18-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Mazao Na Matunda

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

18-Zakaah Ya Mazao Na Matunda

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Zakaah ya mazao na matunda ni lazima katika ujumla wake. Ulazima wake umethibiti katika Qur-aan, Sunnah na Ijma’a, ingawa Fuqahaa wamekhitilafiana katika uchambuzi wake. [Badaai‘u As-Swanaai (2/54)]

 

Dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah zitakuja mbeleni tukiendelea kulichambua suala hili.

 

Mazao Na Matunda Ambayo Ni Lazima Yatolewe Zakaah

 

‘Ulamaa wamekubaliana wote kuwa ni lazima kutoa Zakaah katika aina ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alizichukulia Zakaah ambazo ni ngano, shayiri, tende na zabibu kavu. Lakini wamekhitalifiana kuhusu aina zingine ambazo hazikugusiwa. Kauli zao kiujumla ni hizi zifuatazo:

 

1- Hakuna Zakaah isipokuwa katika aina hizi hizi nne, na zisizo hizi, hakuna Zakaah

 

[Al-Muhalla (5/209) na kurasa zinazofuatia, Naylu Al-Awtwaar (4/170), Al-Amwaal cha Abiy ‘Ubayd (469/1378), Tamaam Al-Minnah (uk. 372-373) na Fiqh Az Zakaah (1/377)]

 

Haya ni madhehebu ya Ibn ‘Umar([1]), Al-Hasan Al-Baswriy([2]), Ath-Thawriy, Ash-Sha’abiy, Ibn Siyriyn, Ibn Al-Mubaarak, Abu ‘Ubayd na Masalaf wengineo. Ni riwaya toka kwa Ahmad. Pia ni madhehebu ya Ibn Hazm isipokuwa Hadiyth ihusianayo na zabibu kavu, si swahihy kwa upande wake, na hakuizungumzia. Kadhalika, ni madhehebu ya Ash-Shawkaaniy kisha Al-Albaaniy.

 

Dalili za wenye kauli hii ni:

 

- Yaliyosimuliwa toka kwa Abu Burdah toka kwa Abu Muwsaa na Mu’aadh kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipowatuma kwenda Yemen –ili kuwafundisha watu diyn yao –aliwaamuru wasichukue Zakaah isipokuwa kwa mazao haya manne tu: Ngano, shayiri, tende na zabibu kavu. [Al-Haakim (1/401) na Al-Bayhaqiy (4/125). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Swahiyhah (879)]

 

Na kwa vile mazao na matunda mengine yasiyo haya manne hayakutajwa na Aayah wala Hadiyth wala Ijma’a wala hata vinavyofanana navyo kwa ukaribu katika vyakula vinavyoliwa zaidi, uwepo wake na manufaa yake mengi, hivyo basi, haitofaa kuvifanyia vipimo juu ya mazao tajwa, wala kuvinasibisha nayo. Hivyo yanabakia katika asili yake.

 

Pia, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wakati alipoyaainisha mazao haya manne kwa Zakaah na kuyakataa mengine, alikuwa anajua kwamba watu wana vyakula vinginevyo na mali katika vinavyotolewa na ardhi. Hivyo kuviacha na kuvikataa ni msamaha kutoka kwake kama alivyosamehe Zakaah ya farasi na watumwa.

 

2- Zakaah hutolewa kwa kila kinacholiwa na kuhifadhiwa

 

[Al-Muwattwa (1/276 chapa ya Al-Halabiy), Al-Muhaddhab (5/493), na Fiqhu Az Zakaah (1/378)]

 

Ni madhehebu ya Maalik na Ash-Shaafi’iy.  Vinavyoliwa ni vile ambavyo watu wanavitumia kwa utashi wao katika mazingira ya kawaida na si katika hali ya kulazimika. Ni kama ngano, shayiri, mahindi, mchele na mfano wake. Si lazima kutoa Zakaah ya jozi (walnut), lozi, fistiki (pistachio) na mfano wake. Hivi hata kama vinahifadhiwa, lakini si vyakula vya lishe na shibe kwa watu.

 

Dalili za wenye kauli hii ni Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal ikisema: ((Ama matango, matikiti maji, makomamanga, miwa na mboga, hivi amevisamehe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (4/129), Al-Haakim (1/558) na Ad-Daaraqutwniy (2/97). Angalia At-Talkhiysw (837)]

 

Na kwa vile vyakula manufaa yake ni makubwa, vinakuwa kama wanyama wa mifugo.

 

3- Zakaah ni kwa kila kinachokauka, kinachobakia na kinachopimika [Al-Mughniy (2/690), Sharhu Muntahaa Al-Iraadaat (1/388) na Fiqh Az Zakaah (1/381).

 

Ni katika riwaya mashuhuri zaidi toka kwa Ahmad. Hapa zinaingia nafaka na matunda yanayopimwa na kuhifadhiwa, na nafaka zinazohifadhiwa nyumbani kama fuli (jamii ya maharagwe), njegere, adesi n.k. Pia tende, zabibu kavu, lozi, fistiki na kadhalika kwa kuwa zote zina sifa moja.

