Masharti Ya لآ اِلَهَ اِلّا اللّهُ مُحَمَّدٌ رَسُوُل اللّهِ

 

Masharti Ya لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ مُحَمد رَسُول الله

(Hapana Mwabudiwa Wa Haki Isipokuwa Allaah, Muhammad Ni Rasulu Wa Allaah)

 

Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (حفظه الله)     

Kutoka Kitaab ‘Aqiydah At-Tawhiyd

 

Alhidaaya.com

 

 

Hakika Himdi Anastahiki Allaah, Tunamshukuru na kumuomba msaada, na tunamtaka maghfirah, na tunajilinda kwake kutokana na shari za nafsi zetu, na makossa ya ‘amali zetu, atakaemuongoza Allaah hakuna wa kumpoteza, na atakaempoteza hakuna wa kumuongoza, na ninashuhudilia ya kwamba hakuna apasae kuabudiwa kwa haki ispokuwa Allaah Peke Yake Hana mshirika, na ninashuhudilia yakuwa Muhammad ni mja wake na ni Rasuli wake  (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

Ammaa baad. Hii ni sherehe kwa muhtasari ya Masharti ya

 

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ   

Laa Ilaaha Illa Allaah (hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah), yaliyoandikwa na Shaykh: Swaalih Fawzaan(حفظه الله)   kwenye kitabu chake cha: ‘Aqiydah At-Tawhiyd. Tunamuomba Allaah (عز وجل) Anufaishe kwa kitabu hicho.

 

 

Masharti Ya لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ   

 

 

Ni lazima katika Shahaadah ya لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ  yapatikane masharti saba, na hatoweza kunufaika mtamkaji wa shahada hiyo mpaka zikusanyike kwake sharti zote.

 

Hizo sharti kwa ujumla ni:

 

 

Sharti Ya Kwanza:  'Ilmu (Elimu, Maarifa, Ujuzi, Utambuzi), inayo ondosha ujinga.

 

 

Sharti Ya Pili: Yaqini, inayoondosha shaka.

 

 

Sharti Ya Tatu: Kukubali, kunakozuia kupinga.

 

 

Sharti Ya Nne: Kunyenyekea, kunakopinga kuacha.

 

 

Sharti Ya Tano: Ikhlaasw, inayopinga kumshirikisha.

 

 

Sharti Ya Sita: Ukweli, unaopinga kukadhibisha.

 

 

Sharti Ya Saba: Kupenda, kunako pinga chuki.

 

 

Ama tafsili ya masharti haya ni kama ifuatavyo:

 

 

Sharti Ya Kwanza: 'Ilmu (Elimu, Maarifa, Ujuzi, Utambuzi).

 

 

Anakusudia 'Ilmu kwa maana yake inayokusudiwa, maana inayopinga na inayothibitisha, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴿٨٦﴾

Na wala wale wanaowaomba badala Yake hawana uwezo wa kumiliki uombezi isipokuwa yule aliyeshuhudia kwa haki nao wanajua. [Az-Zukhruf: 86]

 

Ameshuhudia kwa لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ ilihali wanajuwa kwa nyoyo zao, kile kilichoshuhudiwa na ndimi zao, na lau mtu akitamka bila kujua maana yake, hiyo Shahaada haitamnufaisha, kwa sababu hajaizingatia ile maana inayo julishwa na لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ.

 

 

 

Sharti Ya Pili:  Yaqini:

 

Nayo ni kuwa aliyeitamka ana yaqini na maana inayojulishwa na tamko hilo, na kama atatia shaka kwenye maana ya لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ   basi neno hilo halitamsaidia na hatopata manufaa yake, anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا  

Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Rasuli Wake, kisha wakawa si wenye shaka [Al-Hujuraat: 15]

 

Akiwa mwenye mashaka mtu huyo huwa ni mnafiki. Na katika Hadiyth:

 

