Mume Inampasa Amhudumie Mke Katika Eda? Mume Anayo Haki Ya Kudai Mahari Ikiwa Mke Anataka Kuachika?

SWALI:

Salaam alaykum kaka zangu na dada zangu.Mungu awabariki na akulipeni mema duniani na akhera. Masuali yangu ni kuhusu ndoa kwasababu ni mambo yanayoleta mtafaruku kila siku katika jamii yetu.Najaribu kuangalia katika majibu lakini sioni. Suali langu la kwanza- Mwanamke amedai kuachwa (talaka) na wazee wa mwanamke wamechangia. Mke anataka lazima akafanye kazi ingawa mume anamuhudumia ipasavyo. Mume amekubali kutoa talaka bila kutaka kuepusha balaa zaidi. Jee Mume huyu ni lazima aendelee kumuhudumia mke mpaka eda yake iishe. Jee Mume anayo haki kudai mahr? Jee kama mke atajilazimisha kwenda kufanya kazi, mume aendelee kumuhudumia?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Asli talaka ni katika jambo lisilopendeza katika Uislamu.

Mwanamke amedai kuachwa (talaka) juu ya kuwa Uislamu umetoa haki ya kutolewa na kukubaliwa kwa talaka ila aliyepewa haki ya kuitoa ni mume na sio mke. Mke amepewa haki nyengine inaitwa khulu’ (kujivua na ndoa au kujikombowa) kama itavyokuja elezwa mbele insha Allaah, na haitokuwa vyema kushawishiwa mume au kushinikizwa na kuchagizwa na mtu yeyote au kuitoa kwa kujiepusha na matatizo zaidi. Umesema kuwa mume amekubali kutoa talaka kutaka kuepusha balaa, lakini haipendezi japo kalazimishwa na wazazi wa mwanamke kumuacha mkewe, mke na mwanamke hana haki ya kuiomba talaka au kumchagiza mumewe amuache kama anaamini Allaah na Siku ya Mwisho na ni mwenye kumpenda al Habiybi Musttafa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani akifanya hivyo bila ya kuwepo sababu yo yote huwa mke huyo haramu kwake kunusa harufu ya Pepo wachilia mbali kuingia katika Pepo yenyewe kama ilivyothibti katika Hadiyth ya Thawbaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Mwanamke yoyote atakayeomba talaka kwa mume wake bila ya sababu yoyote (inayokubalika bila ya ovu lolote) ni haramu kwake kupata (kunusa) harufu ya Pepo” Al-Haakim.

Na ikitokea kuwa patahitajika kupatanishwa basi upatanishi ni katika mambo yenye fadhila kubwa kwa mwenye kuweza kuwapatanisha wahusika wawili hata kama kuwapatanisha kwenyewe kutapelekea kutumia uongo, kwani katika kuwapatanisha watu uwongo unaruhusiwa kwa mtapatanishaji.

Qur-aan imethibitisha kuwa mazungumzo na mashauriano yoyote hayana kheri isipokuwa ya namna hizi:

Kuamrisha jambo la sadaka ya kuwapa watu

Kufanya jambo lolote jema

Kupanga mipango ya kusuluhisha baina ya watu (wakiwemo mke na mume) kama ilivyosema Qur-aan:

“Hakuna kheri katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Allaah, basi tutakuja mpa ujira mkubwa.”  An-Nisaa: 114.

Ikiwa wazee wa mwanamke wamechangia pindi pakitokea mtafaruku na kukhitalifiana baina ya mke na mume, na pakakhofiwa kutokea kufarikiana kutakopelekea kutolewa talaka, Qur-aan imeshauri kuwa pachaguliwe watu wawili na bila shaka wawe ni wenye hekima na wenye kupendelea kupatikana kwa kila lenye kheri sio wawe wenye kuchangia na kushadidia kutolewa kwa talaka na kupalilia moto, na hao wapatanishi wanatakiwa mmoja atoke upande wa mume na mwengine upande wa mke; na kama wana nia ya kupatana basi Allaah Atawawafikisha, kwani yawezekana kuendelea kukaa pamoja au kuachana yote yaweza kuwa ni kheri, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari.” An-Nisaa: 35.

Hivyo basi talaka huenda ikawa kheri lakini ni katika jambo lililowekwa kuwa liwe la mwisho kufikiriwa na kuchaguliwa au kupendekezewa wahusika tena bila ya ushawishi wa wazazi au wa mtu yeyote yule; kwani kusababisha kutolewa talaka kwa kumchukiza mke kwa mumewe kwa namna yoyote ile ikiwemo kumtajia mke maovu ya mumewe ili amchukia au kumtajia mke wa mtu uzuri wa mwanamme asiyekuwa mumewe ni katika maovu yaliyokatazwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi mwenye kumchukiza mwanamke kwa mume wake (kumtajia mke wa mtu mazuri ya mwanamume asiyekuwa mumewe au kumtajia mke maovu/machafu ya mumewe) au kumchukiza mtumwa kwa bwana wake” Abu Daawuud.

Sasa ikifikia kuwa hakuna njia ya wawili hawa kuweza kukaa pamoja basi kitu cha mwisho ndio talaka itayotolewa na mume na Mume huyu ni lazima aendelee kumuhudumia mke mpaka eda yake iishe kwani huyo aliyeachwa huwa bado ni mke wa huyo mume isipokuwa hakuna haki ya kindoa baina yao na atakapotaka kumrejea (ikiwa talaka rejea; yaani ya kwanza au ya pili) huwa ana haki hiyo bila ya mke au wazazi wa mke kumkatalia.