 

Hakuna Zakaah katika matunda mengineyo kama jozi, matufaha na mfano wake, au mboga mboga.

 

Dalili za wenye kauli hii ni:

 

1- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((ليس فيما دون خمسة اوسق صدقة))

((Hakuna chini ya “wasq” tano [pishi 300] Zakaah)). [Al-Bukhaariy (1447) na Muslim (979)]

 

Wanasema kwenye Hadiyth pamezingatiwa ufunganyaji, hivyo inadulisha kuwa Zakaah inakuwa kwa vinavyofunganywa na kupimwa.

 

[Wasq 1 = pishi 60. Pishi 60 × wasq 5 = pishi 300. Pishi 1 = kilo 2.175. Hivyo, kiwango cha Zakaat ni takriban kilo 653 kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Wengine wanasema pishi moja ni sawa na kilo 3, na kiwango cha Zakaah ni kilo 900]

 

2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((ليس في حب ولا تمر صدقة حتى يبلغ خمسة أوسق))

((Hakuna Zakaah katika nafaka wala tende mpaka zifikie wasq tano)). [Muslim (979) na An-Nasaaiy ( 2485).

Wanasema: Hii inadulisha kuwa ni lazima kutoa Zakaah ya nafaka na tende, na si lazima kwa visivyo viwili hivyo. Ibn Taymiyyah amekhitari kuwa kinachozingatiwa ni kuhifadhika mazao na si vinginevyo, kwa kuwepo maana mwafaka ya kuwajibisha Zakaat ndani yake kinyume na mizani, kwani ni ukadiriaji tu na uzito katika maana yake.

 

4- Zakaah ni kwa kila kinachooteshwa na ardhi katika vinavyolimwa na mwanadamu [Al-Muhallaa (5/212), Al-Hidaayah (2/502), na ‘Aaridhwat Al-Ahwadhiy (3/135)]

 

Ni kauli ya ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz, na madhehebu ya Abu Haniyfah na Daawuwd Adh-Dhwaahiriy. Ibn ‘Arabiy ameitilia nguvu na amejikita sana katika kuiunga mkono, na Al-Qaradhwaawiy ameikhitari.

 

Hoja za mwelekeo wao huu ni:

 

1- Ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ))

((Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi)). [Al-Baqarah (2:267)]

 

Wamesema: Hakutofautisha kati ya vinavyotokana na chumo la mtu au vinavyotolewa na ardhi.

 

2- Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ))

((na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake)). [Al-An’aam (6:141)]

 

Na hii ni baada ya kutaja aina za vyakula vya mashamba, mitende, mimea, zaituni na makomamanga.

 

3- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((فيما سقت السماء العشر، وفيما سقي بالنضح نصف العشر))

((Kwa yaliyonyeshelezewa na mvua 10%, na yaliyonyeshelezwa kwa mnyama 5%)).

 

Wamesema: “Hapa hakupambanua kati ya kinachofanywa chakula na kisichofanywa chakula, au kinacholiwa na kisicholiwa, au kinachohifadhika na kisichohifadhika”.

 

Ibn Al-‘Arabiy amesema: “Madhehebu yenye nguvu zaidi kwa upande wa dalili kuhusiana na suala hili, ni madhehebu ya Abu Haniyfah. Yamewatizama zaidi masikini, yanawezesha zaidi kuishukuru Neema ya Allaah, na yanadulisha ujumuishi wa Aayah na Hadiyth”.

 

Na hawa wameziponda Hadiyth zilizoifunga Zakaah ndani ya aina hizi nne tu wakisema kuwa ikiwa tutajaalia kuwa ni Hadiyth Swahiyh, basi zitafasiriwa kwa maana kuwa hakukuwa wakati huo na mazao mengine zaidi ya haya manne?

 

Zakaah ya mazao na matunda si lazima ipitiwe na mwaka

 

Hakuna sharti ya kupitiwa na mwaka katika Zakaah ya mazao na matunda kwa makubaliano ya ‘Ulamaa kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِه))

((na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake)). [Al-An’aam (6:141)]

 

Kwa kuwa kinachovunwa ni barakah na kheri katika dhati yake, hapo imewajibika kutolewa Zakaah kinyume na mali nyinginezo za Zakaah. Mali hizo ni sharti zipitiwe na mwaka ili ziweze kuwekezwa. [Al-Mughniy (6/696)]

 

Ni wakati gani Zakaah ya mazao na matunda inakuwa waajib? Wakati gani hutolewa?

 

Zakaah inakuwa waajib wakati mazao yanapoonekana yamekomaa na punje kuwa ngumu, kwa kuwa katika hali hiyo, punje zinakuwa ni chakula. Punje kabla ya kufikia hali hii zinakuwa ni changa na haziliki. Ni waajib pia wakati mwaka unapokamilika, au tende (tamr) na zabibu kubadilika rangi, nazo kabla ya kugeuka rangi, zinakuwa ni tende mbichi “balah” au “haswram”, na zabibu mbichi.