 وقال النبي صلى الله عليه وسلم مَنْ لَقِيتَ مِنْ وَرَاء هَذَا الْحَائِطِ يَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاّ اللّهُ مُسْتَيْقِنا بِهَا قَلُبُهُ فَبَشّرْهُ بِالْجَنّةِ))

((Ee Abaa Hurayrah (akanipa viatu vyake) Nenda na viatu vyangu hivi, utakayemkuta nyuma ya ukuta huu akiwa anakiri moyoni na anashuhudia kwamba: لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ   )laa ilaaha illa Allaah( hapana muabudiwa wa haki ila Allaah akiwa amethibitika nayo moyoni, mbashirie Jannah)) [Muslim]

 

Yeyote ataekosakuwa na yaqiini kwenye moyo wake hatostahiki kuingia Jannah.
 

 

 

Sharti Ya Tatu: Kukubali

 

Kile kinachopelekea (kumaanisha) kwenye hili neno, ambayo ni kumwabudu Allaah Pekee, na kuacha kila aina ya ‘ibaadah isiyokuwa ya Allaah (عز وجل), atakayetamka bila kukubali moyo wake, na bila kulazimiana na neno hilo, huyo atakuwa kwenye kundi ambalo amesema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu hao:

 

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٣٥﴾ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ ﴿٣٦﴾

 

Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: Laa ilaaha illa Allaah, Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, hutakabari. Na wanasema: Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi majnuni?! [Asw-Swaffaat: 35 – 36]

 

Na ndio kama hivi, hali ya waabudia makaburi, kwani wao wanatamka لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ na wala hawaachi kuabudia makaburi, hawa wanakuwa hawajakubali bado maana ya لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ.

 

 

 

Sharti Ya Nne: Kunyenyekea.

 

Kwa kile kilichojulishwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَن يُسْلِمْ وَجْهَهُ إِلَى اللَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ

Na anayeusalimisha uso wake kwa Allaah, naye akawa ni mtenda ihsaan, basi kwa yakini ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika. [Luqmaan: 22]

 

  العُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ

 

Kishikio madhubuti ni:  لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ

 

Na maana ya

يُسْلِمْ وَجْهَهُ

 

anayeusalimisha uso wake ni: Kunyenyekea kwa Allaah kwa Ikhlaasw.

 

 

 

Sharti Ya Tano: Ukweli.

 

Mtu anatakiwa atamke neno la لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ kwa moyo wake ukiwa unasadikisha kile kinachotamkwa na ulimi wake,  kama atatamka kwa ulimi ilihali moyo hausadikishi hilo, mtu huyu anakuwa ni mnafiki, anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ ﴿٨﴾ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَمَا يَخْدَعُونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿١٠﴾

Na miongoni mwa watu wako wasemao: Tumemuamini Allaah na Siku ya Mwisho hali ya kuwa si wenye kuamini. (Wanadhani) Wanamhadaa Allaah na wale walioamini lakini hawahadai ila nafsi zao na wala hawahisi. Ndani ya nyoyo zao mna maradhi na Allaah Akawazidishia maradhi, na watapata adhabu iumizayo kwa waliyokuwa wakiyakadhibisha. [Al-Baqarah: 8 – 10]

 

 

 

Sharti Ya Sita: Ikhlaasw:

 

Nako kusafisha ‘amali kutokana na takataka za ushirikina, asikusudie kwa kauli yake tamaa fulani katika tamaa za kidunia, wala Riyaa (kujionyesha kwa watu), wala kutaka umaarufu kwa watu, imekuja katika Hadiyth:

 

عن عِتْبَانَ بْن مَالِكٍ الْأَنْصارِيَّ رضي الله عنه أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ قَدْ حَرَّمَ عَلَى النَّارِ مَنْ قَالَ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ يَبْتَغِي بِذَلِكَ وَجْهَ اللَّهِ ))

