Kulazimika Kutoa Rushwa Kwa Sababu Ya Matibabu

 
SWALI:
 
 
Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh Kwanza kabisa natoa shukurani zangu za dhati kwenu kwa kutupa majibu yenye manufaa na kutufunua macho na masikio yetu kwa kutupa majibu ya tusiyoyajua.
 
Napenda kutuma swali langu la kwanza kwa kuuliza hivi:- Katika miaka na karne tuliyonayo ni asilimia kubwa sana hakuna uwezekano wowote wa kupata haki yako bila ya kutoa rushwa.
 
Inafahamika wazi kwamba hata kama kitu ni haki yako lakini usipotoa rushwa utazungushwa sana na hatimae hutoipata haki hiyo na kupangiwa tarehe kila siku. Kadhalika ambacho kinatusikitisha zaidi ni kuwa hata tiba nzuri kuipata ni mpaka utoe rushwa. Ukienda spital na usipokuwa na dokta unayemfahamu ama kutoa chochote basi si ajabu ukazungushwa bila ya tiba au kupaiwa tia isiyo sahihi mpaka maradhi yakuzidi na kuleta athari zaidi.
 
 Upo mfano ulio wazi kwa jirani yangu ambaye hakuwa na uwezo wa kuzaa kwa njia ya kawaida. Siku ya kufanyiwa upasuaji ilifika lakini kila siku ilikuwa ikisogezwa mbele mpaka alipopata pesa na kutoa rushwa ili apatiwe huduma hiyo.
 
Sasa kutokana na matatizo kama haya. Sisi Waumini wa dini ya kiislam tuyachukulie vipi??? Ahsante
 
 


 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Ifahamike kuwa rushwa imepigwa vita vikali na Uislamu kwani huko ni kula mali za watu kwa dhulma na batili. Hiyo ni kuwa mwenye kutoa ima anataka kupata kisichokuwa chake au apitishiwe hukumu dhidi ya mgomvi wake. Dhulma na kula mali kwa batili imeharamishwa katika Uislamu kwani kufanya hivyo ni kuwanyanyasa wenzio. Kutoa na kupokea rushwa (hongo) kote kumekatazwa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Wala msiliane mali zenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua” (2: 188).
 
Katika hilo amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Amelaaniwa na Allaah mwenye kuhonga na mwenye kuhongwa katika hukumu” (Ahmad, at-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan).
 
Na imepokewa kutoka kwa Thawbaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema: amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani: “Mtoa rushwa, mlaji rushwa na tarishi baina yao (Ahmad na al-Haakim).
 
Ikiwa mchukuaji rushwa amechukua ili adhulumu basi ni uhalifu mkubwa sana huo alioufanya na siku ya Qiyaamah atakuwa na cha moto kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ogopeni dhulma, kwani dhulma ni kiza Siku ya Qiyaamah” (Muslim).
Lau atafanya uadilifu atakuwa hana haja ya kuchukua chochote na malipo yake yatakuwa makubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka.
 
Si ajabu kwa Uislamu kuharamisha rushwa na kutia mkazo juu ya kila aliyeshiriki katika jambo hilo, kwani kuzagaa katika jamii ni kuzagaa kwa ufisadi, dhulma, kurudisha nyuma maendeleo na kuongeza fitna. Hiyo inaleta hisia katika jamii ya kujinufaisha na sio ya kutekeleza wajibu na kutumikia wananchi.
 
Sasa hebu tuingie katika kiini cha suala lako ambalo ni nyeti sana, nasi hatujui uhakika wa hayo isipokuwa yale uliyotuelezea. Nasi kama Waislamu tuna dhana nzuri kuwa uliyoyasema ni ya kweli na ni kama yalivyo kabisa. Ikiwa sivyo basi fahamu ya kwamba jukumu hilo utalibeba mwenyewe.
 
Awali ya yote ni wajibu wa Muislamu na Waislamu kutetea haki zao kwa njia zote zilizo sahihi. Hivyo, haifai kusalimu amri kwa sababu ya matatizo ambayo yanaonekana yamewakabili mpaka ikabidi mtoe hongo. Hilo si suluhisho bali ni kujiletea taabu za ziada katika jamii hiyo mnayoishi.
 
Ikiwa hospitali ni ya kibinafsi sidhani kama shida kama hizo zitatokea kwani wao ndio wanapatia riziki hapo na wanajaribu kuiboresha ili wapate wateja zaidi. Yaonyesha kuwa hospitali hii ni ya serikali ambamo mambo haya yanafanyika. Hivyo, ni lazima mfanye juhudi kwa kwenda kwa wakubwa wa hospitali yenyewe kuwalalamikia kuhusu tatizo hilo ambalo laonyesha limekuwa sugu. Ikiwa hamkufanikiwa basi muelekee kwa wizara ya afya kupeleka malalamiko yenu. Kisha mtakwenda kwa vyombo vya habari. Katika haya yote ni lazima wanajamii washirikiane kwa hilo ili waweze kufanikiwa kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ikiwa haya yote mliyoyafanya hamkufanikiwa kabisa basi hapo ni katika kuokoa maisha ya wagonjwa wenu ambao wako katika hali mahututi na itakuwa ni katika hali ya dharura tena.
 
 
Jaribuni kutetea haki zenu kama wananchi katika nchi yoyote mliopo na Allaah Aliyetukuka Atakusaidieni.
 
 
Na Allaah Anajua zaidi
Share