Nimetuhumiwa Kuwa Mwizi Kwa Sababu Ya Kupokea Posho Kwa Kumpa Mtu Fursa Ya Kumuuzia Chakula Chake

SWALI:

 

Asalam aleykum,

Nilikuwa treasurer wa waislamu, ila kabla ya hapo nilikuwa naendesha program binafsi ya kuwauzia chakula baadhi ya wanajumuiya hao. Nilipopata uongozi huo niliendelea na biashara hii kwani ilinisaidia. Ilinilazimu kumbadili mpishi ili kuboresha huduma.

Ilipofika Ramadhani mpishi wa mwanzo alinifuata ili nimpatie tender futari kama ilivyokuwa hapo nyuma ila nikamuambia nina mpishi mwingine, tuliongea na tukakubalina, atanipa kiasi fulani kwa kila sahani kama kwenye ile program binafsi. Futari ilianza kuletwa na mambo yalienda kama tulivyopanga. Baada ya wiki mbili yule mama alivunja utaratibu wetu, nikamuambia kama ni hivyo asilete tena futari. Mama alikataa na kuanza kuwa mkali kiasi kwamba hali hiyo iliwafikia viongozi wengine. Tuliitisha kikao na uongozi ulinishutumu mimi kama MWIZI. Jee madai hayo ni sahihi?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu posho mliyokubaliana na aliyekuwa mfanyi kazi wako.

Gogoro kama hilo huwa linatokea sana katika taasisi zetu na hasa kunapoletwa lalamishi kwa viongozi au kiongozi. Mara nyingi ufumbuzi huwa haupatikani kwa sababu wenye kuhukumu au kusikiliza malalamishi huwa hawasikilizi pande zote mbili kwa makini na kutaka suluhu.

 

Biashara Kiislamu ni maelewano baina pande mbili husika na baada kuelewana inabidi kila upande uwe ni wenye kutimiza mapatano hayo kwa kiasi cha juu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Waislamu wapo juu ya masharti (waliosikilizana)". Hivyo, ni wajibu kila upande utimize maagano maadamu hakuna haramu kati ya hayo maafikiano. Lakini mara nyingi huwa haiwi hivyo kwa kutojua uzito wa ahadi waliyoekeana baina yao.

Katika mapatano hayo hakuna haramu yoyote kwani wewe umempatia fursa ya kuuza chakula chake katika sehemu yako. Ikiwa mama huyo hakutaka kuingia katika mapatano hayo anagekuambia kuanzia mwanzo ili kusiwe na mivutano kama hiyo naye angetafuta mahali pengine. Hapo hakuna wizi wa aina yoyote ile.

Hata hivyo, yaonyesha kuwa nawe una makosa kwa upande mwengine, kama ulivyosema ulikuwa na mpishi mwengine lakini ukampa huyo mama hiyo nafasi kwa sababu alikuahidi kukupa posho ya pembeni kwa kila sahani na ndio ukavutika na kumtoa mpishi wa mwanzo. Kwa hali hiyo, hapo kunaweza kuingia utata na kunaweza pia kuingia masuala ya rushwa vilevile. Na kama ni hivyo basi, utaingia kwenye madhambi ya kupokea rushwa ambayo tayari Mtume wetu kataja kulaaniwa na Allaah kwa yule mwenye kutoa na kupokea rushwa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share