32-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Ziara Ya Madiynah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

32-Ziara Madiynah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

Utukufu wa Madiynah

 

Toka kwa Jaabir bin Samurah amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema:

((إن الله تعالى سمى المدينة طابة))

((Hakika Allaah Ta’aalaa Ameiita Al-Madiynah Twaabah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1385)]

 

 

Na toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

 ((إِنَّ الْمَدِينَةَ كَالْكِيرِ تُخْرِجُ الْخَبِيثَ ‏.‏ لاَ تَقُومُ السَّاعَةُ حَتَّى تَنْفِيَ الْمَدِينَةُ شِرَارَهَا كَمَا يَنْفِي الْكِيرُ خَبَثَ الْحَدِيدِ))

((Hakika Madiynah ni kama mvukuto [wa mhunzi] ambao utamtoa mwovu toka humo. Haisimami Saa (Qiyaamah) mpaka Madiynah iwatoe wabaya wake kama mvukuto unavyotoa uchafu wa chuma)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1381)]

 

 

Ubora wa Msikiti wake na fadhla za kuswali ndani yake

 

Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((لا تشد الرحال إلا إلى ثلاثة مساجد، مسجدي هذا، ومسجد الحرام، ومسجد الأقصى))

((Safari hazifungwi isipokuwa kwa Misikiti Mitatu; Msikiti wangu huu, Masjidil Haraam na Masjidil Aqswaa)). [Muttafaqun ‘Alayhi. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1189) na Muslim (1397)]

 

Na kasema tena Abu Hurayrah: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((صلاة في مسجدي هذا خير من ألف صلاة في غيره من المساجد، إلا المسجد الحرام))

((Swalaah moja katika Msikiti wangu huu ni bora kuliko Swalaah elfu moja kwenye Misikiti mingine isipokuwa Al-Masjidil Haraam)). [Muttafaqun ‘Alayhi. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1190) na Muslim (1394)]

 

Na toka kwa ‘Abdullaah bin Zayd kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam amesema:

((ما بين بيتي ومنبري روضة من رياض الجنة))

((Sehemu iliyo baina ya nyumba yangu na mimbari yangu ni kiwanja kati ya viwanja vya Jannah)). [Muttafaqun ‘Alayhi. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1195) na Muslim (1390)]

 

 

Adabu za kuzuru Msikiti wa Rasuli na Kaburi lake tukufu

 

Ubora uliohusishiwa Msikiti Mtukufu wa Rasuli, Al-Masjidul Haraam na Al-Masjidul Aqswaa, na Swalaah ndani yake kuwa na thawabu zaidi kuliko kwenye Misikiti Mingineyo, bila shaka hiyo ni takrima toka kwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa. Mwenye kuiendea, bila shaka anafanya hivyo kwa utashi wa kupata thawabu na kuitikia wito wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipohimizia watu wafunge safari kuiendea na kuizuru.

 

Misikiti hii Mitatu haina adabu maalum kulinganisha na Misikiti Mingine. Lakini baadhi ya watu hukanganyikiwa na kuufanyia Msikiti wa Rasuli adabu mahsusi kutokana na kuwepo kaburi lake ndani ya Msikiti.

 

Na ili Muislamu awe analijua jambo vizuri akija Madiynah na akataka kuuzuru Msikiti wa Rasuli, hapa sisi tunamhabarisha adabu hizo za ziyara.

 

1- Anapoingia aingie kwa mguu wake wa kulia, kisha aseme:

 

((اللهم صل على محمد وسلم، اللهم افتح لي أبواب رحمتك))

((Ee Allaah! Mswalie Muhammad na Mpe salaam. Ee Allaah! Nifungulie milango ya Rahmah Zako)).

 

Au:

((أعوذ بالله العظيم، وبوجهه الكريم، وسلطانه القديم، من الشيطان الرجيم))

((Najilinda kwa Allaah Al-‘Adhwiym, na kwa Uso Wake Al-Kariym, na kwa Uqahari Wake wa Azali, kutokana na Shaytwaan aliyewekwa mbali na rahmah)).

