10-Uswuul Al-Fiqhi: Wakati Wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

 

 

Maymuun bin Mahraan alifupisha utaratibu wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliokuwa akiutumia kwenye kufikia maamuzi kama ifuatavyo:

 

Mgogoro unapofikishwa kwake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliangalia ndani ya Qur-aan, kama atapata chochote kwa mujibu wa hilo na ataweza kutoa hukumu, alifanya hivyo. Kama hatopata kuona suluhisho ndani ya Qur-aan, lakini akakumbuka kipengele fulani cha mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), atatoa hukumu kwa mujibu wa hiyo (Sunnah). Kama hatopata kuona kitu chochote ndani ya Sunnah, atakwenda na kuwaambia Waislamu: “Mgogoro fulani na fulani umefikishwa kwangu. Yupo yeyote kati yenu anayetambua chochote katika mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa huo (mwenendo) hukumu inaweza kutolewa?Kama yeyote ataweza kujibu suala lake na kutoa maelezo yenye kufanana, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) husema: “Shukrani ni za Allaah Ambaye Amemuwezesha miongoni mwetu kukumbuka walichojifunza kutoka kwa Mtume wetu.” Kama hatopata kuona suluhisho lolote ndani ya Sunnah, basi atawakusanya viongozi na watu walio bora kabisa na kushauriana nao. Kama watakubalina kwenye suala, basi atatoa hukumu kwa msingi huo[1].

 

Kama taratibu zote hapo juu zitashindwa kufikia mwisho wowote, basi atafanya Ijtihaad na kutengeneza mawazo yake mwenyewe, aidha kwa kutolea maana ya andiko katika namna ambayo maana halisi itakuwa wazi, au kwa kufanyia kazi uwerevu wa akili yake ya kisheria.

 

Mfano wa Ijtihaad ya aina ya mwanzo ni pale alipoulizwa kuhusu Kalaalah Akijibu, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Mawazo yangu, kama ni sahihi, basi ni kutoka kwa Allaah, na kama si sahihi, basi ni kutoka kwangu na Shaytwaan. Kalaalah ni yule asiye na mrithi kuendea juu wala mrithi kuendea chini”[2].

Mfano mwengine kama huo ni pale ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotamka kwake Hadiyth ifuatayo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Nimeamrishwa kupigana vita dhidi ya watu hadi waseme kwamba Hapana mungu isipokuwa Allaah…[3] na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Zakaah ni sehemu ya hiyo.[4]

 

Pale Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotaka kupigana vita dhidi ya wale wanaozuia kutoa Zakaah, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alinukuu Hadiyth hii kuonesha kwamba kupigana nao hakuruhusiwi kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema “…hadi waseme kwamba Hapana mungu isipokuwa Allaah. Kisha, kama watasema hivi, damu zao na mali yao haitosumbuliwa na mimi, isipokuwa kwa haki thaabit (yaani mpaka wafanye vitendo ambavyo vinaadhibiwa kwa mujibu wa Shariah ya Kiislamu.)

 

Kwa mujibu wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), vitendo hivi vilikuwa ni: uzinifu, mauaji, na kuritadi, kwa vile kuzuia kutoa Zakaah haikutamkwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwambia: “Zakaah ni sehemu ya hiyo, kwa ajili ya Allaah, nitapigana na yeyote aliyetekeleza Swalaah lakini hakulipa Zakaah! Kama yeyote atajaribu kuzuia kutokana na mimi, hata kiwango kidogo walichokuwa wakilipa kwa Mtume, nitakwenda nao vitani juu yake (Zakaah).

 

Mfano wa pili wa Ijtihaad ni pale alipoamua kwamba mama yake mama anaweza kurithi, lakini baba yake mama hawezi kurithi.

 

Baadhi ya Answaar walimwambia: “Unamruhusu mwanamke kurithi kutoka kwa aliyefariki, wakati yeye (mwanamme) hatorithi kutoka kwake (mwanamke) kama huyo (mwanamke) atakuwa na aliyefariki. Na unaacha bila ya chochote kwa mwanamke kutoka kwa yule (mwanamme) ambaye anaweza kurithi pale hali inapogeuka.” Baadaye Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliamua kwamba wote kuukeni na mabibi wa kuumeni watagawana moja ya sita ya urithi.

