23-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaatul Fitwr:

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

23-Zakaatul Fitwr

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Zakaatul Fitwr kiistilahi, ni Zakaah inayolazimu (kutolewa) kwa kumalizika Ramadhwaan.

 

Hikma Ya Kufaradhishwa Zakaatul Fitwr

 

Ni kuwafariji mafukara kwa kuwatosheleza wasiombe katika siku ya ‘Iyd, kuwapa furaha katika siku hii ambayo Waislamu hufurahi kwa kuingia ‘Iyd, na kumtakasa aliyewajibikiwa kuitoa baada ya Mwezi wa Swawm kutokana na upuuzi na “rafath” (matamanio ya jimai, mazungumzo yake, vitangulizi vyake na jimai yenyewe). [Al-Mughniy (3/56)]

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefaradhisha Zakaatul Fitwr, kwa ajili ya kumtakasa mfungaji kutokana na upuuzi na “rafath” (matamanio ya jimai, mazungumzo yake, vitangulizi vyake na jimai yenyewe), na kuwalisha masikini. Na atakayeitoa kabla ya Swalaah, basi hiyo ni Zakaah yenye kukubaliwa, lakini atakayeitoa baada ya Swalaah, basi hiyo ni swadaqah kati ya swadaqah nyinginezo)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1609), Ibn Maajah (1827) na wengineo kwa Sanad Hasan]

 

Hukmu Yake

 

Zakaatul Fitwr ni waajib kwa kila Muislamu kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefaradhisha Zakaatul Fitwr pishi ya tende, au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume au mwanamke, na mdogo na mkubwa katika Waislamu. Ameamuru itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1503), Muslim (984) na wengineo]

 

Sa’iyd bin Al-Musayyib na ‘Umar bin ‘Abdul ‘Azizy wamesema kuhusu Kauli Yake Ta’aalaa:

 

 

قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ

((Hakika amefaulu ambaye amejitakasa)),

kwamba makusudio ni Zakaatul Fitwr.

 

Ibn Al-Mundhir kasema: “Wote tunaowajua vyema katika ‘Ulamaa wamesema kwa sauti moja kuwa Zakaatul Fitwr ni fardhi”. [Al-Ijma’a cha Ibn Al-Mundhir (uk.9)]

 

Ni waajib kwa nani?

 

Zakaatul Fitwr ni waajib kwa mwenye masharti yafuatayo:

 

[1] Awe Muislamu

 

Kwa kuwa Zakaatul Fitwr ni ‘amali katika ‘amali za kujikurubisha mtu kwa Allaah, na ni kitwaharisho kwa mfungaji kutokana na “rafath” na upuuzi –kama ilivyotangulia- na kafiri hahusiki na haya bali ataadhibiwa Aakhirah kwa kuacha kutoa. Na kwa ajili hiyo, amesema katika Hadiyth iliyotangulia ya Ibn ‘Umar “katika Waislamu”. Uislamu ni sharti kwa Jumhuri ya ‘Ulamaa kinyume na Mashaafi’iy ambao la sahihi kwao ni kuwa ni lazima kwa kafiri aitoe kuwapa jamaa zake Waislamu. [Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/72) na Mughnil Muhtaaj (1/402)]

 

[2] Awe na uwezo wa kuitoa

 

Mpaka wa uwezo huu ni mtu kuwa na ziada katika mlo wake na mlo wa anaowakimu kimaisha usiku wa ‘Iyd na mchana wake kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa (Maalik, Ash-Shaafi’iy na Hanbali). [Mughnil Muhtaaj (1/403, 628) na Al-Mughniy (3/76)]

 

Hii ni kwa vile mtu ambaye hali yake iko hivi, anakuwa ni mwenye kujitosheleza, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii amesema:

 

((من سأل وعنده ما يغنيه فإنما بستكثر من النار)) فقالوا يا رسول الله، وما يغنيه؟ قال: ((أن يكون له شبع يوم وليلة))

