09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Sunnah Za Swawm Na Adabu Zake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

09-Sunnah Za Swawm Na Adabu Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kula daku

 

Toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((تسحروا، فإن في السحور بركة))

((Kuleni daku, kwani katika daku kuna barkah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1923) na Muslim (1095)]

 

Na toka kwa ‘Amri bin Al-‘Aaswiy amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((فصل ما بين صيامنا وصيام أهل الكتاب أكلة السحور))

((Tofauti kati ya Swiyaam yetu na Swiyaam ya Ahlul Kitaab ni mlo wa daku)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1096), Abu Daawuwd (2343), At-Tirmidhiy (709) na An-Nasaaiy (4/46)]

 

 

Daku inakidhi lengo lake hata japo kwa funda la maji. Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((تسحروا ولو بجرعة ماء))

((Kuleni daku japokuwa kwa funda la maji)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ibn Hibaan (3476). Ina Hadiyth mwenza kwa Ahmad (3/12) na Abiy Ya’alaa (3340) toka kwa Anas]

 

Na lau tende italiwa kwa daku, basi ni bora zaidi. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((نعم سحور المؤمن التمر))

((Daku bora zaidi kwa Muumini ni tende)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2345) na Ibn Hibaan (3475). Ina Hadiyth wenza]

 

2- Kuchelewesha daku

 

Ni kwa Hadiyth ya Anas toka kwa Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:

 

((Tulikula daku pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), kisha akasimama kwenda kwenye Swalaah. Nikauliza: Ni muda gani kati ya adhana na daku? Akasema: ((Kiasi cha Aayah 50)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1921), Muslim (1097) na wengineo]

 

Toka kwa Unaysah bint Habiyb amesema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) :

((إذا أذن ابن أم مكتوم، فكلوا واشربوا، وإذا أذن بلال فلا تأكلوا ولا تشربوا. فإن كانت الواحدة منا ليبقى عليها الشيء من سحورها، فنقول لبلال: أمهل حتى أفرغ من سحوري))

((Akiadhini Ibn Ummi Maktuwm, basi kuleni na kunyweni. Na akiadhini Bilaal, basi msile wala msinywe)). “Na kama mmoja wetu imebaki sehemu ya daku yake hajaimaliza, tunamwambia Bilaal: Subiri kidogo mpaka nimalize daku yangu”. [Isnaad yake ni Swahiyh. An-Nasaaiy ameikhariji kwa tamko hili (2/10), Ahmad (6/433) na Ibn Hibaan (3474)]

 

Na kama mtu atasikia adhana ya Alfajiri nailhali chakula chake au kinywaji chake kiko mkononi, basi anaweza kumalizia tonge lake na kinywaji chake. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

  ((إِذَا سَمِعَ أَحَدُكُمُ النِّدَاءَ وَالْإِنَاءُ عَلَى يَدِهِ، فَلَا يَضَعْهُ حَتَّى يَقْضِيَ حَاجَتَهُ مِنْهُ))

((Akisikia mmoja wenu adhana, na chombo kiko mkononi mwake, basi asikitue mpaka amalize haja yake toka humo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2333) na Al-Haakim (1/426). Angalia Swahiyh Al-Jaami’i(607)]

 

3- Kuwahisha kufuturu

 

Toka kwa Sahl bin Sa’ad kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((لا يزال الناس بخير، ما عجلوا الفطر))

((Watu wataendelea kuwa kwenye kheri, madhali wanaharakia kufungua)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1957) na Muslim (1098)]

 

Na toka kwa ‘Abdullaah bin Abiy Awfaa amesema: ((Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika safari –na yeye amefunga- na jua lilipokuchwa, aliwaambia baadhi ya watu: Ee fulani, simama utukorogee chakula. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ikiingia jioni. Akasema: Shuka, utukorogee chakula…(×3). Akateremka na kuwakorogea. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akanywa, kisha akasema:

((إذا رأيتم الليل قد أقبل من ها هنا فقد أفطر الصائم))

((Mkiuona usiku umeingia kutokea hapa, basi mfungaji ameshafungua)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1955) na Muslim (1101)]

 

4- Kufungulia kwa rutwab (tende laini) au tamr (tende kavu) -zikipatikana- au maji

 

Toka kwa Anas amesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akifungulia kwa rutwab kabla ya kuswali, na kama si rutwab, basi kwa tamr, na kama hakupata, hunywa mafundo ya maji)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2356) na At-Tirmidhiy (692). Angalia Al-Irwaa (822) na Asw-Swahiyha (2065)].