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Itbaan bin Maalik Al-Answaariyy Radhhwiyaa1 kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ameharamisha An-Naar (Moto) kwa anayesema:  لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ (laa ilaaha illa Allaah) akitafuta Wajihi wa Allaah.” [Al-Bukhaariy (425), Muslim (33)] 

 

 

 

Sharti Ya Saba: Kupenda:

 

Nako ni kulipenda Neno la لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ pamoja na maana yake na kuwapenda wanaolifanyia kazi Neno hilo, kwa mujibu wa maana yake, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ  

Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah.  [Al-Baqarah: 165]

 

 

Watu wa لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ wanampenda Allaah mapenzi yenye Ikhlaasw, na watu washirikina wanampenda Allaah na wanapenda vitu vingine na hivi huwa vinapinga maana na malengo yake.

 

 

Masharti Ya Shahaadah مُحَمد رَسُول الله

 

 

Masharti ni kama yafuatayo:

 

 

Sharti Ya Kwanza:

 

Kukiri (kukubali) Risala yake na kuiitakidi (kuuamini) katika moyo.

 

 

Sharti Ya Pili:

 

Kutamka na kukiri kwa dhahiri (kutamka) kwa ulimi.

 

 

Sharti Ya Tatu:

 

Kumfuata Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kukifanyia kazi alichokuja nacho, ambayo ni haki, na kuacha aliyoyakataza ambayo ni baatil.

 

 

Sharti Ya Nne:

 

Kumsadikisha kwa yale aliyoyaelezea, katika mambo ya ghaib (yaliyo jificha), yaliyopita na yajayo.

 

 

Sharti Ya Tano:

 

Kumpenda yeye zaidi ya kuipenda nafsi mali, watoto wazazi na watu wote.

 

 

Sharti Ya Sita:

 

Kuitanguliza kauli yake kabla ya kauli ya mtu yoyote yule, na kuzifanyia kazi Sunnah zake.

 

Tafsiyr ya Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ﴿١٩﴾

Basi jua kwamba: hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. Na Allaah Anajua harakati zenu huku na kule na pahala penu pa kupumzikia. [Muhammad (47:19)]

 

 

Yanayopelekea Kutambua Ujuzi Wa Laa Ilaaha Illa-Allaah:

 

 

Kulijua ipasavyo neno “Laa Ilaaha Illa Allaah” kunahitajia moyo kulikiri na kulijua, kwa maana kwamba Rasuli (pamoja na sisi) anatakiwa alijue neno hilo inavyotakikana, halafu akamilishe ujuzi huo kwa kutenda kwa mujibu wa vipengele vyake.

 

Ilimu hiyo ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameiamuru - ambayo ni ilimu ya Tawhiyd (Kumpwekesha Allaah) ni fardhw ‘ayn (faradhi kwa kila mtu binafsi), kwa kila mwanaadam, na haisamehewi kwa yeyote yule, na haijalishi yeye ni nani. Bali kila mtu amewajibika kuijua. Na njia ya kujua kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye (Allaah عزّ وجلّ) ni kwa haya yafuatayo:  

 

 

(i) Ya kwanza bali iliyo kuu kabisa ni kuzingatia Majina Yake (Allaah عزّ وجلّ) na Sifa Zake na Matendo Yake yanayodalilisha Ukamilifu Wake, na U’adhwama Wake, na Ujalali Wake, kwani yanampelekea mtu kufanya jitihada ya kujisabilia Kwake, na kumwamudu Rabb Anayemiliki Majina Mazuri Kabisa Na Sifa, na Ambaye Himdi zote ni Zake, Utukufu, Ujalali na Uzuri. 

 

 

(ii) Kujua kwamba Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Muumbaji Pekee na Msimamizi. Hivyo basi mtu atambue kuwa Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Pekee Mwenye Kustahiki kuabudiwa.

 

 

(iii) Kujua kwamba Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Pekee Mwenye Neema za dhahiri (zinazoonekana) na za siri (zisizoonekana) za kidini na za kidunia. Kujua hilo kunaulazimisha moyo kushikamana Naye na Kumpenda na kujisabilia Kwake Yeye Pekee, Asiye na mshirika.