 

Ama wakati wa kutolewa Zakaah yake, kwa nafaka, inakuwa ni baada ya kupukuchwa na kutolewa maganda. Ama kwa matunda, inakuwa ni baada ya kukaushwa, kwa kuwa huo ndio wakati wa ukomavu kamili na uwezekaniko wa kuhifadhiwa.

 

Na ikiwa mazao yataharibika kabla ya kuwajibikiwa na Zakaah, yaani kabla ya kukomaa, basi Zakaah husamehewa. Na kama yataharibika baada ya kukomaa lakini kabla ya kuhifadhiwa na kuwekwa ghalani, basi hakuna dhamana juu yake. [Al-Mughniy (2/702) na Sharhu Muntahaa Al-Iraadaat (1/390)]

 

Je, ni lazima mazao na matunda yafikie kiwango? Kiwango chake ni kiasi gani?

 

Ili Zakaah iwe waajib, ni lazima ifikie kiwango kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Kiasi chake ni “wasq”tano  za nafaka safi zilizopembuliwa.

 

Hii ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((ليس فيما دون خمسة اوسق صدقة))

((Hakuna chini ya wasq tano [pishi 300] Zakaah)). [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kipimo hiki ni sawa na “kaylah” 50 za Kimisri. [Fiqhu Az Zakaah (1/400)] Ni sawa na “irdabu” 4 1/6 . Ni sawa vile vile kujaza chombo chenye ujazo wa takriban kilo 647 za ngano.

 

Ikiwa mavuno yatapungua chini ya uzito huu, basi Zakaah si lazima kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. Kati yao ni maswahibu wawili wa Abu Haniyfah. Lakini Abu Haniyfah amewajibisha Zakaah kwa kidogo na kingi akitolea dalili ujumuishi wa Hadiyth isemayo:

(( فيما سقت السماء العشر))

 

((Kwa yaliyonyeshelezewa na mvua 10%)).  [Takhriyj yake itakuja mbeleni kidogo]

 

Na kwa kuwa yeye hazingatii kupitiwa na mwaka, na hata kiwango pia hakizingatii.

 

Lakini Hadiyth: ((Hakuna chini ya wasq tano [pishi 300] Zakaah)), haijuzu ipingane na Hadiyth iliyotangulia [Kwa yaliyonyeshelezewa na mvua 10%], kwa kuwa hii ni khususi, muhkam (inafahamika bila utata) na  iwazi, na ile ni jumuishi, ni mutashaabah (tata inayohitaji kubainishwa), na mujmal (yenye maana mchanganyo). Hii inabainisha kiwango, na ile bila shaka imekusudiwa kwayo kupambanua kati ya ambayo ni wajibu kutolewa asilimia 10 na ambayo ni wajibu kutolewa asilimia 5. Hivyo hakuna ukinzano kati yao.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Vipi kinakadiriwa kiwango cha zao lisilopimika kwa wenye kuwajibisha Zakaah kwa zao hilo?

 

Zao lisilokadiriwa kwa kupimwa kama pamba mfano, -kwa wenye kusema ni wajibu litolewe Zakaah– ukadiriaji wa kiwango chake umekhitalifiwa kwa kauli mbalimbali: [Angalia Fiqh Az Zakaah (1/401)]

 

1- Itaangaliwa thamani. Ikiwa thamani yake itafikia karibu sana na kiwango cha mazao yanayofungashwa, basi Zakaah itatolewa. Kama haikukurubia, basi haitolewi.

 

2- Kitaangaliwa kiwango cha pesa.

 

3- Kiwango hakiangaliwi, bali Zakaah itatolewa kwa kichache chake na kingi chake.

 

4- Kitakadiriwa kwa uzito uliotajwa nyuma ambao ni kilo 647.

 

Kauli ya tano imetiliwa nguvu na Ibn Qudaamah katika Al-Mughniy (2/697). Amesema akiziandamiza kauli nyingine: “Sijui dalili yoyote wala asili yoyote ya kutegemewa juu ya kauli hizi. Zinanyamazishwa na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam): ((Hakuna chini ya wasq tano [pishi 300] Zakaah)).

 

Al-Qaradhwaawiy amekhitari kauli ya kuangalia thamani.

 

Je, mavuno yanaweza kuwekwa pamoja ili kukamilisha kiwango?

 

Kauli imara zaidi ya ‘Ulamaa inasema kuwa mazao ya jamii moja huwekwa pamoja yenyewe kwa yenyewe, lakini ya aina tofauti hayachanganywi. Ngano haichanganywi na shayiri na mfano wa hilo, wala nafaka zinazohifadhiwa nyumbani hazichanganywi pamoja. Dengu haichanganywi na adesi na mfano wa hilo. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/511-513)]

 

Haya ni madhehebu ya Jumhuri ya Masalaf.