((Mwenye kuomba naye ana [chakula] cha kumtosha, basi hakika anajikusanyia moto)). Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni kipi kinamtosha?Akasema: Awe na mlo wa kumshibisha mchana na usiku)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1629) kwa Sanad Hasan]

 

Abu Haniyfah na wenzake wamelikhalifu hili wakisema kuwa Zakaah haipasi isipokuwa kwa yule anayemiliki kiwango cha dhahabu na fedha (silver) au thamani yake mbali na nyumba yake. [Sharhu Fat-hil Qadiyr (2/218) na Haashiyatu Ibn ‘Aabidiyna (2/360)]

 

Wametoa dalili kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((لا صدقة إلا عن ظهر غنى))

((Hakuna swadaqah [iliyo kamili] isipokuwa inayotokana na mtu kuwa amejitosheleza)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1426)]

 

Wamesema: Fakiri hana cha kujitosheleza, hivyo si waajib kwake, na kwa kuwa Zakaah ni halali yeye kupewa, inakuwa si waajib kwake kutoa kama asiye na uwezo wa kuitoa.

 

Ninasema:

 

Rai ya Jumhuri ina uzito zaidi kwa mambo haya:

 

1- Kufaradhishwa Zakaatul Fitwr kumekuja kwa wote bila uainisho; kwa mdogo, mkubwa, mwanamume, mwanamke, muungwana na mtumwa. Haikufunganishwa na utajiri au umasikini kama ilivyofunganishwa Zakaatul Maal kwa neno lake Rasuli: ((Huchukuliwa toka kwa matajiri wao ikarejeshwa kwa mafukara wao)).

 

2- Zakaatul Fitwr haiongezeki kutokana na wingi wa mali ya mtu, hivyo uwajibu wa kiwango haupo ndani yake kama kafara.

 

3- Wao kutoa dalili kwa Hadiyth: ((Hakuna swadaqah [iliyo kamili] isipokuwa inayotokana na mtu kuwa amejitosheleza)) hakukubaliwi, na sisi tunasema pamoja nao: Asiyeweza kuitoa hawajibikiwi, bali tumeleta Hadiyth inayosema kuwa mwanadamu kinamtosheleza chakula cha kumshibisha mchana wake na usiku wake.

 

Faida

 

Zakaatul Fitwr ni waajib kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kuitoa hata kama ni mtumwa anayemilikiwa –kama walivyosema Mahanbali- kinyume na Jumhuri ya Fuqahaa. Fuqahaa hawa wameshurutisha mtu awe muungwana ili awajibikiwe na Zakaah. Wamesema kuwa si waajib kwa mtumwa, kwa kuwa mtumwa hamiliki kitu.

 

Lililo sahihi ni kuwa ni waajib kwa Muislamu anayemiliki mtumwa amtolee Zakaatul Fitwr mtumwa wake kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefaradhisha Zakaatul Fitwr pishi ya tende au pishi ya shayiri kwa kila mtumwa na muungwana, mdogo au mkubwa)). [Hadiyth Swahiyh. Imeshatajwa nyuma]

 

Kwa Muhtasari

 

Zakaatul Fitwr ni waajib kwa kila Muislamu aliye huru –anayemiliki chakula chake na chakula cha watoto wake mchana au usiku- ajitolee yeye mwenyewe na wale anaowakimu kimaisha kama mke wake, watoto wake na watumishi wake walio Waislamu. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar amesema: ((Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam ameamuru Zakaatul Fitwr kwa mdogo na mkubwa, muungwana na mtumwa katika mnaowalisha)). [Hadiyth Hasan Lighayrih. Imekharijiwa na Ad-Daaraqutwniy (220), na kwa njia yake Al-Bayhaqiy (4/161). Angalia Al-Irwaa (835)]

 

Ibn Hazm anaona kuwa Zakaatul Fitwr haimlazimu mtu kumtolea mwingine, si baba yake wala mama yake, wala mke wake, wala yeyote kati ya anaowalisha isipokuwa ajitolee yeye mwenyewe. Na hawa (wanaolishwa) ni waajib kila mmoja wao ajitolee mwenyewe kwa pesa zake kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyokubaliwa na wote.

