Kuweka Milio Ya Miziki Kwenye Simu Za Mkononi Au Qur-aan Inayosomwa Au Adhaana Au Du'aa

 

 

Kuweka Milio Ya Miziki Kwenye Simu Za Mkononi

Au Qur-aan Inayosomwa Au Adhaana Au Du'aa

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:  

 

Namshukuru Allah aliye niwezesha kuuliza swali na Allaah atawalipa mema.  Jee kuweka ring tone ktk simu ni vibaya? yaani ndio ikawa mlio wa simu.  Shukran wajazaakumu-Allahul khayra. musinisahau nami kunijibu ktk email yangu nisome kiurahisi  

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Twataraji kuwa majibu haya yatakayotolewa yatawafaidi wengi wenye tatizo . Awali ya yote tufahamu kuwa Mobile zimekuja na mazuri mengi kurahisisha mawasiliano baina ya watu. Lakini kama ilivyo vitu vizuri vingi huwa havikosi maafa na madhara vinapotumiwa kwa njia mbaya.

 

 

Ni hakika inayojulikana na kila mmoja kuwa vifaa hivi huwa vinaleta ghasia kubwa katika Misikiti na hivyo kuharibia unyenyekevu wa wenye kuswali wakati zinapoanza kulia na mbaya zaidi zinapokuwa na miziki. Jambo hili limepelekea katika Miskiti yetu kuwa Imaam baada ya tu kusema tengenezeni safu zenu, anakariri 'zimeni mobile zenu'. Hapo hapo tutakuta za wengineo zinalia watu wakiwa katika Swalaah. Haya yamekuwa ni maudhi na kero kubwa. Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾

Na wale wanaowaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike bila ya kuwa wamechuma kosa, basi kwa yakini wamejibebea usingiziaji mkuu wa dhulma na dhambi bayana. [Al-Ahzaab: 58]

 

 

Hakuna maudhi kama kumuharibia mtu Swalaah yake, ambayo ni 'Ibaadah kubwa katika Uislamu.

Sana

 

 

Kwa hakika shaytwaan ametupambia njia zake mpaka tukaziona kuwa ni nzuri na hivyo kuziendea kwa njia moja au nyingine.   Katika hizo shaytwaan ametufanya kuona kuwa muziki ni halali kabisa mbali na kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Anatuambia:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

6. Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha. 

[Luqmaan 31: 6]

 

 

'Abdullaah bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliapa kuwa maneno hayo ya upuuzi ni muziki na hivyo kuwa ni haramu kwa Muislamu, kusikiliza au yeye mwenyewe kuimba.

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha ala za muziki pale aliposema:

 

"Kutakuwa na watu miongoni mwa Ummah watakaohalalisha uzinzi, hariri, pombe na ala za muziki" [Al-Bukhaariy]

Hadiyth hii inatuashiria kwa kutujulisha kuwa ala za muziki ni haramu kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam) ametuambia kuwa wapo watu watakaoona kuwa zinaruhusiwa mbali na kuwa ni haramu. Pia ala hizo zimetajwa na vitu ambazo vinafahamika kuwa ni haramu uzinifu na pombe lau hazingekuwa haramu hazingetajwa pamoja navyo. 

 

Inawezekana kuacha kitu hicho cha haramu kwa njia rahisi kabisa kwa kuweka mlio wa kawaida au mlio mwingine wowote ambao si wa muziki. Hakika ni kuwa mlio wa muziki aina yoyote hauruhusiwi kuwekwa katika simu za mkono (mobile phones).

Japokuwa muulizaji hakuuliza swali la kuweka sauti za wasomaji wa Qur-aan kuwa ndio mlio wa simu tungependa kuwatanabahisha ndugu zetu kwa kuwaambia yafuatayo: 

 

Ni hakika isiyopingika kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambayo yanafaa yaheshimiwe kwa kiwango cha juu kabisa na kila Muislamu. Qur-aan imeteremshwa kuwa ni uongofu kwa wanaadamu wote alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ  

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185]

 

 

Qur-aan inafaa isomwe au isikilizwe kwa makini na kutafakari yaliyo ndani pamoja na kufuata. 

 

Kuiweka tu kuwa ni mlio huwa umeitweza kwa kiasi kikubwa kwa kuwa inaweza kuwa inalia nawe unazumgumza bila kujali. Au inalia na wewe kwa kuwa una haraka kuipokea unafanya hivyo hata kabla ya Aayah yenyewe kukamilika. Na tufahamu kuwa simu hiyo inaweza kupigwa ukiwa chooni na hivyo kuikosea heshima kabisa kwani ikiwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  likiwa limeandikwa mahali hufai kuingia na kitu hicho chooni na pia ikiwa hufai kulitaja katika sehemu hiyo seuze sasa Aayah zake zikawa zinasomwa katika sehemu hiyo – chooni.

 

Pia wengine huweka mlio wa Adhaana au Du’aa kwenye simu zao, nayo pia haipasi kwani havikuletwa hivyo  kwetu kwa ajili ya kumjulisha mtu kuwa anaitwa katika simu bali ni kwa ajili ya kujulisha wakati wa kuwadia Swalaah na kwa ajili ya kumwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Vilevile huenda ikamshughulisha mtu kudhani wakati wa Swalaah umeingia kumbe bado na pia huenda ikalia wakati wa Magharibi na mtu amefunga akadhani ni wakati wa futari na kumsababishia mtu kufungua kabla ya wakati!

 

Tunamnasihi kila mmoja katika ndugu zetu asiwe ni mwenye kuweka sauti za usomaji wa Qur-aan au Adhaana au Du’aa kama mlio wa simu bali aweke mtikisiko au mtetemo (vibration) au ikibidi waweke mlio wa kawaida wa asili ile milio ya kizamani ya simu.

 

Na muhimu wenye kuweka sauti kwenye mobile zao wawe wanazima simu zao wanapoingia sehemu Msikitini, kwenye Madarsa ya Dini, au kwenye Mihadhara ili wasiharibu Swalaah au utulivu wa waliohudhuria kusikiliza mafunzo ya Dini katika sehemu hizo, na pia kuheshimu sheria za nyumba ya Allaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share