15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Masuala Kadhaa Kuhusiana Na Swawm Za Sunnah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

15-Masuala Kadhaa Kuhusiana Na Swawm Za Sunnah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kutia niya ya kufunga tokea usiku

 

Nyuma katika kuzungumzia masharti ya kuswihi Swiyaam, tumeona kwamba madhehebu ya Jumhuri yamejuzisha kuweka niya ya kufunga Swawm ya Sunnah wakati wa mchana kwa ambaye hakula au kunywa na akataka kufunga, na kwamba hakuna sharti ya kutia niya usiku kama ilivyo kwenye Swawm ya Faradhi. Lakini kutia niya hiyo kabla ya Alfajiri inakuwa akiba zaidi.

 

2- Mwenye kufunga Swawm ya Sunnah ni mfalme wa nafsi yake, akitaka atakamilisha Swawm, na akitaka atakula, na hatolipa.

 

Aliyeamua kufunga Swawm ya Sunnah, linalopendeza kwake ni kuikamilisha, lakini kama ataona ale, basi afanye hivyo na hatolipa. Yamesemwa haya na Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Majmuw’u (6/393) na Sharhul ‘Umdah]

 

Wametolea dalili yaliyosimuliwa toka kwa Ummu Haaniy: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliingia kwangu Siku ya ukombozi wa Makkah, akaletewa kinywaji akanywa, kisha akanipa mimi nikamwambia: Mimi nimefunga. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:

 

((إن المتطوع أمير نفسه، فإن شئت فصومي، وإن شئت فأفطري))

((Mwenye kufunga Swawm ya Sunnah ni mfalme wa nafsi yake, hivyo ukitaka funga, na ukitaka kula)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (732), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (503) na Ahmad (6/341)]

 

Ninasema: “Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, lakini maana yake inatolewa ushahidi na Hadiyth ya Abu Juhayfah aliyesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliunga udugu kati ya Salmaan na Abud Dardaa,... Salmaan akamwandalia chakula na kumkaribisha. Akasema Mimi nimefunga. Akasema: Mimi sili mpaka ule, naye akala,… Salmaan akamwambia: Hakika Mola wako Ana haki Yake toka kwako, nafsi yako ina haki yake toka kwako, mke wako ana haki yake toka kwako, basi mpe kila mwenye haki haki (yake). [Abud Dardaai] akamwendea Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwelezea hilo. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia: ((Salmaan kasema kweli)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth hii inatueleza kuwa Abud Dardaai alikula, na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakumwamuru kulipa.

 

Na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliniambia siku moja: ((Ee ‘Aaishah! Je mna chochote? Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah, hatuna kitu. Akasema: ((Basi kwa hivyo mimi nafunga)). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam akatoka, tukaletewa zawadi., au alitujia mgeni. Na wakati aliporudi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) nilimwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Tumeletewa zawadi au ametujia mgeni [na zawadi], nami nimekufichia kidogo. Akauliza: ((Ni nini hicho?)) Nikamwambia ni “hays” [Chakula cha mchanganyo wa samli na tende]. Akasema: Ilete, nikamletea, naye akaila. Kisha akasema: ((Hakika niliamka nikiwa nimefunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1154) na imetajwa nyuma]

 

Na hii ni Hadiyth inayogusia kujuzu kufungua baada ya kutia niya ya kufunga. Na hili limethibiti kwa Asaaniyd Swahiyhah toka kwa Ibn ‘Abbaas, Ibn Mas’uwd, na Jaabir.

 

Lakini Abu Haniyfah na Maalik wanasema kuwa aliyeamka na Swawm ya Sunnah kisha akala kwa kusudi, basi ni lazima alipe. Wametoa dalili kwa yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia yeye na Hafswah walipokuwa wamefunga halafu wakala:

 

((اقضيا يوما آخر مكانه))

((Lipeni siku nyingine mahala pake)), lakini ni Dhwa’iyf. [Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (735), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (3291) na Ahmad]

 

Pia wametoa hoja kwa ziada iliyokuja katika Hadiyth ya ‘Aaishah -kuhusiana na kufungua Rasuli baada ya kufunga-, na nyongeza hiyo ni:

 

((إني كنت أردت الصوم، ولكن أصوم يوما مكانه))

((Hakika mimi nilitaka kufunga, lakini nitafunga siku nyingine mahala pake)), lakini ni Shaadh. [Imekharijiwa na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (3300), ‘Abdur Razzaaq (7793), Ad-Daaraqutwniy (2/177) na Al-Bayhaqiy (4/275). An-Nasaaiy kasema: Hili ni kosa. Na Al-Bayhaqiy kasema: Kwa ‘Ulamaa ni Hadiyth isiyohifadhiwa]

 

