Amezini Na Mwanamume Asiye Muislamu Akapata Mtoto Hakumjulisha Mumewe.

SWALI:
 
 
Asalaam aleykum,
 
Inamshukuru ALLAAH s.w) kwa kuifahamu Alhidaaya.
 
Swali? mwanamke alieolewa kisha akabarikiwa watoto wawili wakiume katika ndoa yake.Baadae akaenda nje ya ndoa, maana ya kua kazini na mwanamume mwingine ambae si mume wake tena si muislam na hatimae pakapatikana mtoto wakike katika zina hiyo bila kumfahamisha mumewe habari za mtoto huyu .Ni hatua gani mume wamwanamke huyu anatakiwa aifanye kwa misingi ambayo haita mkasirisha ALLAAH (s.w ) baada yakugundua jambo hili. Shukran.
 
 

JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hili kuhusu tendo la zinaa. Hili limekuwa ni tatizo sugu katika jamii yetu ya Waislamu. Tatizo jingine ni wasichana wetu ima kuzini na Waislamu au wasiokuwa Waislamu kwa kuwa wazazi wameweka mahari makubwa kwa mabinti zao, ambayo vijana wanashindwa kumudu. Matokeo yake ni kuwa vijana hao wawili wanatoroshana au asiye Muislamu anakuja na mahari makubwa kumletea mzazi ambaye anamtoa binti yake akidhania kuwa anakwenda kuolewa huku hajui kuwa wawili hao wanazini. Sheria imeliweka wazi kabisa jambo hili kuwa msichana Muislamu hawezi kabisa kuolewa na asiyekuwa Muislamu.
 
Swali lililoulizwa linaashiria kama tunavyoliona kuwa ni kosa kubwa kuwa mwanamke Muislamu amezini na asiyekuwa Muislamu kama kwamba si hatia akifanya hiyo zinaa na Muislamu. Tufahamu kuwa zinaa ni zinaa ikiwa utaifanya na Muislamu au asiyekuwa Muislamu.
 
Jambo la zinaa katika Uislamu ni dhambi kubwa na ndivyo adhabu yake ni kali sana. Kwa ukali wa adhabu yake Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametaka washuhudie watu wanne miongoni mwa Waislamu kwa kufanyika kitendo hicho chenyewe. Pia inatakiwa ifahamike kuwa:
 
Na wale wanaowasingizia wanawake watahirifu (kuwa wamezini), kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigane mijeledi thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao wao tena, na hao ndio mafasiki” (24: 4).
 
Hii ni adhabu ya mwenye kusingizia katika suala hilo. Ieleweke kuwa lau mwanamume au mwanamke aliyeoa au kuolewa atapatikana na kosa hilo adhabu yake ni kupigwa mawe mpaka wafe na wakiwa hawajaoa au kuolewa basi ni mijeledi mia moja. Hili ni suala gumu na linaweza kumuingiza muulizaji au msambazaji habari pahala pabaya hapa duniani na Kesho Akhera.
 
Sijui muulizaji ana uhusiano gani na mume wa mke huyo na habari hizi kazipata wapi? Kwa nini, mume mwenyewe asiulize swali hilo? Maswali ambayo yanaweza kujitokeza ni mengi, lakini la muhimu ni kuwa je, wapo mashahidi walioona kitendo hicho au ni habari za kusikia na kushuku tu? Ikiwa ni kusikia na kushuku basi tujue kuwa Uislamu hauendi hivyo.
 
Ikiwa ni fununu tu ambazo mume anasikia naye akaingia shaka inatakiwa azungumze na mkewe kinaganaga kuhusu hilo. Na jambo hili si geni kwani lilimtokea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo kupata muongozo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Wanafiki wakiongozwa na ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluul baada ya Vita vya Banu Mustwaliq walieneza masingizio kuwa mkewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mama wa waumini ‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anha) amezini na Swafwaan bin Mu’utwtwaal as-Sulamiy (Radhiya Allaahu ‘anhu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza na mkewe kuwa lau umefanya kitendo hicho basi rudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) uombe msamaha na kama hukufanya basi Allaah Atatufunulia hilo. Hapo mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akalia na kutaka babake amjibie, naye akashindwa kusema chochote. Baadaye akasema kwa kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wazazi wake kuwa lau nitasema sikufanya hamutaniamini na nikiwaambia kinyume chake mtaniamini. Sina la kusema ila kauli ya babake Yuusuf (‘Alayhis Salaam): “Subira ni njema” (12: 83). Na ndipo Allaah (Subhaanhu wa Ta’ala) Akateremsha maneno Yake katika Surah An-Nuur kumtakasa na kumsafisha mama wa waumini ‘Aaishah na tuhuma alizotuhumiwa na hao wanafiki.
 
 
Ikiwa mke katika mazungumzo hayo atasema mimi sijafanya basi inatakiwa umwamini isipokuwa kunapokuwa na ushuhuda madhubuti wa kisheria kama tulivyotaja hapo awali. Ikiwa atakiri kuwa amefanya kosa hilo, hapo itategemea maelewano na mumewe. Inawezekana kuwa mke huyo kwa kufanya kitendo hicho akajuta na kuweka azma ya kutorejea tena, mume anaweza kumsamehe na wakaendelea kuishi pamoja kama awali (mume na mke). Lau ataona kuwa hawezi tena kukaa naye basi atamuacha kwa kumpatia talaka.
 
Lakini tunarudia tena inatakiwa tuwe na tahadhari kuhusu mas-ala haya ya zinaa. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Atuepushe na uchafu huo kabla ya kuoa au kuolewa na hata baada yake.
 
Na Allaah Anajua zaidi.
 
 
Share