 

2- Kisha ataswali rakaa mbili za Maamkuzi ya Msikiti (Tahiyyatul Masjid) kabla hajakaa.

 

3- Atahadhari asiswali kwa kulielekea Kaburi Tukufu, au kulielekea wakati anapoomba du’aa.

 

4- Halafu atakwenda kwenye Kaburi Tukufu ili amtolee salaam Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), na atahadhari asiweke mikono yake kifuani, au kuinamisha kichwa, au kujinyenyekeza –ambako hakutakikani kwa yeyote isipokuwa kwa Allaah Pekee-, au kumlilia shida Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Amtolee salaam Rasuli kwa matamshi na maneno ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiwasalimia kwayo Ahlul Baqiy’i. Kuna matamshi kadhaa swahiyh yaliyopokelewa toka kwake ambayo kati yake ni:

 

((السلام علي أهل الديار من المؤمنين والمسلمين ويرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين، وإنا إن شاء الله بكم للاحقون))

((Amani iwe juu ya watu wa makazi haya kati ya Waumini na Waislamu, na Allaah Awarehemu waliotangulia kati yetu na wanaofuatia nyuma. Na sisi bila shaka Akipenda Allaah tutaungana nanyi)).

 

Kisha atawatolea salaam Maswahibu wake wawili Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa)) kwa salaam hiyo hiyo.

 

5- Asinyanyue sauti ndani ya Msikiti au mbele ya Kaburi Tukufu, sauti yake iwe ya chini. Kwa kuwa kumfanyia hishma Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa maiti ni kama kumfanyia akiwa hai.

 

6- Afanye pupa kuswali Jamaa katika safu za mwanzo mwanzo kutokana na fadhla kubwa na thawabu nyingi zinazopatikana katika safu hizo.

 

7- Pupa ya kuswalia kwenye Rawdhwah isimfanye achelewe kuwahi safu za mwanzo, kwani kuswalia kwenye Rawdhwah hakuna tofauti na kuswalia sehemu nyingine yoyote ya Msikiti.

 

8- Si katika Sunnah mtu kupapia kuswali kwenye Msikiti Swalaah arobaini mfululizo kwa kutegemea Hadiyth Dhwa’iyf iliyotangaa kwa watu wengi isemayo:

 

((من صلى في مسجدي أربعين صلاة لا يفوته صلاة؛ كُتبت له براءة من النار، ونجاة من العذاب، وبرئ من النفاق))

((Mwenye kuswali kwenye Msikiti wangu Swalaah arubaini isimpite Swalaah yoyote, ataandikiwa kutoguswa na moto, kuokoka na adhabu, na atatakasika na unafiki)). [Hadiyth Dhwa’iyf, haifai. Angalia Adh-Dhwa’iyfah (364)]

 

9- Si katika sharia mtu kupita mara kwa mara kwenye Kaburi Tukufu ili kumtolea salaam Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), kwani salaam humfikia toka sehemu yoyote hata ikitolewa toka mwisho wa dunia. Anayetoa salaam akiwa mbele ya Kaburi la Rasuli na aliyeko mwisho wa ncha ya ardhi, wote wanapata thawabu sawa za kumswalia Rasuli na kumtolea salaam.

 

10- Anapotoka Msikitini asitembee kinyume nyume, bali atoke kwa mguu wake wa kushoto akisema:

((اللهم صل على محمد، اللهم إني أسألك من فضلك))

((Ee Allaah! Mswalie Muhammad. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Fadhla Zako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1193) na Muslim (1399)]

 

Masjid Qubaa

 

Imesuniwa kwa aliyekwenda Madiynah aukusudie na auendee Masjid Qubaa na aswali humo kufuata kitendo cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Rasuli alikuwa ameuwekea ahadi ya kuuzuru, na anauendea kila siku ya Jumamosi na kuswali ndani yake rakaa mbili. Alikuwa anakwenda kwa miguu au kwa kupanda mnyama. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1193) na Muslim (1399)]

 

Na alikuwa anasema:

 