 

Ama aina mbalimbali za ngano, hizi huchanganywa zenyewe kwa zenyewe, pia shayiri hivyo hivyo, na tende kadhalika kwa aina zake tofauti na majina yake tofauti hata kama mashamba anayoyamiliki mtu yakawa yametengana huku na kule. [Al-Muhallaa cha Ibn Hazm (5/253)]

 

Kuna ‘Ulamaa waliojuzisha kuchanganya ngano na shayiri, na kuchanganya nafaka zinazohifadhiwa nyumbani kwa chakula kama fuli, dengu, adesi, njegere na mfano wake ili kukamilisha kiwango kutokana na mkusanyo wake. Haya ni madhehebu ya Maalik, riwaya toka kwa Ahmad, na Sheikh wa Uislamu ameikhitari kauli hii. [Al-Mughniy (2/560), Al-Mudawwanah (1/288), na Majmuw’u Al-Fataawaa (25/23-24)]

 

Ninasema: “Lakini, kauli hii, sijui dalili yoyote ya kuithibitisha. Yenye nguvu zaidi ni ya kwanza. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”

 

Je, mavuno ya mwaka mmoja hukusanywa pamoja kukamilisha kiwango?

 

Ikiwa mtu ana shamba, na baadhi ya mazao yake huvunwa mapema na mengine baadaye, mazao haya yatachanganywa ili kukamilisha kiwango madhali ni mwaka huo huo. Ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Majmu’u Al-Fataawaa (25/23). Angalia Al-Mughniy (2/733)]

 

Lakini hili tunalifungamanisha na masharti yaliyotangulia ya kuwa mazao yawe ya aina moja. Ama matunda ya miaka miwili, haya hayachanganywi.

 

Ukisiaji wa mavuno ya mitende na mizabibu

 

Matunda yanapoanza kukomaa, kiongozi wa nchi anatakiwa atume mtaalamu wa kukadiria kiasi cha mavuno baada ya kukauka matunda ili kiasi cha Zakaah kijulikane kwa wenye mashamba na kisha awajulishe. Atawakhiyarisha kati ya kuyahifadhi mpaka yakauke, au kula sehemu ya matunda hayo –yakiwa bado mabichi– na kuchunga haki ya masikini. Kama mwenye shamba atachagua kuyahifadhi mpaka yakauke, basi wakati huo atawajibikiwa Zakaah ya matunda aliyoyahifadhi yakiwa mengi au kidogo. Na kama atachagua –mwenye shamba- kula sehemu ya matunda hayo, basi atatoa fungu la masikini kwa mujibu wa hesabu ya makadirio.

 

Toka kwa Abu Hamiyd As Saa’idiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu): ((Tulipigana vita vya Tabuk pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Alipofika Waadiy Al-Quraa, alimkuta mwanamke kwenye shamba lake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akawaambia Swahaba wake: Kisieni mavuno. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akakisia “wasq” kumi. Akamwambia: Dhibiti hesabu (ya mavuno) yatakayotoka humo…. Alipofika Waadiy Al-Quraa alimwambia mwanamke yule: Shamba lako limetoa mavuno kiasi gani? Akasema: Wasq kumi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikisia mavuno)). [Al-Bukhaariy (1482) na Muslim (1392)]

 

Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam)  alikuwa anamtuma ‘Abdullaah bin Rawaaha kwenda kufanya makisio ya mitende wakati matunda yanapoanza kupata utamu kabla ya kuliwa, kisha huwakhiyarisha Mayahudi: (Ima) mitende (yote) iwe yao kwa mujibu wa makisio hayo [lakini wadhamini fungu la Waislamu], au wawaachie (yote Waislamu) kwa mujibu wa makisio hayo [lakini Ibn Rawaaha atawadhaminia kiasi cha fungu lao] ili aidhibiti Zakaah kabla matunda hayajaliwa na kutawanywa)). [Abu Daawuwd (1606), Abu ‘Ubayd katika Al-Amwaal (483/1438), Al-Bayhaqiy (4/123) na Ahmad (8/163). Ni Hadiyth Hasan Lishawaahidihii kama ilivyo katika Al-Irwaa (805)]

 

Je, inajuzu kula mazao kabla ya kuvuna? Je, yaliyoliwa hutiwa hesabuni?

 

Mwenye shamba anaruhusiwa kula chochote toka shambani mwake kiasi anachohitaji kabla ya kuvuna, na pia anaweza kutoa swadaqah kutoka humo wakati wa kuvuna, na haya hayatiwi hesabuni. Atakachotoa Zakaah ni kile kitakachopembuliwa baada ya hapo, kwa kuwa Zakaah haiwi waajib mpaka pale mazao yanapoweza kupimwa. Kwa hiyo, kilichotoka kabla ya hapo, kinakuwa kimetoka kabla ya kuwajibikiwa Zakaah.

 

Haya yamesemwa na Ash-Shaafi’iy, Al-Layth na Ibn Hazm. [Al-Muhallaa (5/259)]

 

Ni kiasi gani cha Zakaah ya mazao na matunda hutolewa kama yakifikia kiwango?