 

“Kwani kuupa mwili kitu tamu tumbo likiwa tupu, kunalifanya likipokee haraka zaidi na mwili unanufaika nacho vizuri zaidi na kupata nguvu. Ama maji, ini kutokana na Swawm, hupatwa na ukavu hivi, na linapopata unyevu kwa maji, basi hunufaika kikamilifu na chakula kinacholiwa halafu. Na kwa ajili hiyo, inakuwa ni vizuri zaidi kwa mwenye kiu na njaa, aanze kunywa maji kidogo kabla ya kula, kisha ale baada ya kunywa. Hii ukiongezea na faida mahususi zilizopo kwenye tamr na maji ambazo husaidia sana katika kuweka moyo wa mtu katika hali imara ya afya. Faida hizi hawazijui isipokuwa madaktari wa moyo”. [Zaadul Ma’aad (2/50 na 51]

 

5- Kuomba du’aa wakati wa kufungua kwa yafuatayo:

 

Toka kwa Ibn ‘Umar amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anapofungua husema:

((ذهب الظمأ وابتلت العروق، وثبت الأجر إن شاء الله))

((Kiu kimeondoka, mishipa ya damu imelowana, na ajri imethibiti In Shaa Allaah)). [Al-Albaaniy kasema Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2357), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (10131-3329) na Ibn As-Sunniy (472). Angalia Al-Irwaa (920)]

 

6, 7- Utoaji kwa ukwasi, kuisoma Qur-aan na kuidurusu

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa mkwasi zaidi wa watu kwa kheri. Alikuwa mwingi wa ukwasi zaidi katika Ramadhwaan wakati Jibriyl anapokutana naye. Jibriyl alikuwa anakutana naye kila usiku wa Ramadhwaan mpaka inamalizika, na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anamsomea Qur-aan. Na Jibriyl anapokutana naye, alikuwa mkwasi zaidi wa kheri kuliko upepo uvumao)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6) na Muslim (2308)]

 

8- Kujiweka mbali na yenye kubomoa thawabu za Swiyaam kati ya maaswiya ya dhahiri na yasiyo dhahiri

 

Ni lazima mfungaji auchunge ulimi wake kutokana na maneno yasiyo na faida, kubwabwaja, kuongopa, kusengenya, kufitini, maneno machafu, maneno ya karaha, mizozano na mijadala. Na avizuie viungo vyake kutokana na aina zote za matamanio na maharamisho, kwani hii ndio siri halisi ya Swawm kama Alivyosema Ta’aalaa:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))

((Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa)). [Al-Baqarah (2:183)]

 

Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ اَلزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ، فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ))

((Ambaye hatoacha kusema ya haramu na kuyatenda, basi Allaah Hana haja ya [mtu huyo] kuacha chakula chake na kinywaji chake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1903), Abu Daawuwd (2345) na At-Tirmidhiy (702)]

 

Na toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إذا كان يوم صوم أحدكم فلا يرفث ولا يصخب ولا يجهل، فإن شاتمه أحد أو قاتله قليقل: إني صائم))

((Itakapokuwa siku ya Swiyaam ya mmoja wenu, basi asitamke maneno machafu, wala asipayuke akipaza sauti, wala asifanye mambo ya ovyo. Na ikiwa mtu atatafuta sababu ya kutukanana naye au kupigana naye basi aseme: Hakika mimi nimefunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151)]

 

Tunapata funzo kutokana na Hadiyth hizi mbili kuwa ubaya wa maasia haya huzidi katika mfungo wa Ramadhwaan kuliko katika miezi mingineyo, na kuwa maasia haya hudhuru usalama wa Swiyaam, bali yanaweza kumfanya mfungaji akose kabisa thawabu.

 

9- Aseme kama atatukanwa: “Mimi nimefunga”

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia. Inakuwa ni vizuri kwa aliyetukanwa amwambie aliyemtukana wakati wa Swiyaam: “Mimi nimefunga”. Na ni vizuri aseme hivyo kwa sauti ya kusikika sawasawa kwa Swawm ya Faradhi au Swawm ya Sunnah. Katika hili kuna faida mbili:

 

Ya kwanza: Ni kumjuvya mtukanaji kuwa anayetukanwa hakuacha kukabiliana naye kwa kuwa hamwezi, bali ni kwa kuwa amefunga.

 

Ya pili: Ni kumkumbusha mtukanaji kuwa mfungaji hatukanani na yeyote, hivyo inakuwa ni kama kumkataza asiendelee kutukana.

 

 

 

Share