 

Mfano mwengine ni hukumu yake kwamba kila mmoja apokee mgao ulio sawa kutoka nyumba ya hazina baytul maal. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuuliza: “Utamuweka nafasi gani yule aliyeingia kwenye Uislamu akiwa na mashaka ya kuwa sawa na yule ambaye ameacha nyuma; nyumba yake na mali yake, na kuhama ili kuwa pamoja na Mtume?

 

Hata hivyo, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), alitilia mkazo kwamba: “Wote wameingia kwenye Uislamu kwa ajili ya Allaah, na malipo yao yapo Kwake Yeye; dunia hii si chochote.” Hata hivyo, pale ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa Khaliyfah, alitofautisha baina ya watu na kulipa “ujira” kwa mujibu wa kila mmoja alivoanza kuingia kwenye Uislamu, kama wamehama, na kiwango gani wameumia kwa ajili ya Uislamu.

 

Mfano mwengine wa namna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alivoifanya kazi ya Ijtihaad ni pale alipotofautisha uteuzi wa Khaliyfah kwa (kumuweka) mrithi wake, (tofauti) na ule uteuzi kwa njia ya Bay’ah. Hivyo, alimteua ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni Khaliyfah baada yake, na Maswahaba walikubaliana nae.

Khaalid bin al-Waliyd (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuandikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), kumwambia kwamba katika baadhi ya sehemu za Mkono wa Nchi za Kiarabu amekuta watu wakifanya vitendo vya liwaatw. Abu Bakr aliamua kushauriana na Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuchukua hatua ipi kuhusiana na hilo. Mmoja miongoni mwa Swahaabah alikuwa ni ‘Aliyy (Radhiya Allaahu ‘anhu), na hukumu yake ilikuwa ni kali kuliko zote.

 

Alisema: “Ovu lake lilitambulika kwa taifa moja tu, na unajua nini Allaah Aliwafanyia. Ninashauri kwamba watu hawa wachomwe hadi kufa.

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimjibu Khaalid kumwambia kwamba wachomwe hadi kifo; na hili lilifanyika.[5]

 

 

[1] Ad-Dahlaawiy, HujajatuLlaah Al-Baalighah, (Misri), I, uk. 315.

[2] Kuna khitilafu kuhusu maana ya neno Kalaalah. Kwa mujibu wa baadhi, lina maana ya wale waliokufa bila ya kuacha nasaba ya mrithi, wala kizazi, wala baba au babu. Wengine, hata hivyo wanaona lina maana ya wale wanaokufa bila ya kizazi, bila ya kujali kama amefuatiwa na baba au babu. Aya inayoelezea ndani ya Qur-aan inapatikana Surat an-Nisaai, 4:176. Na ilikuwa ni kutokana na msingi huu wa aya kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliamrisha kama alivyofanya. Sababu ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ilikuwa kwamba aya hiyo inaelekeza kwamba ndugu wa kike wa Kalaalah apatiwe nusu ya urithi, na kama huyo baba angelikuwa hai, huyo ndugu wa kike asingerithi chochote kutoka kwa Kalaalah. Hivyo, ijapokuwa Qur-aan haielezi suala hilo, ni uadilifu ulio wazi kwamba maana iliyokusudiwa ni kwamba huyo Kalaalah ni yule anayekufa bila ya kuacha nasaba ya mrithi pande yoyote.

[3] Hadiyth hii ni sahihi na imepokewa kutoka kwa Maimamu al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy, Ibnu Maajah, Ahmad, At-Twayaalisii, na wengineo.

[4] Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na maana ya kusema kwamba maana hiyo aliyoitoa kwa maneno ya Hadiyth hayakuwa na maana halisi. Isipokuwa, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alihisi kwamba mfumo wa shahaadah: “Hapana mungu isipokuwa Allaah.” Hakika ifahamike kwa mzunguko, kama lenye maana ya imani, ambapo imani inajumuisha vifungu vingi, kikiwemo Zakaah, na kuongezea kwa ahadi ya shahaadah.

[5] Ibn Qayyim, I’laam al-Muwaqqi’iyn.

Share