07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Kumhijia Mwingine

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

07-Kumhijia Mwingine

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kumhijia aliyeshindwa kwenda

 

 

Atakayepata uwezo wa kwenda Hijjah, kisha akashindwa kutokana na uzee au ugonjwa sugu, basi ni lazima atafute mtu wa kumhijia na amlipie gharama zote kwa fedha zake. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas toka kwa Al-Fadhwl bin ‘Abbaas: ((Kwamba mwanamke mmoja toka Khath-’am alisema: Ee Rasuli wa Allaah, Hakika baba yangu imemkuta Faradhi ya Allaah katika Hajj akiwa mzee kikongwe, hawezi kukaa sawa juu ya mnyama, basi je naweza kumhijia? Akamwambia: Na’am)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1855) na Muslim (13334)]

 

Na katika riwaayah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:

 

((أرأيت لو كان على أبيك دين، أكنت قاضيته؟)) قالت: نعم، قال: ((فدين الله أحق أن يقضى))

((Nieleze, kama baba yako alikuwa anadaiwa deni, je ungelilipa?)). Akasema: Na’am. Akasema: ((Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6699) na An-Nasaaiy (5/116)]

 

Hii ni kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik.

 

Faida

 

Akihijiwa mwenye maradhi sugu yasiyotegemewa kupona kisha Allaah Akamponya maradhi yake, basi huyo deni lake la Hajj litakuwa limeshasafika na hatotakwa ahiji mwenyewe baada ya hapo –katika moja ya kauli mbili swahiyh zaidi za ‘Ulamaa- kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ameeleza -katika Hadiyth iliyotangulia- kwamba Deni la Allaah hulipwa kwa mtu kuhijiwa na hufutika asidaiwe tena. Hivyo haijuzu faradhi hiyo imrejelee tena isipokuwa kwa dalili, na hapa dalili ya hilo hakuna. Na kama ingekuwa inamrejelea, basi Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) angelibainisha hilo na hususan ukiwepo uwezekano wa mzee kikongwe kuja kupata uwezo wa kupanda (mnyama au kipando kingine). Hivyo faradhi haijuzu kumrejelea baada ya kuhijiwa kwa usahihi unaotakikana.

 

Haya ni madhehebu ya Mahanbali, Is-Haaq na Ibn Hazm. Lakini Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ibn Al-Mundhir wanasema Hajj itamwajibikia tena, na ni lazima, kwa kuwa alipopona, imebainika kuwa ugonjwa wake haukuwa wa kukatiwa tamaa kupona, hivyo asili inamganda.

 

Rai ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Al-Mughniy (3/449) na Al-Muhallaa (62)]

 

2- Kumhijia maiti aliyewajibikiwa na Hajj kwa gharama ya mali yake aliyoacha

 

Aliyekufa naye ana uwezo wa moja ya picha tulizozielezea, atahijiwa kwa fedha za mali yake kabla ya kulipwa madeni anayodaiwa –kama hakupatikana mtu wa kumhijia kwa kujitolea- ni sawa ameusia hilo au hajausia. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

((مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ))

((baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni)). [An-Nisaa (4:11)]

 

Hapa Allaah Ameyagusa madeni yote. Na tushaeleza nyuma kidogo kuwa Deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na kundi la Masalaf. [Al-Majmuw’u (7/93) na Al-Muhallaa (62)]

 

Abu Haniyfah na Maalik wamesema hatohijiwa isipokuwa tu kama ameusia, na inakuwa ni katika theluthi ya mali aliyoacha.

 

3-  Anayemhijia mtu ajihijie mwenyewe kwanza

 

Imeshurutishwa kwa mtu anayetaka kumhijia mwingine, awe yeye ameshafanya Hajj yake ya faradhi kwanza, ili aweze kuhijia kwa niaba. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Hanbali na ‘Ulamaa wengi. Ni kauli pia ya Ibn ‘Abbaas, na hakuna Swahaba yeyote aliyejulikana kulipinga hilo. [Al-Majmuw’u (7/98), Al-Mughniy (3/245), Al-Furuw’u (3/265) na Fataawaa Ibn Taymiyah]

 

Dalili yao ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimsikia mtu akisema:

 

((لبيك عن شبرمة، قال: ((من شبرمة؟)) قال: أخ لي – أو قريب لي- قال: ((حججت عن نفسك؟)) قال: لا، قال: ((حج عن نفسك ثم حج عن شبرمة))

 “Labbayka”(Nimekuitikia) kwa niaba ya Shubrumah. Akasema (Rasuli): ((Ni nani Shubrumah?)). Akasema: Ni ndugu yangu –au jamaa yangu- Akasema: ((Ushajihijia mwenyewe?)). Akasema: Hapana. Akasema: ((Jihijie mwenyewe, kisha mhijie Shubrumah)). Imezozaniwa kuhusu Raf-‘u yake, Waqf yake na uswahiyh wake. [Imetiwa doa kwa kuelezewa kuwa ni Mawquwf na Mudhw-twarib. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1811), Ibn Maajah (2903) na wengineo]

 

Abu Haniyfah na Maalik wamesema Hajj itamtosheleza hata kama hajajihijia mwenyewe. Wametoa dalili kwa Hadiyth isiyoainisha ya mwanamke wa Khath-‘amah iliyotangulia Rasuli alipomwambia: ((Mhijie baba yako)), bila ya kumuuliza kama ameshajihijia mwenyewe au la.

