02-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Utangulizi Wa Mtungaji

Sifa zote zamstahiki Allaah سبحانه وتعالى Ambaye Amesema katika aayah iliyo wazi kwenye Kitabu Chake:

 

 

 

((وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ))

 

 

((Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri)) (Ar-Ruum 30: 21)

 
Na Swalah na Salaam zimwendee kipenzi Chake Muhammad ambaye amesema katika Hadiyth Swahiyh:

 

 

((تَزَوَّجُوا الْوَدُودَ الْوَلُودَ فَإِني مُكَاثِرٌ بِكُمُ الأَنْبِيَاءَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ))

((Oeni wapenzi wazaao, kwani nitashindana na Mitume wengine kwa idadi ya wafuasi siku ya Qiyaamah)).[1]

Baada ya utangulizi huu:

 

Katika Uislamu kuna desturi na taratibu ambazo zatakikana kufuatwa na za mtu anayeoa au anayetaka kufunga ndoa. Waislamu wengi leo hata wale ambao wanajitahidi katika ibada mbali mbali, hawajui kabisa hizi desturi za Kiislamu. Kwa hiyo, nimeamua kuandika makala hii ndefu yenye faida kwa kuelezea wazi mambo haya katika mnasaba wa harusi ya mtu ambaye ni kipenzi changu. Natumai kuwa itamsaidia yeye na ndugu wengineo waumini katika kumfuata Bwana wa Mitume alivyotuamrisha kutokana na amri ya Mola Wa Ulimwengu.

 
Baada ya hapo nimetahadharisha kuhusu baadhi ya mas-ala muhimu kwa kila anayeoa, na ambayo yamekuwa ni mitihani kwa wake wengi.

 

Namuomba Allaah سبحانه وتعالى Ajaaliye kitabu hiki kiwe ni chenye manufaa na Ajaaliye kazi hii iwe ya ikhlaas yenye kumridhisha Yeye Pekee kwani Yeye Ndiye Mwema na Rahiym.

 

 

 

Ifahamike kwamba kuna desturi nyingi katika sherehe za ndoa, lakini yaliyonishughulisha zaidi katika uandishi huu wa haraka, ni yale mambo yaliyo Sahihi katika Sunnah za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Muhammad ambayo hayawezi kukanushwa kutokana na msimamo maalumu wa mfululizo wa usimulizi (sanad) ambao hauna shaka katika muundo wake na maana yake. Hivyo yeyote atakayesoma na kufuata maelezo haya atakuwa katika msingi uliothibiti wa Dini yake na atakuwa katika hali ya matumaini ya uhalali wa vitendo vyake.

 
Namuomba Allaah سبحانه وتعالى Amkhitimishe kwa furaha na thawaab kwa kuanza maisha yake ya ndoa kwa kufuata Sunnah na Amjaaliye miongoni mwa waja Wake Aliyewaelezea katika kauli Yake:

 

 

((وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا))

 

 

((Na wale wanaosema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na watoto wetu yaburudishayo macho, na Utujaalie tuwe waongozi kwa wachaji Allaah)) (Al-Furqaan 25: 74)

 

Na mwisho mwema ni wa waja wanaomcha Allaah kama Anavyosema Mola wa Ulimwengu:

 

 

 

((إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي ظِلَالٍ وَعُيُونٍ ﴿41 وَفَوَاكِهَ مِمَّا يَشْتَهُونَ ﴿42 كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿43 إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنينَ))

 

 

((Hakika wachaji Allaah watakuwa katika vivuli na chemchem. Na matunda wanayoyapenda. Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.  Hakika ndio kama hivyo Tunavyowalipa watendao mema)) (Al-Mursalaat 77: 41-44)

 

 

 

Adabu na desturi hizo ni hizi zifutazo:

 

 

[1] Ahmad na At-Twabaraaniy kwa isnaad iliyo hasan, na Ibn Hibbaan amekiri kuwa ni Swahiyh kutoka kwa Anas

Share