Kutumia Ukumbi (Hall) Unaotumiwa Na Makafiri Kwa Ajili Ya Kuswalia

 

SWALI:

Assalam aleikum.

Ndugu zangu katika Uislam. Swali langu ni: - JEE TWAFAA KUSWALI KWENYE HALL AMBALO WAKATI MWENGINE HUKODIWA NA WAKIRISTO KWA MAOMBI YAO YA JUMAPILI?

HALL LENYEWE SI KANISA WALA HALIKUJENGWA KAMA KANISA BALI NI HALL AMBALO HUKODIWA KWA MAMBO TAFAUTI TAFAUTI KAMA VILE SWALA YA SIKU IJUMAA KWA WAISLAMU, MADRASA KWA WAISLAMU SIKU YA IJUMAMOSI, MAOMBI YA WAKIRISTO SIKU YA IJUMAPILI NA MIKUTANO.JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hakujaalia katika Dini yetu Tukufu uzito wa aina yoyote. Kinyume chake ni kuwa Dini hii yetu imejengwa na usahali na tahfifu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuarifu kuwa yapo mambo matano ambayo hakupatiwa mwengine yeyote katika Ummah zilizopita. Moja wapo katika hizo ni: “Ardhi yote imejaaliwa mimi na Ummah wangu kuwa ni Msikiti na twahara” (al-Bukhaariy na Muslim).

Kwa minajili hii hakuna tatizo kabisa lenu nyinyi kulitumia hall hilo ambalo wakati mwingine hutumika kama Kanisa kuwa ni sehemu ya Ibadah au kufanyia shughuli nyingine za Kidini. Ikiwa mnatumia mikeka mtandika chini na kuendelea na Ibadah za Swalah au ikiwa mnaswali juu ya sakafu basi mnaweza kufagilia tu na hapo hall likawa tayari kwa minajili hiyo mnayotaka kuitumia kwayo.

Muhakikishe kuwa hakuna masanamu wala mapicha sehemu hiyo.

Kufagia au kuliosha kunakuja tu ikiwa mumeona najisi ambayo inabidi ioshwe lakini ikiwa hakuna mnaweza kufanya Ibadah zenu bila ya tatizo au wasiwasi aina yoyote. Ila mnatakiwa muwe mmefanya jitihada za kutosha za kutafuta sehemu nyingine isiyo na mashaka, na endapo mmekosa kabisa ndipo mnaweza kutumia sehemu hiyo.

Na Allaah Anajua zaidi

Share