029-Asbaabun-Nuzuwl: Al-‘Ankabuwt Aayah 08: وَوَصَّيْنَا الإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا‏

 أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

029-Asbaabun-Nuzuwl: Al-‘Ankabuwt Aayah 8

 

 

 

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۚ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾

Na Tumemuusia insani kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Lakini wakikushikilia kuwa unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii; Kwangu ni marejeo yenu, Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Al-‘Ankabuwt (29:8)]

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

حَدَّثَنَا أَبُو بَكْرِ بْنُ أَبِي شَيْبَةَ، وَزُهَيْرُ بْنُ حَرْبٍ، قَالاَ حَدَّثَنَا الْحَسَنُ بْنُ مُوسَى، حَدَّثَنَا زُهَيْرٌ، حَدَّثَنَا سِمَاكُ بْنُ حَرْبٍ، حَدَّثَنِي مُصْعَبُ بْنُ سَعْدٍ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّهُ نَزَلَتْ فِيهِ آيَاتٌ مِنَ الْقُرْآنِ - قَالَ - حَلَفَتْ أُمُّ سَعْدٍ أَنْ لاَ تُكَلِّمَهُ أَبَدًا حَتَّى يَكْفُرَ بِدِينِهِ وَلاَ تَأْكُلَ وَلاَ تَشْرَبَ ‏.‏ قَالَتْ زَعَمْتَ أَنَّ اللَّهَ وَصَّاكَ بِوَالِدَيْكَ وَأَنَا أُمُّكَ وَأَنَا آمُرُكَ بِهَذَا ‏.‏ قَالَ مَكَثَتْ ثَلاَثًا حَتَّى غُشِيَ عَلَيْهَا مِنَ الْجَهْدِ فَقَامَ ابْنٌ لَهَا يُقَالُ لَهُ عُمَارَةُ فَسَقَاهَا فَجَعَلَتْ تَدْعُو عَلَى سَعْدٍ فَأَنْزَلَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ فِي الْقُرْآنِ هَذِهِ الآيَةَ: ((وَوَصَّيْنَا الإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا‏...)) ((وَإِنْ جَاهَدَاكَ عَلَى أَنْ تُشْرِكَ بِي‏)) ‏ وَفِيهَا: ((وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا‏))‏ قَالَ وَأَصَابَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم غَنِيمَةً عَظِيمَةً فَإِذَا فِيهَا سَيْفٌ فَأَخَذْتُهُ فَأَتَيْتُ بِهِ الرَّسُولَ صلى الله عليه وسلم فَقُلْتُ نَفِّلْنِي هَذَا السَّيْفَ فَأَنَا مَنْ قَدْ عَلِمْتَ حَالَهُ ‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ رُدُّهُ مِنْ حَيْثُ أَخَذْتَهُ ‏"‏ ‏.‏ فَانْطَلَقْتُ حَتَّى إِذَا أَرَدْتُ أَنْ أُلْقِيَهُ فِي الْقَبَضِ لاَمَتْنِي نَفْسِي إِلَيْهِ فَفَرَجَعْتُ قُلْتُ أَعْطِنِيهِ ‏.‏ قَالَ فَشَدَّ لِي صَوْتَهُ ‏"‏ رُدُّهُ مِنْ حَيْثُ أَخَذْتَهُ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ فَأَنْزَلَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ: ((يَسْأَلُونَكَ عَنِ الأَنْفَالِ‏))‏ قَالَ وَمَرِضْتُ فَأَرْسَلْتُ إِلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَأَتَانِي فَقُلْتُ دَعْنِي أَقْسِمْ مَالِي حَيْثُ شِئْتُ ‏.‏ قَالَ فَأَبَى ‏.‏ قُلْتُ فَالنِّصْفَ ‏.‏ قَالَ فَأَبَى ‏.‏ قُلْتُ فَالثُّلُثَ ‏.‏ قَالَ فَسَكَتَ فَكَانَ بَعْدُ الثُّلُثُ جَائِزًا ‏.‏ قَالَ وَأَتَيْتُ عَلَى نَفَرٍ مِنَ الأَنْصَارِ وَالْمُهَاجِرِينَ فَقَالُوا تَعَالَ نُطْعِمْكَ وَنَسْقِيكَ خَمْرًا ‏.‏ وَذَلِكَ قَبْلَ أَنْ تُحَرَّمَ الْخَمْرُ - قَالَ - فَأَتَيْتُهُمْ فِي حَشٍّ - وَالْحَشُّ الْبُسْتَانُ - فَإِذَا رَأْسُ جَزُورٍ مَشْوِيٌّ عِنْدَهُمْ وَزِقٌّ مِنْ خَمْرٍ - قَالَ - فَأَكَلْتُ وَشَرِبْتُ مَعَهُمْ - قَالَ - فَذُكِرَتِ الأَنْصَارُ وَالْمُهَاجِرُونَ عِنْدَهُمْ فَقُلْتُ الْمُهَاجِرُونَ خَيْرٌ مِنَ الأَنْصَارِ - قَالَ - فَأَخَذَ رَجُلٌ أَحَدَ لَحْيَىِ الرَّأْسِ فَضَرَبَنِي بِهِ فَجَرَحَ بِأَنْفِي فَأَتَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَأَخْبَرْتُهُ فَأَنْزَلَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ فِيَّ - يَعْنِي نَفْسَهُ - شَأْنَ الْخَمْرِ: ((‏إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنْصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ‏))