((من تطَهَّرَ في بيتِهِ، ثمَّ أتى مسجدَ قباءٍ، فصلَّى فيهِ صلاةً، كانَ لَهُ كأجرِ عمرة))

((Mwenye kutawadha nyumbani kwake, kisha akauendea Masjid Qubaa, akaswali ndani yake Swalaah moja, basi anapata thawabu za mfano wa ‘Umrah)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Maajah (1412)]

 

 

Al-Baqiy’u na Uhud

 

Al-Baqiy’u ni eneo la makaburi ya Waislamu huko Madiynah. Hapo wamezikwa Swahaba wengi, na bado Waislamu wanaendelea kuzikwa hapo hadi hivi leo. Wengi wanaozikwa hivi leo ni wale wanaokwenda Madiynah kwa utashi wa kufia huko ili wazikwe Al-Baqiy’u.

 

Na Uhud kama anavyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((وأحد جبل يحبنا ونحبه))

((Na Uhud ni Mlima, unatupenda na sisi tunaupenda)). [Muttafaqun ‘Alayhi. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4083) na Muslim (1393)]

 

Katika uwanda wake walizikwa Shuhadaa sabini na kitu hivi waliouawa katika vita vilivyotokea hapo. Vita hivyo vimenasibishiwa Mlima huu na kujulikana kama Vita vya Uhud.   Na yeyote aliyekwenda Madiynah na akataka kuzuru Al-Baqiy’u, au kuwazuru Shuhadaa hao, basi hakuna ubaya. Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa amekataza kuyazuru makaburi kisha akaja kuruhusu ili yawakumbushe watu Aakhirah na wawaidhike na hatima ya waliomo ndani yake. Lakini ni lazima mtu atahadhari kutabaruku na makaburi, au kuwalilia shida maiti, au kuwaomba wamsaidie kutatua matatizo yake kwa walio hai, au kutawassal kwao kama njia ya kumfikia Mola wa waja.

 

Na hakuna usharia kwa anayekwenda Uhud akusudie kisemwacho kama "مصلى النبي"  chini ya Mlima ili aswali hapo, au kupanda Mlima wa Uhud kupata barkah, au kupanda Mlima wa walenga mishale ili kufuatishia athari ya mabaki ya ukumbusho wa  Swahaba hao.  Hayo yote na mengineyo hayafai, ni mambo ya uzushi yaliyokatazwa. La muhimu hapo ni kuwatolea salaam na kuwaombea du’aa Shuhadaa hao. Na kuhusu hilo, Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) anasema:

((إنما هلك من كان قبلكم بتتبعهم آثار أنبيائهم))

((Hakika waliangamia waliopita kabla yenu kwa sababu ya kufuatilia kwao athari za mabaki ya kumbukumbu za Manabii wao)).

 

Basi tuyazingatie vyema maneno haya ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa)) na tuyatekeleze.

 

Mazaaraat

 

Kuna maeneo mengineyo Madiynah yajulikanayo kama Mazaaraat. Ni kama Al-Masaajidu As-Sab-‘at (Misikiti Saba) iliyo karibu na eneo la Vita vya Khandaq, Masjid Al-Qiblatayn, baadhi ya visima, Masjid Al-Ghamaamah, na Misikiti inayonasibishwa kwa Abu Bakr, ‘Umar na ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhum). Maeneo haya yote, hayana lolote la kisharia linaloyahusisha kwa ziara, na mwenye kuyazuru asidhanie kabisa kuwa atapata thawabu za ziada kwa kuyatembelea. Kufuatisha athari ya mabaki ya kumbukumbu za Manabii na watu wema ilikuwa ndio sababu ya kuangamia umma zilizopita kabla yetu, na haiwi ni jambo zuri kwa Waislamu kukhalifu hadyi ya Nabii wao Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na hadyi ya Swahaba wake (Ridhwaanul Laah ‘alayhim). Kheri yote iko katika hadyi yake na hadyi yao, na shari yote iko katika kukhalifu hadyi yake na hadyi yao.