 

Ninasema: “Lililo bora asimhijie mwingine ila baada ya kujihijia mwenyewe ili kutoka kwenye mvutano. Isitoshe, hiyo ni kauli ya Swahaba, nayo inazingatiwa zaidi kuliko kauli ya mwingine na hususan ikijulikana kuwa hakuna Swahaba yeyote aliyekwenda kinyume na kauli hiyo. Halafu, uangalizi (wa kihulka) unamsukuma mtu ajitangulize mwenyewe kabla ya mwingine kwa ujumuishi wa neno lake (Rasuli) kuhusu matumizi:

((ابدأ بنفسك))

((Jianze mwenyewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (997) toka kwa Jaabir]

 

Na kwa haya, inachukulika kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakumuuliza mwanamke huyo wa Khath-‘amah kwa kuwa alishajua kuwa ameshajihijia mwenyewe kwa kutumia vielelezo kama alivyosema Ibn Al-Hammaam. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

 

4- Kumhijia mtu Hajj ya Sunnah

 

Inaruhusika kumhijia mtu Hajj ya Sunnah kwa hali yoyote –hata kama anaweza- kwa kuwa ni Hajj ambayo haimlazimu mwenye uwezo kuifanya mwenyewe. Hivyo inajuzu kumwakilisha mtu mfano wa mwenye ugonjwa sugu. Na kwa vile pia, katika Sunnah anajiachilia asivyoweza kujiachilia katika faradhi. Na kama katika faradhi inajuzu kumwakilisha mtu, basi katika Sunnah inajuzu zaidi. Haya ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa ya Abu Haniyfah na Hanbali, pia Maalik pamoja na ukaraha.

 

 5- Mwanamke kumhijia mwanamke mwenzake  

 

(a) Inajuzu mwanamke kumhijia mwanamke mwingine kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote, ni sawa akiwa binti yake au mwanamke mwingine. [Majmuw’u Fataawaa Ibn Taymiyah (26/13)]

 

Toka kwa Muwsaa bin Salamah kuwa mwanamke mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuwa mama yake amekufa na hakuwahi kuhiji, je itamtosheleza yeye kumhijia mama yake?Akasema:

 

((نعم، لو كان على أمها دين فقضته عنها ألم يكن يجزئ عنها؟ فلتحج عن أمها))

((Na’am, lau angelikuwa mama yake ana deni akamlipia, je isingekuwa inamtosheleza? Basi amhijie mama yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (5/116) na Ahmad (1/279) kwa Sanad Swahiyh. Na mfano wake kwa Muslim (1149) na At-Tirmidhiy (667) toka kwa Buraydah]

 

(b) Inajuzu pia kwa mwanamke kumhijia mwanaume kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo. Ni kwa Hadiyth ya mwanamke wa Khath-‘amah tuliyoitaja mara kadhaa.

 

6- Kuhiji kwa mali haramu

 

[Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (7/51)]

 

‘Ulamaa wengi wanasema kwamba mtu akihiji kwa mali haramu, au akapanda mnyama wa kupora, basi atapata madhambi lakini Hajj yake ni sahihi na itamtosheleza. Wamesema, kwa kuwa, vitendo vya Hajj ni vitendo maalum, na uharamisho ni wa maana iliyo nje ya vitendo hivyo.

Lakini Imaam Ahmad amekhalifiana nao kwa kusema kuwa haimtoshelezi akitoa dalili kwa Hadiyth isemayo:

((إن الله طيب لا يقبل الا طيبا))

((Hakika Allaah ni Mtakasifu, Hakubali isipokuwa kitakasifu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1015), At-Tirmidhiy (2986) na wengineo]

 

Na kwa Hadiyth Marfuw’u isemayo:

 

((Anapotoka mwenye kukusudia Hajj kwa kuhiji kwa fedha halali, akiweka mguu wake juu ya kipandio akanadi: Labbayka Al-Laahumma Labbayka, basi mwenye kunadi humwita toka mbinguni: Labbayka wa sa’addayka [Umeitikiwa na umefurahikiwa], masurufu yako ni ya halali, kipando chako ni cha halali, na Hajj yako ni salama iliyotakasika isiyo na madhambi. Na anapotoka na fedha chafu akaweka mguu wake juu ya kipandio akanadi: Labbayka, mwenye kunadi humwita toka mbinguni: Laa Labbayka, walaa sa’addayka [Huitikiwi wala hufurahiwi]. Masurufu yako ni ya haramu, fedha zako ni za haramu, na Hajj yako ni ya madhambi isiyo salama)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Twabaraaniy katika Al-Awsatw (5228) na Abu Nu’aym katika Al-Hilyah. Angalia Al-‘Ilal Al-Mutanaahiyah]

 

Ninasema: “Yenye nguvu ni kauli ya Jumhuri kwa yaliyotangulia. Ama Hadiyth ya ((إن الله طيب..)) hakuna ndani yake hujjah. Na Hadiyth ya ((وحجك مأزور غير مأجور)) ni Dhwa’iyf, haifai”.

 

 

 

Share