ni Hadiyth ya Ubayya bin Ka’ab. Inasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aliyetoa ngamia jike mkubwa aliyenona, naye kawajibikiwa kutoa binti makhaadh katika ngamia wake- :

((ذاك الذي عليك، وإن تطوعن بخير قبلناه منك، وآجرك الله فيه))

((Yule ndiye unayepaswa kumtoa, lakini ukijitolea cha ziada kwa khiyari yako, basi tunakikubali kutoka kwako, na Allaah Atakulipa kwacho)). [Abu Daawuud (1583), na Ahmad (5/14 3) na Sanad yake ni Hasan]

 

Ya pili: Atoe ngamia jike badala ya mbuzi, na pia kwenye idadi iliyolazimu kutoa mbuzi (yaani ngamia walio chini ya 25). Hili lina mvutano:

 

Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy, wanasema itamtosha.  Maalik anasema hilo ndio sahihi zaidi. Lakini Hanbali anasema haimtoshelezi kwa kuwa amemtoa mwingine asiyetajwa kwenye Hadiyth na asiye wa kundi lake. [Al-Mughniy (2/578) na Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/154)]

 

Na wengine wameunga mkono kauli ya Jumhuri ambayo pengine ndiyo yenye nguvu zaidi. [Al-Inswaaf (3/49)]

 

Sababu ni kuwa (Allaah) Mpangaji sharia Hakufaradhisha ngamia (kutolewa Zakaah) kwa idadi ya chini ya ngamia 25 ili kumfanyia takhfiyf mmiliki, kwani haikubaliki kiakili binti makhaadh atosheleze katika ngamia 25 na asitosheleze katika ngamia 20! [Ash-Sharhu Al-Mumtií]

 

 

Share