 

Kiasi cha Zakaah ya mazao na matunda hutofautiana kwa kutofautiana njia za umwagiliaji. Yaliyomwagiliwa bila kutumia zana za umwagiliaji (au wanyama), hayo yatatolewa moja ya kumi (yaani 10%). Ama yaliyomwagiliwa kwa zana, au kwa maji ya kununua, basi yatatolewa nusu ya kumi (moja ya ishirini au 5%).

 

Na dalili ya hili ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

 ((فيما سقت السماء والعيون أو كان عثريا العشر، وفيما سقي بالنضح نصف العشر))

((Kwa yaliyomwagiliwa na mvua na chemchemu, au ikawa mitende iyfonzayo yenyewe maji toka chini, ni moja ya kumi [10%], na kwa yaliyomwagiliwa kwa mnyama ni nusu ya kumi [5%])). [Al-Bukhaariy (1483), Abu Daawuwd (1581), At-Tirmidhiy (635), An-Nasaaiy (5/41) na Ibn Maajah (1817)].

 

2- Hadiyth ya Jaabir toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

(( فيما سقت الأنهار والغيم: العشور، وفيما سقي بالسانية: نصف العشور))

((Kwa yaliyomwagiliwa kwa mito na mvua, ni moja ya kumi, na katika yaliyomwagiliwa kwa ngamia, ni nusu ya kumi)). [Muslim (981), Abu Daawuwd (1582) na An-Nasaaiy (5/42).

 

Na ikiwa shamba litamwagiliwa nusu yake kwa gharama na nusu yake nyingine bila gharama, basi Zakaah ni robo tatu ya kumi (7.5%) kwa makubaliano ya Jumhuri.

 

Na ikiwa eneo moja limemwagiliwa zaidi ya jingine, basi Jumhuri wanalizingatia lililomwagiliwa zaidi, na hukmu ya uchache huondoka. Wengine wamesema kila eneo kati ya mawili litaangaliwa kivyake.

 

Na kama hakujua kiasi kilichozidi, atatoa moja ya kumi kiakiba, kwa kuwa wajibu wa moja ya kumi ndio asili, nao hupomoka kwa kuwepo gharama. [Angalia Al-Mughniy (2/699)]

 

Je, gharama, masurufu ya ulimaji na madeni hutolewa kando kisha kinachobaki hutolewa Zakaah?

 

1- Madeni anayokuwa nayo mkulima wa mazao au matunda hayakosi moja ya mawili:

 

La kwanza:

 

Awe amekopa kwa ajili ya kugharamia shughuli ya ulimaji kama kununua mbegu, mbolea, malipo kwa vibarua na kadhalika. Madeni haya yatatolewa kando kutokana na kitakachopatikana shambani, na kinachobakia kitatolewa Zakaah. Haya ni madhehebu ya Ibn ‘Umar, na kundi la Masalaf akiwemo Sufyaan Ath-Thawriy, Yahyaa bin Aadam na Imaam Ahmad.

 

La pili:

Awe amekopa kwa matumizi yake binafsi na familia yake. Ibn ‘Umar anaona kuwa deni litalipwa, kisha kinachobakia atatoa Zakaah.

 

Ama Ibn ‘Abbaas, yeye anaona kuwa deni lake halitotolewa toka nje isipokuwa kama alilitumia kugharamia matunda yake kama ilivyotangulia.

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: ((Ataanza kwa alichokopa alipe, kisha atoe Zakaah kilichobakia)).

 

Ibn ‘Abbaas amesema: ((Atalipa alichotumia kugharamia matunda, kisha atatoa Zakaah kilichobakia)). [Abu ‘Ubayd amekhariji kutoka kwao wawili katika Al-Amwaal (uk. 509), na Yahyaa bin Aadam katika Al-Khuraaj (uk. 162) kwa Sanad Swahiyh]

 

Kuna riwaya mbili zimepokelewa toka kwa Imaam Ahmad.

 

Abu ‘Ubayd ametilia nguvu madhehebu ya Ibn ‘Umar na waliokubaliana naye ya kulipa kwanza madeni yote ya nje, kwa kuwa mwenye kudaiwa, mali yake huzingirwa na deni lake, na hapo anakuwa ni katika watu wanaostahiki kupewa swadaqah (Zakaah), basi vipi atoleshwe Zakaah na yeye ni katika watu wanaostahiki kupewa? Vipi awe tajiri na masikini kwa wakati mmoja? [Al-Amwaal cha Abu ‘Ubayd (uk. 510)]

 

Ninasema: “Kauli hii ndio yenye nguvu zaidi. Na kwa muktadha wake, ikiwa mtu shamba lake limetoa “wasq” 20 za ngano kwa mfano [pishi 1200], na anadaiwa pesa sawa na thamani ya “wasq” 17, basi atatoa “wasq” 17 kulipia deni na atabakiwa na “wasq” 3 ambazo zitakuwa hazina Zakaah, kwa kuwa ni chini ya kiwango. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