 

Fawaaid

 

1- Si lazima mtu kumtolea Zakaatul Fitwr mkewe ambaye bado hajamwingilia kwa kuwa bado hajawajibikiwa kumlisha.

 

2- Ikiwa mke atamwasi mumewe katika wakati wa kutoa Zakaatul Fitwr, basi mke atajitolea Zakaah mwenyewe, na si mume.

 

3- Ikiwa mke ni Ahlul Kitaab (Myahudi au Mnaswara), basi hatolewi Zakaatul Fitwr.

 

Aina za vyakula vinavyotolewa katika Zakaatul Fitwr

 

Zakaatul Fitwr hutolewa kwa vyakula vinavyoliwa na Waislamu, si tu vile vilivyotajwa kwenye Hadiyth (shayiri, tende na zabibu), bali hutolewa mchele, mahindi, na mfano wake katika mazao yanayotumika kama vyakula.

 

Hii ni kauli swahiyh zaidi ya ‘Ulamaa, nayo ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Maalik. [Lakini wao wameshurutisha vyakula viwe katika mazao yanayotolewa 10% (moja ya kumi) ya Zakaah]

 

Na Sheikh wa Uislamu ameikhitari. Ama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kufaradhisha pishi ya tende au pishi ya shayiri, ni kuwa hivi ndivyo vilivyokuwa vyakula vikuu vya watu wa Madiynah. Na kama hivi visingekuwa vyakula vyao bali wanakula vingine, basi asingeliwakalifisha watoe wasichokila. Kama ambavyo hakuamuru hilo katika malipo ya kafara. Allaah Ta’aalaa Amesema kuhusu kafara:

مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ

((chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu)). [Al-Maaidah (5:89)]

 

Na Zakaatul Fitwr ni kundi moja na malipo ya kafara, zote mbili zina mahusiano na kiwiliwili kinyume na Zakaatul Maal.  Zakaatul Maal ni lazima kwa sababu ya mali itokanayo na aina ile ile ambayo Allaah Amemruzuku mtu. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/69)]

 

Ama Mahanbali, wao wamesema kuwa haitoshelezi isipokuwa tende, shayiri na burri.

 

Ni kiasi gani cha uwajibu anachotolewa kila mtu katika Zakaatul Fitwr?

 

‘Ulamaa wako katika madhehebu mawili kuhusiana na kiasi cha uwajibu anachotolewa kila mtu. [Al-Mudawwanah (1/358), Al-Majmuw’u (6/48), Al-Mughniy (3/81) na Sharhu Fat-hil Qadiyr (2/225)]

 

La kwanza: Wajibu ni pishi ya aina yoyote (ya chakula)

 

Hii ni kauli ya Jumhuri –kinyume na Abu Haniyfah na Maswahibu wake- na dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy aliyesema: ((Tulikuwa tunatoa Zakaatul Fitwr wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) yuko pamoja nasi, pishi ya chakula, au pishi ya shayiri, au pishi ya tende, au pishi ya zabibu kavu au pishi ya samli kavu ya maziwa. Na hatukuacha kuitoa (hivyo) mpaka alipokuja Mu’aawiyah Madiynah, akazungumza. Na kati ya aliyoyazungumzia kwa watu ni: Hakika mimi naona kwa uyakini vibaba viwili vya ngano ya Sham ni sawa na pishi ya tende, na watu wakalifuata hilo. [Abu Sa’iyd akasema]: Ama mimi, bado naendelea kuitoa kama nilivyokuwa naitoa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1505), Muslim (985), Abu Daawuwd (1616) na At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy]