 

Maangalizi mawili muhimu sana

 

La kwanza: Mahujaji wengi hupupia kukaa Madiynah siku nyingi zaidi kuliko siku wanazokaa Makkah pamoja na kwamba Swalaah moja kwenye Al-Masjid Al-Haraam (Makkah) ni sawa na Swalaah laki moja kwenye Misikiti mingine. Ama Swalaah moja kwenye Al-Masjid An-Nabawiy (Madiynah) ni sawa na Swalaah elfu moja katika Misikiti mingine.

 

Tofauti hii kubwa ya malipo kati ya Swalaah kwenye Al-Masjid Al-Haraam na Al-Masjid An-Nabawiy ingebidi iwe chachu kwa Mahujaji hao ya kukaa zaidi Makkah kuliko Madiynah.

 

La pili: Mahujaji wengi wanadhani kuwa kuuzuru Msikiti wa Nabiy (Al-Masjid An Nabawiy) ni sehemu ya Manaasik za Hajj. Hivyo wanapapia hilo kama wanavyopapia Manaasik za Hajj kufikia hali ya kuona kwamba Hajj haikukamilika kwa ambaye hakwenda Madiynah.

 

Wanasimulia kuhusu hili Hadiyth kadhaa za kutungwa kama:

 " من حج فلم يزرني  فقد جفاني" 

((Aliyehiji na hakunizuru, basi kanitupa mkono)).

 

Hivi wanavyodhani hawa ni kinyume kabisa. Kuuzuru Al-Masjid An-Nabawiy ni Sunnah aliyoiweka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam kwa ajili ya kuswali ndani ya Msikiti, na hakuna mahusiano kati ya ziara hiyo na Hajj, na kuswihi Hajj hakuhusiani na ziara, bali ziara ni ‘ibaadah kando.

 

Yaliyo Marufuku Kwenye Haram Mbili (Makkah na Madiynah)

 

[Imenukuliwa toka Irshaadus Saariy cha Fadhwiylat baba Sheikh Muhammad Ibraahiym Shaqrah (uk. 260-261)]

 

Imekuja katika Swahiyh Mbili na kwengineko Hadiyth ya ‘Ibaad bin Tamiym toka kwa ami yake kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((إنَّ إبراهيمَ حرَّم مكةَ، و دعا لها، و إنِّي حرَّمتُ المدينةَ ، كما حرَّم إبراهيمُ مكةَ))

((Hakika Ibraahiym aliiharamisha Makkah na akaiombea, na hakika mimi nimeiharamisha Madiynah kama Ibraahiym alivyoiharamisha Makkah)).

 

Uharamishaji huo bila shaka ni kwa Wahyi toka kwa Allaah Subhaanah kwa Manabii Wake na Mitume Wake hawa wawili Watukufu (Swalawaatul Laahi wa Salaamuhuu ‘alayhimaa). Tunaposema Al-Haramayn, basi tunakusudia Makkah na Madiynah, na haijuzu kisharia kuitwa kwa jina hilo isipokuwa Miji hii miwili tu. Hata Al-Masjid Al-Aqswaa, haufai kisharia kuitwa Al-Haram, wala kwa Msikiti wa Ibraahiym Al-Khaliyl, kwa kuwa Wahyi haukushuka na jina Haram isipokuwa kwa Makkah na Madiynah tu. Na hiyo ni sharia, akili ya binadamu hapo si uwanja wake.

 

Kuna mambo yaliyopigwa marufuku kuyafanya katika ardhi za Makkah na Madiynah kwa mkazi asili au kwa wenye kuitembelea kwa Hajj au ‘Umrah au kwa mengineyo. Mambo hayo ni:

 

1- Kuwinda wanyama au ndege, kuwatimua au kusaidia katika kuwadhuru.

 

2- Kukata mimea na miba isipokuwa kwa haja au dharura.

 

3- Kubeba silaha.

 

4- Kuokota alichoangusha au alichopoteza mtu katika Haram ya Makkah kwa Hujaji. Ama kwa mkazi wa Makkah, huyu anaruhusiwa kukiokota ili akitangazie. Na tofauti kati ya Hujaji na mkazi i wazi katika hilo.