2- Ama gharama za ukulima ikiwa hazitokani na deni

 

Ni kama gharama za mbegu, mbolea, kulima ardhi, uvunaj na mfano wake. ‘Ulamaa katika hili wana kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Hazitolewi toka kwenye mazao yaliyopatikana kabla ya kuchukuliwa moja ya kumi au nusu yake. Ni madhehebu ya Hanafiy na Ibn Hazm. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyn (2/49), Fat-hul Qadiyr (2/8-9) na Al-Muhallaa (5/258)]

 

Wamesema kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alichukulia tofauti ya cha wajibu (10% au 5%) toka tofauti ya gharama. Na kama gharama zitaondoshwa, basi cha wajibu kingekuwa kwa kiasi hicho hicho, kwa kuwa hakikuteremsha 10% hadi nusu yake isipokuwa gharama. Na fardhi ni chenye kubakia baada ya kutoa kiasi cha gharama, na si gharama zikiwa ndani.

 

Ya pili:

 

Hutolewa toka kwenye mazao yaliyopatikana na kinachosalia hutolewa Zakaah. Ni madhehebu ya Hanbali ambayo yameungwa mkono na Ibn Al-‘Arabiy. [Al-Mughniy (2/698), na ‘Aaridhwat Al-Ahwadhiy (3/143)]

 

Na hili ndilo lenye nguvu zaidi na lililo karibu zaidi na roho ya sharia, nalo linaungwa mkono kwa mambo mawili: [Fiqhu Az Zakaah (1/424)]

 

1- Ni kuwa gharama na matumizi yana athari. Gharama zinaweza kupunguza kiwango cha wajibu kama kumwagilia kwa mashine, na pia zinaweza kuzuia kabisa Zakaah kama kwa wanyama wanaolishwa majani kipindi kikubwa cha mwaka. Hivyo hakuna ajabu ya kupomosha kilicho mkabala wake katika kinachopatikana toka kwenye ardhi.

 

 2- Ni kuwa ustawi wa kitu ni kuongezeka na kuzidi. Mali haiwezi kuhesabiwa kuwa imeongezeka na kuwa na faida ikiwa itatumiwa mfano wake ili kuipata.

 

Ardhi Ni Aina Mbili: “’Ushariyyah” (Ya Moja Ya Kumi) Na “Kharaajiyyah” (ya kodi)

 

“’Ushariyyah” ni ardhi ambayo wamiliki wake wamesilimu kwa khiyari yao wenyewe, au ni ardhi iliyokombolewa kwa nguvu (ya silaha) na kugawanywa kwa wakombozi, au ni ardhi ambayo Waislamu wameifufua.

 

Na “Kharaajiyyah” ni ardhi iliyokombolewa kwa nguvu kisha wakaachiwa wamiliki wake waendelee kuimiliki bila kugawanywa ngawira kwa wakombozi, au wamiliki hao wakakubalishwa wailipie kodi maalum kwa mkabala wa kuachiwa waitumie.

 

Kodi hii ni ya aina mbili:

 

1- Kodi Kazi: Ni kodi inayotoleshwa kwa ardhi, ni sawa mmiliki wake ameitumia kuzalisha au hakuitumia. ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliitolesha na kuitumia.

 

 

2- Kodi Mgawano: Ni kodi inayokatwa kutokana na mazao yaliyopatikana. Ni kama kuchukuliwa nusu ya mazao, au theluthi yake, au robo yake. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alilifanya hilo alipoikomboa Khaybar.

 

Zakaah Ya Mazao Yanayotoka Kwenye “’Ardhi Kharaajiyyah”

 

Ardhi Kharaajiyyah ikitoa mazao yanayofikia kiwango cha waajib wa Zakaah, Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema kuwa italipwa kwanza kodi, kisha yaliyobakia yatatolewa Zakaah. Dalili zao ni:

 

1- Ujumuishi wa Aayaat na Hadiyth zilizotangulia zinazodulisha uwajibu bila kubagua kati ya ‘Ushariyyah na Kharaajiyyah.

 

2- Barua ya ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz aliyomwandikia ‘Abdullaah bin ‘Awf –aliyempa kazi ya kusimamia Palestina- kuhusiana na mwenye ardhi pamoja na jizya yake kati ya Waislamu: achukue jizya yake, kisha achukue kutoka humo Zakaah ya kilichobakia baada ya kutolewa jizya (yaani kodi). [Al-Amwaal cha Abu ‘Ubayd (uk. 88)]

 

3- Toka kwa Sufyaan Ath-Thawriy akisema kuhusu mazao yaliyotoka kwenye ardhi kharaajiyyah: ((Toa deni lako na kodi yako, na ikiwa itafikia “wasq” tano baada ya hapo, basi toa Zakaah)). [Al-Kharaaj cha Yahyaa bin Aadam (uk. 163)]

 

4- Ni kuwa kodi na moja ya kumi ni haki mbili zenye kutofautiana kidhati, kimahala, kisababu, kistahikivu na kidalili. Mahanafi wamekwenda kinyume katika hili, wakazuia kujumuika pamoja kodi na moja ya kumi katika ardhi moja. Wametoa dalili kwa Hadiyth baatwil isemayo:

 

((Moja ya kumi (‘ushru) na kodi (kharaaj) hazikutani katika ardhi ya Muislamu)). [Al-Kaamil cha Ibn ‘Uday (7/2155)].