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar: ((Kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifaradhisha Zakaatul Fitwr pishi ya tende, na pishi ya shayiri, na watu wakageuza na kutoa nusu pishi ya burri)). (Kutokana na ubora wa ngano ya Sham kulinganisha na ya Hijaaz). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1511) na Muslim (984)]  

 

La pili: Wajibu ni pishi isipokuwa katika burri ambayo inatosha nusu pishi

 

Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maswahibu wake. Zabibu kavu ni kama burri kwa Abu Haniyfah katika riwaayah. Na dalili zao ni:

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Tha’alabah toka kwa Abiy Swu’ayr toka kwa baba yake toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliyesema:

((صاع من بر أو قمح على كل اثنين))

((Pishi ya burri au ngano kwa kila wawili)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Abu Daawuwd (1619) kwa Sanad Swahiyh]

 

2- Toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimtuma mpiga mbiu kwenye barabara za Makkah atangaze:

((ألا إن صدقة الفطر واجبة على كل مسلم ذكر أو أنثى أو عبد، صغير أو كبير، مدان من قمح، أو سواهما صاع من طعام))

((Jueni kuwa Zakaatul Fitwr ni waajib kwa kila Muislamu; mwanaume au mwanamke, au mtumwa, mdogo au mkubwa, vibaba viwili vya ngano, au kama si vibaba viwili [vya ngano] pishi ya chakula)). [Hadiyth Dhwa’iyf. At-Tirmidhiy (669) kwa Sanad Layyin. Kuna makhitalifiano, angalia Tuhfat Al-Ahwadhiy (3/348)]

 

Al-Haafidh katika Al-Fat-h (3/437) amesema: “Ibnul Mundhir amesema: Hatujui habari yakini ya kutegemewa kuhusiana na ngano toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), na burri haikuwepo Madiynah wakati huo isipokuwa kiasi kidogo tu. Na ilipokuwa nyingi enzi ya Swahaba, waliona kuwa nusu pishi ya burri ni sawa na pishi moja ya shayiri, nao ndio Maimamu. Hivyo basi haijuzu kuiacha kauli yao ila tu kama mtu ataiacha na kuifuata kauli ya wengine mfano wao. Kisha imepokewa kwa Sanad Swahiyh toka kwa ‘Uthmaan, ‘Aliy, Abu Hurayrah, Jaabir, Ibn ‘Abbaas, Ibn Az Zubayr, na mama yake Asmaa bint Abiy Bakr kwamba wao wanaona ni nusu pishi ya ngano katika Zakaatul Fitwr….mpaka mwisho wa maneno”. [Maneno ya Ibn Al-Mundhir] Hatima hii imemfanya akhitari mwelekeo wa Hanafiy. Lakini Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy inaonyesha kuwa yeye hakukubaliana na hilo, na pia Ibn ‘Umar, hivyo hakuna Ijma’a katika suala hili …. (nukuu toka Kitabu cha Al-Fat-h)

 

Faida

 

Pishi moja ni sawa na vibaba vinne, na vibaba vinne ni sawa na 1/6 ya “Kaylah” (chombo cha kupimia nafaka) ya Misri ya Kale ambayo ni sawa na kilo 2.157 (kwa mizani takriban).

 

Ni wakati gani Zakaatul Fitwr hutolewa?

 

Ni lazima Zakaatul Fitwr itolewe kabla ya Swalaatul ‘Iyd. Ni haramu kuichelewesha mpaka baada ya Swalaah. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ameamuru Zakaatul Fitwr itolewe kabla hawajatoka watu kwenda katika Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (1509) na Muslim (986) na wengineo]

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefaradhisha Zakaatul Fitwr, kwa ajili ya kumtakasa mfungaji kutokana na upuuzi na “rafath” (matamanio ya jimai, mazungumzo yake, vitangulizi vyake na jimai yenyewe), na kuwalisha masikini. Na atakayeitoa kabla ya Swalaah, basi hiyo ni Zakaah yenye kukubaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalaah, basi hiyo ni swadaqah kati ya swadaqah nyinginezo)). [Takhriyj yake imetajwa nyuma kidogo]