 

 

(iv) Yale tunayoyaona na kuyasikia juu ya malipo kwa mawalii Wake waliosimamisha Tawhiyd Yake (Allaah عزّ وجلّ), kama vile ushindi na neema za haraka za hapa duniani, pamoja na adhabu zake kwa maadui Zake wanaomshirikisha, hayo yote ni chachu ya kujua kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Pekee Anayestahiki kuelekezewa ibaada zote.

 

 

(v) Kujua hali halisi ya masanamu na mizimu na wanaolinganishwa sawa na Allaah (سبحانه وتعالى) ambao wanaabudiwa pamoja na Allaah, na kufanywa ni waabudiwa, na kwamba hao ni wenye upungufu kwa kila upande, ni madhaifu wa dhati, hawana uwezo wa kujinufaisha au kujidhuru nafsi zao wala kwa wanaowaabudia,   wala hawana uwezo wa kufisha, wala kuhuisha, wala kufufua, wala hawawezi kuwanusuru wanaowaabudia, wala hawawezi kuwanufaisha hata kwa uzito wa chembe ya atomu kwa kuleta kheri au kukinga shari. Basi kwa kujua hayo, kunawajibisha kujua kwamba hapana Mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba miungu inayoabudiwa badala Yake (Allaah عزّ وجلّ) ni ya uongo.

 

 

(vi)  Vitabu vya Allaah vyote vimeafikiana juu ya hilo (Neno la Tawhiyd; laa ilaaha illa-Allaah) na vyote kimoja baada ya kingine vimeelezea hilo.

 

 

(vii) Viumbe bora kabisa ambao wamekamilika katika khulqa (tabia) njema, akili, busara, fikira sahihi, hikma, na ilimu, yaani Rusuli wa Allaah na Manabii na ‘Ulamaa wenye taqwa, wameshuhudia hayo (kwamba laa ilaaha illa-Allaah).

 

 

(viii) Ishara za kilimwengu na za kinafsi (namna tulivyoumbwa) Alizozisimamisha Allaah na ambazo zinaonyesha kwamba Yeye Ni Mmoja Asiye na mshirika, ndizo dalili kubwa kuliko zote. Dalili hizi kwa namna Alivyoziumba kwa uzuri wa ajabu, kwa umadhubuti usiyo na kombo, na kwa uumbaji wa ajabu, zote zinamtangaza Allaah kwa jinsi zilivyo kwa namna ya kipekee kabisa isiyo na ruwaza. Ishara hizi ambazo Allaah Amekithirisha kwazo kuwazindusha viumbe, Akiwajulisha kwamba hakuna mwingine wa kuabudiwa isipokuwa Yeye, Akazieleza katika Kitabu Chake na Akazitawanya kote kote, ikiwa mtu atataamuli kwa kina baadhi yake tu, basi ni lazima atapata yakini na ujuzi wa kweli wa maana ya kumpwekesha Allaah (Tawhiyd). Sasa hali itakuwa vipi ikiwa dalili zote zitakusanyika pamoja, zikaoana, zikakubaliana na zikasimama toka pande zote?! Hapa ndipo pale iymaan na ujuzi wa hilo vinapojikita na kutuama ndani ya moyo wa mja na kuwa mithili ya mlima mrefu usiyoweza kutikiswa na shubha au dhana hewa, bali huzidi nguvu na ustawi kila mtu anapokutana na upotoshaji na propaganda chafuzi. Mwisho wa yote, unabakia mlango mkubwa na mpana zaidi wa kumwezesha mtu kuijua Tawhiyd kwa mapana yake na marefu yake. Mlango huu ni kuizingatia Qur-aan Tukufu na kuzitafakari Aayaat zake, na hili halipatikani toka chanzo kingine chochote isipokuwa humo.

[Tafsiyr As-Sa’diy]

 

 

 

 

 

Share