Majuto Ya Nafsi - 1

Majuto ya Nafsi (1)

 

Alhidaaya.com

 

 

Unapoomba tawbah unakuwa unajitoharisha na madhambi na nafsi inakuwa katika hali ya kuridhiwa na Allaah (‘Azza wa Jalla) na kutoka hapo, Muumin  aendelee kurudi kwa Rabb wake kutubia kila mara anapokosea huku akijishughulisha kutenda ‘amali njema.  Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ﴿٥٤﴾

“Na rudini kila mara kutubu kwa Rabb wenu na jisalimisheni Kwake kabla kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa. [Az-Zumar: 54]

 

Maana; kimbilieni kuomba Tawbah na kufanya mema kabla ghadhabu za Allaah (Subhaanahu wa (Ta'aalaa) hazijakufikieni. 

 

Kisha Allaah (‘Azza wa Jalla) Anaendelea kutuhimiza kufuata Qur-aan ambayo ni Mwongozo  wetu kamili kwani humo yamo maamrisho na makatazo. Na kutofuata Mwongozo wa  Qur-aan humpelekea mtu akawa mbali na kumdhukuru Allaah (‘Azza wa Jalla)  na na hivyo basi kushughulishwa mambo ya dunia na kuisahua Aakhirah.  Kisha   yanapomjia mtu mauti kwa ghafla basi huwa hawezi tena kujisaidia kwani hakuna yeyote wa kumsaidia wala chochote kile alichokuwa akishughulika nacho duniani kuwa kitamfaa wakati huo. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla): 

 

 وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٥٥﴾

 “Na fuateni yaliyo mazuri Zaidi ambayo mmeteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu kabla haijakufikieni adhabu ghafla na hali nyinyi hamhisi.”  [Az-Zumar: 55].

Hapo wakati roho inatolewa  ndipo mtu anapojuta majuto makubwa, na kutamani  kurudi duniani atende mema lakini wapi haiwezekani kama  Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 ﴿٣٦﴾ هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ

“Mbali kabisa, mbali kabisa!“ [Al-Muuminuwn: 36].

 

Majuto ya nafsi yanaelezewa katika Aayah zifuatazo:

 

  أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ﴿٥٦﴾

Isije nafsi ikasema: Ee majuto yangu kwa yale niliyokusuru katika upande wa Allaah! Na hakika nilikuwa miongoni mwa wenye kufanya masikhara.” [Az-Zumar: 56].

 

Nafsi hulalamika hapo kwa mema ambayo mtu ameacha kuyatenda duniani, na pia kujuta kwa maovu aliyoyatenda mtu. Mifano ya majuto kama yafuatayo:

 

 

  • Yaa hasrataa!  (Ee majuto yangu!) kwa kutokumtii Allaah (‘Azza wa Jalla) Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwakutotimiza fardhi za Kiislaam!

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwa kutowatii wazazi wangu.

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwa kutoungana na jamaa zangu.

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwa kufanya maovu.

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwa kupoteza wakati wangu kwa mambo yasiyomridhisha Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

 

  • Yaa hasraata! Ulimi wangu umeniponza kuwateta wenzangu na kuwafitinisha.

 

 

  • Yaa hasraata! Kwa kutojielimisha Dini yangu!

 

 

  • Yaa hasrataa! Kwa kutohudhuria darsa na vikao vya elimu!

 

 

  • Yaa hasraata! Ya hasrataa! Yahasrataa …!

 

 

Al muhim, hapo nafsi itajuta kwa mengi ya kila aina!  Na kama Anavyosema Allaah (‘Azza wa Jalla) kuwa ilikuwa nafsi hiyo ikifanya maskhara kwa katika mambo ya Dini.   

 

Au pia maskhara hayo yalikuwa ya kufanyia istihzai Aayah za Allaah (‘Azza wa Jalla) kama vile kutafuta kuwaridhisha watu na kuwafurahisha watu.  Au istihzai katika  amri za Allaah (‘Azza wa Jalla) na Rasuli Wake ( Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); Mfano wale wanaofanya istihzai katika mavazi ya Waumini wanawake na Waumini wanaume wenye kutekeleza Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama vile kumfanyia istihzai Muumini anayefuga ndevu, au mwenye kuvaa kanzu isiyovuka vifundo vya miguu.   

 

 

…./2

 

 

 

Share