Wametoa ulinganishi (qiyaas) wa kutimiza Swawm ya Sunnah kwa kutimiza Hajji na ‘Umrah, lakini huu ni ulinganishi wa viwili vinavyotofautiana, kwani mwenye kuiharibu Swalaah yake au Swawm yake, anakuwa ni mwenye kuasi lau atabobea kwenye uharibifu huo. Ama katika Hajji, [ikiwa ataiharibu] basi anaamuriwa aendelee kuifisidi, na haijuzu kwake kutoka kwenye ‘ibaadah hiyo mpaka aitimize ikiwa imeshafisidika, kisha atailipa. Lakini kwa Swawm na Swalaah si hivyo, hazifanyiwi ulinganishi na Hajji. Halafu ulinganishi hapa ni kwa mkabala wa Hadiyth, hivyo hauzingatiwi. [Ameinukulu katika At-Tamhiyd (12/77) toka kwa Ash-Shaafi’iy]

 

Isitoshe hapa, Qiyaas ni kwa mkabala wa Hadiyth, hivyo haizingatiwi.

 

3- Je, inajuzu kufunga Swawm ya Sunnah kabla ya kulipa Ramadhwaan?

 

Tumeshatangulia kusema kuwa madhehebu ya Jumhuri ya Salaf na Khalaf imejuzisha kuchelewesha kulipa Ramadhwaan –kwa aliyekula kutokana na udhuru- bila kushurutisha kuharakia kuilipa mara anapoweza kufanya hilo.

 

Kisha wakakhitalifiana katika kujuzu kufunga Swawm ya Sunnah kabla ya kulipa Ramadhwaan. Mahanafii na riwaya toka kwa Ahmad wakajuzisha, Wamaalik wakasema ni makruhu, Mashaafi’iy wakastahabisha kulipa kabla ya kufunga Sunnah, na Ahmad kwa riwaya nyingine akasema haijuzu. [Al-Badaai’u (2/104), Mawaahibul Jaliyl (2/417), Al-Majmuw’u (6/375) na Al-Mughniy (4/401)]

 

Ninasema: “Dalili ya kuzuia kufunga Sunnah kabla ya kulipa Ramadhwaan haiswihi bali inaonyesha kuwa inajuzu. Kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Hakuainisha mpaka ya kulipa kwa Neno Lake:  

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah (2:184)]

 

 Na Hadiyth ya ‘Aaishah inadulisha hilo vile vile aliposema: ((Ilikuwa ninakuwa nadaiwa Swawm ya Ramadhwaan, na siwezi kuilipa isipokuwa katika Sha’abaan)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1950), na Muslim (1146)]

 

Na hakuna shaka kuwa alikuwa anafunga Swawm za Sunnah katika masiku ya mwaka, na hili alilifanya na Rasuli anajua, na kujua huko ni kulikubali jambo. Kisha kulipa ni wajibu unaofungamana na wakati mkunjufu, hivyo imejuzu kufunga Sunnah katika wakati wake kabla ya kulipa. Ni kama Swalaah ya Sunnah anapoiswali mwanzoni mwa wakati wake [kisha akalipa faradhi]. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

4- Mwanamke humtaka mumewe idhni ya kufunga

 

Haijuzu kwa mwanamke kufunga Swawm ya Sunnah na mumewe yupo isipokuwa kwa idhini yake. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliyesema:

((لا تصوم المرأة وبعلها شاهد إلا بإذنه))

((Hafungi mwanamke na mumewe yupo ila kwa idhni yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5192) na Muslim (1026)]

 

Sababu ya katazo hili ni kuwa mume ana haki ya kustarehe naye nyakati zote, na haki hiyo ni lazima apatiwe haraka. Hivyo haki hiyo isimpite kwa Swawm ya Sunnah au ya Waajib ya kucheleweshwa. [Al-Badaai’u (2/107), Al-Mudawwanah (1/186) na Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/65)]

 

Mwanamke mmoja alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mume wangu Swafwaan bin Al-Mu’attwal ananipiga nikiswali, ananifunguzisha nikifunga, na haswali Alfajiri mpaka jua lichomoze. Swafwaan akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ama neno lake ananipiga nikiswali, hakika yeye anasoma Suwrah mbili na wewe umetukataza. Akasema (Rasuli): ((Lau ingelikuwa Suwrah moja, basi ingeliwatosha watu)). Ama neno lake ananifunguzisha, hakika yeye anakurupuka tu na kufunga, na mimi ni mtu kijana, siwezi kuvumilia. Siku hiyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:

((لا تصوم امرأة إلا بإذن زوجها))

((Hafungi mwanamke yeyote ila kwa ruksa ya mumewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2459), Ahmad (3/84) na Al-Bayhaqiy (4/303)]

 

Na ikiwa mumewe hayupo kabisa nyumbani, basi Swawm yake ya Sunnah inajuzu bila makhitalifiano kutokana na Hadiyth ilivyofahamika na kwa kuondoka sababu ya katazo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (6/392)]

 

 

 

 

Share