21-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Kutofanya ‘Azl Ni Bora Zaidi

Kutokufanyika hiyo ‘azl kunapendekezwa kutokana na sababu mbalimbali:

Kwanza:

Ina madhara kwa mwanamke kwa vile inampunguzia starehe ya tendo lile kwani anayefanya hiyo ‘azl huwa anamkatisha kufika kileleni. Na hata ikiwa amekubali mwenyewe, bado kutakuwa kuna upungufu ufuatao:

 

Pili:

Tendo hilo linakanusha mojawapo ya kusudio la ndoa ambalo ni kukuza Ummah Wa Kiislamu kutokana na kizazi kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم:

 

((تَزَوَّجُوا الْوَدُودَ الْوَلُودَ فَإِني مُكَاثِرٌ بِكُمُ الأَنْبِيَاءَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ))

((Oeni wapenzi wazaao, kwani nitashindana na Mitume wengine kwa idadi ya wafuasi siku ya Qiyaamah))[1]

Na hii ndio maana Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alifananisha kama ni 'uuaji mdogo wa watoto wadogo' (ingawa si kama imeharamishwa kama 'uuaji wa watoto wadogo ilivyoharamishwa). Alipoulizwa alisema:

 

((ذََلِكَ الْوأد الْخَفِيِّ )).

 

((Huu ni uuaji wa siri wa watoto wadogo))[2]

Kwa sababu hii pia, yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alionyesha kwamba kutokufanya ni bora zaidi katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Sa'iydil-Khudriy رضي الله عنه akisema "’azl ilitajwa akiweko Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na akasema:

 

((ولم يَفْعَلْ ذَلِكَ أَحَدكُمْ؟!)) ( وَلَمْ يَقُلْ: فَلاَ يَفْعَلْ ذَلِكَ أَحَدكُمْ)  (( فَإَنَّهُ لَيْسَتْ نَفْس مَخْلُوقَةٌ إِلاَّ الله خَالِقُهَا))  وفي رواية ، فقال: ((وَإِنَّكُمْ لَتَفْعََلُونَ، وَإِنَّكُمْ لَتَفْعََلُونَ، وَإِنَّكُمْ لَتَفْعََلُونَ  مَا مِنْ نِسْمَةُ كاَئِنَة إِلى يَوْمِ اْلقِيَامَة إِلاَّ هِيَ كَائِنَة))  

((Kwa nini anafanya mmoja wenu?)) (tanbihi kwamba hakusema "asifanye mmoja wenu") ((Allaah Ndiye Muumba wa kila nafsi)) [3]

 
Katika riwaaya nyingine amesema: ((Mtafanya, mtafanya, mtafanya. Hakuna idadi ya watu iliyopo hadi siku Ya Qiyaamah ila itabaki)) (itakuwepo) (Maana: Hakuna mtu atakayeweza kupangua mipangilio aliyopanga Allaah, yaani kama hata mtu akitaka kuzuia kiumbe kisije kwa kufanya 'azl', basi kitakuja tu maadam Allaah Keshapanga iwe hivyo. Wa Allaahu A'alam)

 


[1] Abu Daawuud, An-Nasaaiy na wengineo: Swahiyh

[2] Muslim, Ahmad na Al-Bayhaaqiy

[3] Muslim

Share