 

Ninasema: “Dalili ya marufuku hizi ni neno lake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) Siku ya Ukombozi wa Makkah:

 

((إنَّ هَذَا الْبَلَدَ حَرَّمَهُ اللَّهُ يَوْمَ خَلَقَ اللَّهُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضَ، فَهُوَ حَرَامٌ بِحُرْمَةِ اللَّهِ إلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ، وَإِنَّهُ لَمْ يَحِلَّ الْقِتَالُ فِيهِ لأَحَدٍ قَبْلِي، وَلَمْ يَحِلَّ لِي إلاَّ سَاعَةً مِنْ نَهَارٍ؛ فَهُوَ حَرَامٌ بِحُرْمَةِ اللَّهِ إلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ. لا يُعْضَدُ شَوْكُهُ، وَلا يُنَفَّرُ صَيْدُهُ، وَلا يَلْتَقِطُ لُقْطَتَهُ إلاَّ مَنْ عَرَّفَهَا، وَلا يُخْتَلَى خَلاهُ))، فَقَالَ الْعَبَّاسُ : يَا رَسُولَ اللَّهِ , إلاَّ الإِذْخِرَ ، فَإِنَّهُ لِقَيْنِهِمْ وَبُيُوتِهِمْ . فَقَالَ: إلاَّ الإِذْخِرَ .

 ((Hakika Allaah Ameuharamisha Mji huu Siku Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Basi Mji huu ni hifadhi isiyoguswa kwa Haramisho la Allaah hadi Siku ya Qiyaamah, na hakuruhusiwa yeyote kabla yangu kupigana ndani yake, na haikuruhusiwa kwangu isipokuwa saa moja ya mchana. Basi ni hifadhi isiyoguswa kwa Haramisho la Allaah mpaka Siku ya Qiyaamah. Mwiba wake haukatwi, wala wanyama wake wa kuwindwa hawatimuliwi, wala  haokoti chenye kupotezwa humo isipokuwa mwenye kukitangazia, na wala manyasi yake hayakatwi)). Ibn ‘Abbaas akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Isipokuwa “idh-khir” (aina ya mmea wenye harufu nzuri), kwani huo ni kwa mhunzi [kuwashia moto] na kwa [kuezekea paa za] nyumba zao. Akasema: ((Isipokuwa idh-khir)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1834) na Muslim (1353)]

 

Toka kwa Jaabir amesema: Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema:

((لا يحل لأحدكم أن يحمل بمكة السلاح))

((Ni marufuku kwa mmoja wenu kubeba silaha Makkah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1356)]

 

Na toka kwa ‘Aliyy toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema [yaani kuhusu Madiynah]:

 

((لَا يُخْتَلَى خَلَاهَا، وَلَا يُنَفَّرُ صَيْدُهَا، وَلَا تُلْتَقَطُ لُقَطَتُهَا إلَّا لِمَنْ أَشَادَ بِهَا، وَلَا يَصْلُحُ لِرَجُلٍ أَنْ يَحْمِلَ فِيهَا السِّلَاحَ لِقِتَالٍ وَلَا يَصْلُحُ أَنْ يقْطَعَ فِيهَا شَجَرَةٌ إلَّا أَنْ يَعْلِفَ رَجُلٌ بَعِيرَهُ))

((Manyasi yake hayakatwi, wala wanyama wake wa kuwindwa hawatimuliwi, wala hakiokotwi kiokotwa chake ila kwa atakayekitangazia, na wala haifai kwa mwanaume kubeba silaha kwa ajili ya mapigano, na wala haifai kukatwa humo mti isipokuwa mtu amkatie ngamia wake majani ya malisho)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2018)]

 

Sheikh Shaqrah amesema: “Mwenye kufanya marufuku hizi basi atapata madhambi, na ni lazima atubie na kuomba maghfirah isipokuwa kwa mnyama. Ikiwa aliyehirimia atamwinda, basi ni lazima achinje mnyama wa malipo mbali na kutubia na kuomba maghfirah”.

 

Share