Hatari Ya Kuihama Qur-aan

 

Hatari Ya Kuihama Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anatuambia jinsi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Alivyokuwa akilalamika kuwa watu wake wameihama na kuipuuza Qur-aan:

 

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا ﴿٣٠﴾

Na Rasuli akasema: “Rabb wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan yenye kuhamwa. [Al-Furqaan: 30]

 

 

Makafiri Quraysh walikuwa hawataki kusikiliza Qur-aan, na ilipokuwa ikisomwa walikuwa wakizungumza upuuzi au kuzungumza kwa sauti za juu mazungumzo mengine ili wasiisikie.    

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ﴿٢٦﴾

 Na wale waliokufuru wakasema: “Msiisikilize hii Qur-aan na ifanyieni rabsha huenda mkashinda.” [Fusswilat: 26] 

 

Hali hii ya kuipuuza Qur-aan vile vile iko miongoni mwa Waislamu, ingawa Waislamu tofauti yake ni kuwa wameiamini na sio kama Makafiri Quraysh ambao ilikuwa ni dhaahiri  kuwa waliikanusha na kutoiamini.

 

Wafasiri Wa Qur-aan wameifafanua Aayah hiyo ya kwanza kuhusu:

 

رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا ﴿٣٠﴾

 “Rabb wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan yenye kuhamwa. [Al-Furqaan: 30

 

 

kwamba: kuihama na kupuuza Qur-aan inawahusu watu wa aina zifuatazo:

 

  • Wasioisoma kabisa.
  • Wanaoisoma lakini hawajifunzi maana yake.
  • Wanaoisoma na kujifunza maana yake lakini hawafuati maamrisho yake na hawajiepushi na makatazo yake.

 

Kuihama Qur-aan na kuipuuza ni hatari kubwa kabisa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuonya na Kututisha  kupitia Aayah nyingi za Qur-aan. Miongoni mwa maonyo hayo ni kwamba mja atakuwa na maisha ya dhiki na hufufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa kipofu:

 

وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾

 “Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu.”

 

قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾

Atasema: “Rabb   wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona?”

 

قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾

(Allaah) Atasema: “Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau   na kadhaalika leo umesahauliwa.”     [Twaahaa: 124-126]

 

Ndugu Waislamu tunaona hatari ya kuipuuza Qur-aan na kuihama basi na tujitahidi kuisoma, kujifunza maana yake na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake ili tuwe miongoni mwa wale Aliowasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika hii Qur-aan kuwa wanaisoma 'ipasavyo kusomwa' katika kauli Yake:

 

 الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٢١﴾

  Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo ya kusomwa kwake; hao ndio wanaokiamini, na atakayekikanusha basi hao ndio waliokhasirika.   [Al-Baqarah:121]

 

Zifuatazo ni kauli za Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)  kuhusu  'kuisoma  ipasavyo’

 

Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, Tilaawa ya kweli ni kufuata yaliohalalishwa na kuacha yaliokatazwa, kusoma kama ilivyoteremshwa, kutokubadilisha maneno katika sehemu zake na kutokuifasiri vingine na ilivyopasa kutafsiriwa" [Atw-Twabariy 2.567]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa): "Wenye kuhalalisha yaliyo halali na kukataza yalioharimishwa na hawabadilishi maneno yake".[Atw-Twabariy 2.567]

 

'Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Ni wale ambao inaposomwa Aayah na inapotajwa rahmah ya Allaah, wanamuomba Allaah rahma Zake na wanaposoma Aayah inayotaja adhabu, wanajikinga kwa Allaah na adhabu Zake". [Al-Qurtwubiy 2:95]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndivyo alivyokuwa akifanya pindi alipokuwa akisoma Qur-aan.

 

 

Mshairi mmoja amesema kuhusu Qur-aan.

 

الله أكبر إن دين محمد         وكتابه أقوى وأقوم قيلا

 

Allaahu Akbar (Allaah Mkubwa), hakika Dini ya Muhammad na Kitabu Chake ni vitu viwili vyenye nguvu na maneno yake yanatua zaidi.

 

لا تتذكر الكتب السوالف عنده   طلع الصباح فأطفئوا القندنيلا

Havitajiki tena vitabu vilivyopita, (kwani kuja kwa Qur-aan)

kumechomoza Asubuhi basi zimeni taa.

 

(Kwani Qur-aan ndio mwangaza hamuhitaji tena mwanga mwingine)

 

Nasi tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   tujaalie kuandamana na Qur-aan ambayo ni uongofu wetu na mwangaza utakaotutoa katika kiza na kutuingiza katika Nuru,  na ndio itakayokuwa sababu ya kufuzu kwetu Duniani na Aakhirah.   Aamiyn.

 

 

Share