Majuto Ya Nafsi - 2

Majuto ya Nafs (2)

 

Alhidaaya.com

 

 

Nafsi inayotenda maovu inaendelea kujuta na kutamani kama mtu angelifuata Mwongozo. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ﴿٥٧﴾

“Au iseme: “Lau Allaah Angeliniongoa, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye taqwa.” [Az-Zumar: 57].

 

 

Basi mtu anapofikishwa na Allaah (‘Azza wa Jalla) kuonyeshwa adhabu zake kwa sababu ya kutokumtii alipokuwa duniani, hutamani kama angelipewa fursa arudi kufanya mema lakini wapi haiwezekani!  Kauli ya Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٥٨﴾

 “Au iseme pale itakapoiona adhabu: “Lau ningelikuwa na (fursa ya) marejeo (ya kurudi duniani) basi ningekuwa miongoni mwa watendao wema.” [Az-Zumar: 58]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea hali ya mtu anavyokuwa kuhusu majuto hayo yatakavyokuwa watu wa Motoni watakavyotamani makazi ya watu wa Jannah:

 

 

 ‏‏عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه  ‏ ‏قال: ‏قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وآله وسلم: ‏ ‏كل أهل النار يرى مقعده من الجنة فيقول لو أن الله هداني فتكون عليه حسرة قال: وكل أهل الجنة يرى مقعده من النار فيقول لولا أن الله هداني قال: فيكون له شكرا )) إمام أحمد‏‏

 

Abu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) amesimulia kwamba Nabiy (Swalla Alaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila mtu wa Motoni ataona makazi yake (aliyoandaliwa) Jannah atasema;  Laiti kama Allaah Angelinihidi! Kisha huwa majuto kwake.” Akasema; “Na kila mtu wa Jannah ataona makazi yake ya Motoni atasema; Kama ingelikuwa si Allaah kunihidi.” Akasema; “Kisha itakuwa sababu ya kushukuru kwake.” [Imaam Ahmad].

 

Na kama tunavyojua kuwa maisha ya Aakhirah ndio maisha ya milele, ilhali maisha ya dunia ni ya starehe fupi. Kama Anavyosema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 

 وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo; na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka hiyo ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua!” [Al -‘Ankabuwt: 64].

 

Nyumba hiyo ya Aakhirah ni ya wale wamchao Allaah (‘Azza wa Jalla) na wenye kufuata mafundisho na mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Anasema Allaah (‘Azz wa Jalla):

 

 وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۖ وَلَلدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يَتَّقُونَ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٣٢﴾

“Na maisha ya dunia si chochote isipokuwa ni mchezo na pumbao. Na bila shaka nyumba ya Aakhirah ni bora zaidi kwa wenye taqwa. Je, basi hamtumii akili?” [Al -An’aam: 32].

 

Lakini waovu hawatopata neema ya hiyo nyumba bora ya Aakhirah, bali malipo yao yatakuwa ni makazi mabaya ya motoni huku, wako katika majuto, baada ya kutambua kuwa wako katika khasara kubwa za nafsi zao pamoja na za jamaa zao. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾.

“Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi! Huko ndiko kukhasirika dhahiri.” [Az-Zumar: 15].

 

 

*****

 

 

 

Share