 

Ibn Hibaan amesema Hadiyth hii si katika maneno ya Rasuli. Na Sheikh wa Uislamu amesema (25/55) ni uongo kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wa Hadiyth.

 

Kauli ya Jumhuri ndiyo yenye nguvu Zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. 

 

Vipi itatolewa Zakaah ya mazao yaliyopatikana toka ardhi iliyokodishwa? Nani atatoa, mwenye ardhi au mkodishiwa?

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa (Maalik, Ash-Shaafi’iy, Hanbali na Maswahiba wawili wa Abu Haniyfah) wanasema kuwa aliyekodisha ardhi kisha akailima na kuipanda, yeye ndiye atakayetoa Zakaah.

 

Lakini Abu Haniyfah amesema kuwa mwenye ardhi atatoa moja ya kumi.

 

Nukta ya mzozano wao ni: Je, moja ya kumi ni haki ya ardhi au haki ya mazao? [Bidaayatul Mujtahid (1/239) na Majmu’u Al-Fataawaa (25/55)].

 

Ninasema: “Lililo bayana zaidi ni kuwa ‘ushru hiyo ni haki ya ardhi. Ni waajib kwa mkodishiwa na si kwa mwenye ardhi –kama wanavyosema Jumhuri- lakini hii ni baada ya kutolewa kodi ya kukodisha ardhi toka kwenye mazao, kwa kuwa inafanana zaidi na kodi ya ardhi”.

 

Kwa mfano, ikiwa kukodi ardhi ni pauni 20, na ardhi ikazalisha “irdabu” 10 za ngano, na kila irdabu moja ni sawa na pauni 5. Thamani ya mazao yaliyopatikana hapa itakuwa ni (10 × 5 = pauni 50). Hapa atatolea Zakaah irdabu sita tu (= pauni 30), na irdabu nyingine nne zitawekwa kando kulipia kodi ya ardhi. Na ikiwa irdabu sita zilizobakia hazikufikia kiwango, basi hazina Zakaah. [Fiqh Az Zakaah (1/430)]

 

Ama mmiliki wa ardhi, yeye atatoa Zakaah ya kodi ya ardhi yake kwa mujibu wa maelezo ya nyuma kuhusu Zakaah ya mishahara ya mwezi na mapato ya kazi.

 

Al-Qaradhwaawiy amekhitari mmiliki wa ardhi alipie Zakaah kile anacholipwa, nayo ni kodi anayoipokea kwa sharti ifikie kiwango kutokana na mazao yaliyopo.

 

Je, Asali Inatolewa Zakaah?

 

Katika suala hili, makundi mawili ya ‘Ulamaa yamekhitalifiana kati ya kutowajibisha na kuwajibisha, na kundi jingine limechukua msimamo wa kati na kati.

 

1- Jumhuri ya ‘Ulamaa akiwemo (Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ibn Abiy Laylaa na Ibn Al-Mundhir) wanasema asali haina Zakaah kwa sababu mbili:

 

(a) Hakuna khabar yoyote wala Ijma’a inayothibitisha uwajibu wa Zakaah kwa asali. Hadiyth ziko wazi kwa vitolewavyo Zakaah, na asali haimo.

 

(b) Asali ni kimiminika kitokacho kwa mdudu mfano wa maziwa. Na maziwa hayana Zakaah kwa Ijma’a.

 

2- Hanafi na Ahmad wanasema asali hutolewa Zakaah, na dalili yao ni mambo mawili:

 

(a) Baadhi ya athar zinazozungumzia hili. Ni kama Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa: ((Alichukua ‘ushru ya asali)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ibn Maajah, (1824) na Abu ‘Ubayd katika Al-Amwaal (497/1489). Sanad yake ni Dhwa’iyf].