 

Ama mwanzo wa wakati wa uwajibu kwa mujibu wa ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy, Kihanbal na Kimaalik, ni pale jua linapokuchwa siku ya mwisho ya Ramadhwaan. Ama kwa Mahanafiy na kauli ya Maalik, ni pale inapochomoza alfajiri ya siku ya ‘Iyd. [Al-Mawsuw’atu Al-Fiqhiyyah (23/340)]

 

Na faida ya makhitilafiano haya kuhusu mwanzo wa wakati wa uwajibu, inapatikana kwa mtu aliyekufa baada ya kuchwa jua siku ya mwisho ya Ramadhwaan. Kwa msingi wa kauli ya kwanza, atatolewa Zakaatul Fitwr kwa kuwa alikuwa hai wakati wa uwajibu, lakini kwa msingi wa kauli ya pili, hatotolewa.

 

Kadhalika, mtoto aliyezaliwa baada ya kuchwa jua siku ya mwisho ya Ramadhwaan. Kwa kauli ya kwanza hatotolewa Zakaah, na kwa ya pili atatolewa.

 

Je, inajuzu kutoa Zakaatul Fitwr kabla ya wakati wa Uwajibu?

 

Inajuzu kutoa Zakaatul Fitwr mapema kabla ya wakati wake kwa siku moja au siku mbili.

 

Toka kwa Naafi’u amesema: ((Ibn ‘Umar alikuwa anawapa wale wanaoikubali, na walikuwa wanaitoa kabla ya kuisha mfungo kwa siku moja au kwa siku mbili)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1511) na Muslim (986)]

 

Je, Zakaatul Fitwr husameheka kwa kutoka wakati wake?

 

‘Ulamaa wote wamekubaliana kuwa Zakaatul Fitwr haisameheki kama wakati wake utatoka, kwa kuwa ni dhima inayomganda mtu kwa watu wanaostahiki kupewa. Ni deni wanalolidai wastahiki hao, halisameheki ila kwa kuwalipa, na deni hilo ni haki ya watu. Ama Haki ya Allaah katika kuichelewesha ukatoka wakati wake, hii haiondoki isipokuwa kwa kuomba maghfirah na kujuta. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Je, inatosha kutoa pesa katika Zakaatul Fitwr badala ya chakula?

Tushazungumza nyuma kuhusu hukmu ya kutoa pesa katika Zakaah mbalimbali kiujumla. Tumesema asli, ni kuitoa kwa namna ilivyobainishwa na Hadiyth, na mtu asitoke nje ya Hadiyth akatoa pesa isipokuwa kwa dharura, au haja, au maslaha nyeti muhimu, hapo itatosheleza kutoa pesa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Wanaopewa Zakaatul Fitwr

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika kauli mbili kuhusu watu wa kupewa Zakaatul Fitwr:

 

Ya kwanza: Wanaopewa ni watu wanane (waliotajwa kwenye Aayah)

 

Ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik. [Ad-Durru Al-Mukhtaar (2/369) na Al-Majmuw’u (6/144)]

 

Ya pili: Wanapewa wahitaji (mafukara na masikini tu)

 

Ni madhehebu ya Maalik, na yamekhitariwa na Sheikh wa Uislamu. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/73)].

 

Ni kauli yenye nguvu zaidi kwa kunasibiana kwake na ufaradhisho wa Zakaatul Fitwr, kwa kuwa kwake ni (lishe kwa masikini). [Hadiyth Hasan. Takhriyj yake imeelezwa nyuma]

 

Na kwa kuwa pia Zakaatul Fitwr inafanana na kafara, hivyo haijuzu kumlisha isipokuwa yule anayestahiki kafara.

 

 

 

Share