04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Swiyaam ya Ramadhwaan Hukmu Yake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

04-Swiyaam ya Ramadhwaan Hukmu Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swiyaam ya Ramadhwaan ni waajib kwa kila Muislamu aliyebaleghe, mwenye akili timamu, mzima wa afya na mkazi. Ni nguzo kati ya nguzo za Uislamu, na uwajibu wake umedulishwa na Qur-aan, Sunnah na Ijma’a ya Ummah.

 

Kutoka Qur-aan ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ • أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ • شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))

((Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa • (Swiyaam ni) Siku za kuhesabika. Lakini atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini. Na atakayefanya kwa khiari yake jema lolote, basi hilo ni bora kwake. Na mkifunga Swiyaam ni bora kwenu mkiwa mnajua • Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru)). [Al-Baqarah (2:183-185)]

 

 

Na kutoka kwenye Sunnah:

 

1- Hadiyth ya Talha bin ‘Ubaydillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba bedui mmoja alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ilhali nywele zake zimevurugika, zimejaa vumbi (kutokana na safari) akasema: “Nieleze Aliyonifaradhia Allaah katika Swiyaam”. Akasema:

((شهر رمضان إلا أن تطوع شيئا))

((Mwezi wa Ramadhwaan isipokuwa kama utafanya kitu cha ziada [cha Sunnah])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (46) na Muslim (11)]

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((بني الإسلام على خمس: شهادة أن لا إله إلا الله وأن محمدا رسول الله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة، والحج، وصوم رمضان))

((Uislamu umejengwa juu ya (nguzo) tano: Kushahadia kuwa hapana mungu isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, Kuhiji na kufunga Ramadhwaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (8) na Muslim (16)]

 

3- Hadiyth mashuhuri ya Jibriyl isemayo: Akasema (Rasuli):

 

((الاسلام أن تعبد الله ولا تشرك به، وتقيم الصلاة، وتؤتي الزكاة المفروضة، وتصوم رمضان...)) الحديث

((Uislamu ni (wewe) umwabudu Allaah na wala usimshirikishe, usimamishe Swalaah, utoe Zakaah iliyofaradhishwa, na ufunge Ramadhwaan..)). Hadiyth [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (50) na Muslim (9)]

 

 

Waislamu wote wanakubaliana kuwa Swawm ni nguzo kati ya nguzo za Uislamu zinazojulikana kwa ulazima katika Diyn ambapo mwenye kuikanusha anakuwa kafiri, na kwamba nguzo hii haipomoki kwa mukallaf (aliyebaleghe) isipokuwa kwa udhuru kati ya nyudhuru za kisharia zinazokubalika ambazo tutakuja kuzielezea. [Al-Ifswaah cha Ibn Habiyrah (1/232), Al-Mughniy (3/285) na Al-Majmuw’u (6/252)]

 

 

 

Share