 

Pia, imepokelewa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake amesema: ((Hilaal -Ahad Baniy Mut’aan- alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na moja ya kumi ya nyuki wake (asali yake). Alikuwa amemwomba (Rasuli) amlindie bonde lijulikanalo kama Salabah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamlindia bonde hilo. Na ‘Umar bin Al-Khattwaab alipotawala, Sufyaan bin Wahab aliandika kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akimuuliza kuhusiana na hilo. ‘Umar (Radhwiya Allaahu anhu) akaandika: Kama atakupa kama alivyokuwa anatoa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) moja ya kumi ya nyuki wake (asali yake), basi mlindie Salabah lake, na kama si hivyo, basi hao ni nyuki wa mvua anaila (asali yao) yeyote atakaye)). [Abu Daawuwd (1600), An-Nasaaiy (1/346) na wengineo kwa Sanad Swahiyh. Angalia Al-Irwaa (810)]

 

Ninasema: “Linalonibainikia mimi ni kuwa riwaya ya pili ndiyo iliyo sawa. Riwaya hii inaitia doa riwaya ya kwanza. Riwaya hii ya kwanza imepitia kwa Ibn Lahiy’ah na nyingine kwa njia ya ‘Amri bin Al-Haarith (anayeaminika, faqiyh na haafidh), na makhraji ni mamoja. Ibn Al-Qayyim –Rahimahul Laah- ameshangaza aliposema: Athar hizi zinatiana nguvu zenyewe kwa zenyewe, na makhraji zake ni nyingi. Njia zake zimetofautiana, mursali yake inatiliwa nguvu na musnadi yake?. [Zaad Al-Ma’aad (1/312].

 

Na hii tukijua kwamba kuna makhitalifiano katika riwaya nyingine kuhusu waswl yake na irsaal yake.

 

Na tukiftaridhi (assume) kuwa imethibiti na ni mawsuwlah, basi hakuna la kusema hapo, kwa kuwa linaloonekana ni kuwa moja ya kumi iliyochukuliwa toka kwenye asali haikuwa ni Zakaah, bali ilikuwa ni kwa mkabala wa lindo. Na kama ingekuwa ni Zakaah ya waajib, basi ‘Umar; Faqihi na Mweledi wa Hadiyth asingeikhiyarisha. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Al-Haafidh ameliashiria hili katika Al Fat-h (3/348), na kabla yake Ibn Zanjawiyya katika Al-Amwaal (1095), halafu Al-Khattwaabiy katika Ma’aalim As-Sunan (1/208), halafu nilimwona Al-Albaaniy katika Tamaam Al-Minnah (uk. 374) amekinaika na hili].

 

(b) Wamesema: “Asali inazalikana kutokana na maua ya miti, hupimwa na huhifadhika. Hivyo ni lazima kuitolea Zakaah kama nafaka na tende. Kwa kuwa pia gharama zake ziko chini kulinganisha na gharama za mazao na matunda”. [Zaad Al-Ma’aad]

 

Na hawa waliowajibisha Zakaah katika asali, wamewajibisha kutoa moja ya kumi. Mahanafi wameshurutisha kwenye asali inayotolewa Zakaah isiwe inatoka kwenye ardhi kharaajiyyah, na iwe inamilikiwa, lakini pia hawakuainisha kiwango chake, bali wanaona Zakaah itolewe kwa asali nyingi au kidogo.

 

Lakini Mahanbali wanasema kuwa kiwango cha asali ni “afraaq” kumi ambazo ni sawa na kilo 46.67.

 

Na Al-Qaradhwaawiy ametilia uzito kiwango kiwe ni “wasq” tano sawa na kilo 647.

 

3- Abu ‘Ubaydah amechukua msimamo wa kati na kati kama anavyoeleza katika Kitabu cha Al-Amwaal (uk. 506):

 

“Njia inayoshabihiana zaidi katika jambo lake, yaani asali, ni kuwa wamiliki wake wanaamuriwa kutoa Zakaah yake, na wanahimizwa juu ya hilo, na ni makruhu kwao kuzuia kuitoa, na hakuna dhamana  kwao ya kutopata madhambi ikiwa wataficha bila ya hilo kuwa ni faradhi kwao kama ulivyo uwajibu wa Zakaah ya ardhi na mifugo, kwa vile hakuna  Hadiyth Swahiyh iliyothibiti kuhusu asali kama ilivyothibiti kwa ardhi na mifugo”.

 

Ninasema: “Hili ndilo lenye nguvu zaidi kuwa Zakaah si wajibu katika asali lakini kheri haikosekani ikiwa itatolewa. Na kama ni waajib, basi mtu atakuwa ametekeleza wajibu wake na kusafisha dhima yake, na kama si waajib, basi ni swadaqah”.

 

Na kwa ajili hiyo, Ibn Muflih ambaye ni mtaalamu mbobezi zaidi wa Fiqh ya Sheikh wa Uislamu, alikuwa anaona kuwa hakuna Zakaah katika asali. [Al-Furuu (2/450)] 

 

 

[1] Abu ‘Ubayd amesimulia kwa Sanad Swahiyh (469/1378) toka kwa Ibn ‘Umar. Amesema kuhusu Zakaah ya mazao na matunda: “Ni ile inayotokana na tende, au zabibu kavu, au ngano, au shayiri”. Na mfano wa hivyo katika Musnad Ash-Shaafi’iy (656) kwa Sanad Swahiyh.

 

[2] Abu ‘Ubayd ameisimulia kutoka kwake (469/1379-1380), Ibn Zanjawiyyah (1030/1899) kwa Sanad zilizo Swahiyh kutoka kwake.

 

Share