 

Ametuhadithia Abu Bakr bin Abiy Shaybah na Zuhayr bin Harb wamesema: Ametuhadithia Al-Hasan bin Muwsaa, ametuhadithia Zuhayr, ametuhadithia Simaak bin Harb, amenihadithia Musw’ab bin Sa’ad toka kwa baba yake kuwa Aayaat kadhaa za Qur-aan ziliteremka kwa sababu yake. Amesema: Ummu Sa’ad aliapa kuwa hatozungumza naye milele mpaka aikufuru na aikane Dini yake (ya Uislamu), na hatokula wala kunywa. Na akamwambia (huyu mwanaye Sa‘ad): Wewe unadai kuwa Allaah Amekuusia kuwatendea wema wazazi wako wawili, na mimi ni mama yako, na mimi ninakuamuru hili. Akakaa siku tatu (bila kula wala kunywa wala kulala) mpaka akazimia kutokana na njaa na kuishiwa kabisa nguvu.  Mwanaye mwingine aitwaye ‘Umaarah akamnywesha (maji, uji, n.k akapata nguvu) na akaanza kumlaani Sa‘ad. Na hapo Allaah (عز وجل)    Akateremsha katika Qur-aan Aayah hii:

 

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي

Na Tumemuusia insani kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Lakini wakikushikilia kuwa unishirikishe…[Al-‘Ankabuwt (29:8)

 

na katika hilo hilo:

وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا

Na suhubiana nao kwa wema duniani.

 

(Hilo ni tukio la kwanza la mnasaba wa kuteremka Aayah hizi. Ama la pili,) Amesema: Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  walipata ngawira kubwa. Nikaona ndani ya ngawira hizo upanga nikauchukua. Nikaenda nao kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  nikamwambia: Niachie mimi upanga huu (uwe fungu la mgawo wangu wa ngawira), wewe ndiye ujuaye zaidi hali yangu (ya kupenda sana kumiliki silaha). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  akaniambia: “Urejeshe pale ulikouchukua.” Nikatoka haraka kuurejesha, na nilipotaka kuutupa kwenye ghala (la ghanima), roho yangu ilinishinikiza (kwamba nirudi nao kujaribu kumsihi tena), nikarejea kwake na kumwambia: Nipe upanga huu. Akaniambia kwa sauti kali: “Urejeshe pale ulikoutoa.” Na hapo Allaah (عز وجل)    Akateremsha:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ 

Wanakuuliza (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu ngawira. [Al-Anfaal (8:1)]

 

(Ama tukio la tatu), anaendelea kusema: Niliugua, nikamtuma mtu kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aniitie, naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  akaja kunijulia hali. Nikamwambia: Nakuomba uniruhusu niigawe mali yangu kwa kiasi ninachokiona mimi mwenyewe. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  akakataa. Nikamwambia: Basi nusu yake. Akakataa. Nikamwambia: Basi theluthi. Akanyamaza, na ikawa baada ya hapo theluthi inaruhusiwa. (Na tukio la nne) amesema: Nililipitia kundi la Answaar na Muhaajiriyna, wakanikaribisha chakula na pombe, na hiyo ilikuwa kabla pombe haijaharamishwa. Nikajiunga nao katika bustani (ambayo walikuwa wameketi wakila na kunywa), nikakuta kichwa cha ngamia kilichobanikwa na mtungi wa pombe. Nikala na kunywa pamoja nao, na mazungumzo yakajilemeza kati ya Answaar (kama kundi) na Muhaajiriyna (kama kundi). Mimi nikasema: Muhaajiriyna ni wabora zaidi kuliko Answaar. Mtu mmoja akachukua fupa la kichwa cha ngamia, akanipiga nalo puani, akaniumiza. Nikaenda kumweleza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).  Na hapo Allaah (عز وجل)  Akateremsha kwa sababu yangu Aayah kuhusu pombe na ulevi:

إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ

Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan. [Al-Maaidah (5:90)]

 

 

[Muslim katika Mujallad wa Kumi na Tano ukurasa wa 185]

 

At-Tirmidhiy amekhariji toka katika Hadiyth hii kishada cha kwanza, na akaashiria kilichobakia, na akasema kuwa Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh. Na Ahmad ameikhariji yote kamili katika mahala pawili katika Mujallad wa Kwanza kurasa za 181 na 186. Katika mahala pa kwanza, ameitaja Aayah ya Suwrah Luqmaan, na At-Twayaalsiy katika Mujallad wa Pili ukurasa wa 18, Al-Bukhaariy katika Al-Adab Al-Mufrad ukurasa wa 23, na At-Twabariy katika Mujallad wa Ishirini na moja ukurasa wa 70 ambapo ameitaja Aayah ya Suwrah Luqmaan. Basi ima ziwe Aayah mbili zimeshuka kwa pamoja, au awe Simaak bin Harb amekoroga (kwa kueleza Hadiyth moja kwa riwaya mbili tofauti), kwani yeye (Rahimahu Allaah) anakoroga katika Hadiyth nyingi, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

 

Share