Ni Lazima Kujisafisha Sehemu Za Siri Unapotaka Kufanya Wudhuu?

 

SWALI:

Napenda kujua ikiwa uko safarini au sehemu ya shughuli ni vigumu kupata kutumia Choo kwa haraka, je ikiwa hujabanwa haja yeyote unaweza kutawadha tu na kuswali bila ya kuingia chooni?? Hapa nina maanisha inawezekana hapo kabla umepata hewa, je inawezekana kutia udhuu tu bila kusafisha sehem za siri?? Wa Billahi Tawfiq

 


 

 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa mdugu yetu muulizaji swali. Ama kuhusu swali lako ni kuwa kwa ajili ya kutawadha si lazima uingie chooni. Ikiwa wudhuu kwa sababu moja au nyingine umetenguka ima kwa kutokwa na hewa, au kushika uchi wa mbele bila kizuizi, au kwenda haja kubwa au ndogo inakubidi wewe uchukue wudhuu.

Kwa hiyo, ikiwa huna haja ya kwenda chooni kwa ajili ya haja – kubwa au ndogo unaweza kuchukua wudhuu wako na utakwenda kuswali. Hata hivyo, ni kuwatanabahisha ndugu na dada zetu kuwa haifai mtu kuchukua wudhuu na kwenda kuswali na huku umebanwa na haja. Haifai kufanya hivyo kwani hutakuwa na unyenyekevu na kila wakati utakuwa unajibana ili mikojo isiwe ni yenye kutoka au haja kubwa. Hivyo, ikiwa unajitayarisha kwa ajili ya Swalah hakikisha kuwa hujashikwa na hali ya kwenda chooni kwa haja ya aina yoyote. 

Ama kina dada inahitajia wajiangalie kabla ya kwenda kuswali kwani huenda wakawa wametokwa na madhii, mabayo yanahitajika kusafishwa na kuchukua wudhuu kwa vile yanatengua wudhuu. Kwa maelezo zaidi kuhusu mas-ala haya ingia katika kiungo kifuatacho:

Tofauti Baina Ya Manii Na Madhii Na Hukumu Zake Za Ghuslu

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share