Je Mume anayo haki kudai mahar? Mahari ni kiwango maalumu cha mali kinachobainishwa na kutolewa na mwanamume kwa makubaliano kuwa ni sadaka ya mwanamke katika ndoa, hii ina maana kuwa kuyadai mahari ni kuidai sadaka yako uliyoitoa na katika Uislamu si katika wema wala si muruwa wala si katika yenye kushajiishwa na Uislamu na wala si katika desturi nzuri ambazo anatarajiwa ajipambe nazo Muislamu kudai sadaka yake aliyoitoa iwe kwa sababu yoyote ile na kumpa mtu (hasa mahari) na baada ya muda kwa kuwa tu uhusianao wenu umetokewa na cha kutokewa ukafikia kuvunjika ukataka yule mtu akurudishie kitu ulichompa hasa baada ya kufaidika na mtu huyo, na hapo tayari umefaidika na mwili wa mwanamke, na kutakiwa kumpa mwanamke sadaka haina maana kuwa ulimpa au ulitoa amana au akiba ‘deposit’ na kukodishwa mwili wake, hivyo siku mkataba ukisha urudishiwe dhamana uliyoitoa ambayo ni uzuri wake huduma zake na kadhalika. 

Uislamu umeweka wazi kuwa si halali kwa mume kuchukua chochote kile katika alichompa mkewe kwa kuwa sasa uhusianao wao haupo tena kama Alivyoeleza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kusema:

“Talaka (ya kuweza kumrejea mke) ni mara mbili, basi ni kushika kwa vizuri au kuwacha kwa wema, na sio halali kwenu kuchukua katika muliyowapa wao chochote kile, isipokuwa ikiwa watakhofia (mume na mke) kuwa hawatasimamisha mipaka ya Allaah, na ikiwa mutakhofia ya kuwa wao hawatasimamisha mipaka ya Allaah basi hakuna tatizo juu yao (mume na mke) katika atakayojifidia (mke) kwayo, hiyo ni mipaka ya Allaah, na mwenye kuichupa mipaka ya Allaah basi hao ndio Madhalimu﴿Al-Baqarah: 229.

 

Aayah imeelekeza wakati ambao mwanamume ataruhusiwa kuchukuwa mahari aliyoyatoa kwa kusema kuwa:

 

“…isipokuwa ikiwa watakhofia (mume na mke) kuwa hawatasimamisha mipaka ya Allaah, na ikiwa mutakhofia ya kuwa wao hawatasimamisha mipaka ya Allaah basi hakuna tatizo juu yao (mume na mke) katika atakayojifidia (mke) kwayo …” Al-Baqarah: 229.

 

Haya ni katika yanayoeleweka na Mafukahaa kuwa ni khulu’ jambo ambalo hutokea ikiwa haiwezekani tena maisha baina ya mume na mke kwa sababu yoyote ile ya kilazima, ndio Allaah kwa rehma Zake akampa mke haki hii kama alivyompa mume haki ya talaka na wote wawili mke na mume hawatakiwi kuzitumia haki walizopowa kinyume cha sharia, mke amepewa haki ya khulu’ kwa maana kuwa anayo haki ya kujivua na ndoa ile (jambo linalohitaji sana katika jamii ni kuelewa kuwa mwanamke anayo haki ya kujivua na ndoa kama yatatokea ya kumpelekea kufanya hivyo) yakiwepo ya kumpelekea mke kufikia kuchagua khulu’ basi mke atajifidia na mume hana haki kumdai mahari/ fidia kwa kiwango kisichozidi mahari yake aliyoolewa kwayo ili ajivue na ndoa iliyomshinda kwa mume huyo kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya ya Ibn Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposimulia kuwa:

 

“Alikuja mke wa Thaabit bin Qays bin Shaamis kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kulalamika kuwa yeye anamchukia sana mumewe kwa kusema: ‘Ewe Mtume wa Allaah mume wangu Thaabit bin Qays simlaumu katika tabia wala dini lakini nachukia (riwaya nyingine inasema, nachelea) ukafiri katika Uislamu. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Je, utarudisha kwake kile ulichokichukua (katika riwaya hadiyqah/ shamba) kwake na akuachie njia yako? Akasema: "Ndio". Basi Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia Ewe Thaabit kubali shamba na umuache muacho.” Al- Bukhaariy.

 

Faida:

 

Kama ilivvyothibiti katika Hadiyth kuwa khulu’ haikuja kwa sababu ya tabia mbaya za mume au dini, wala haikuja kwa sababu ya maudhi ya mume wala vitimbi, hivyo basi mume akifanya ayafanyayo kwa makusudi kumchukiza mkewe (sio mke kumchukia mume bali hapa huwa anachukizwa) ili tu mke ajifidie huwa hapo si pahala pa khulu’, bali asli ya khulu’ ni mke kumchukia mume na sio vyenginevyo.

 

Baadhi ya Maulamaa wanasema kuwa ikiwa mwanamke atafanya khulu’ basi mume hana haki ya kumrejea huyo mwanamke, na huyo mwanamke atakaa eda, kwa wenye kuhesabu kuwa khulu’ ni talaka basi hukumu zake ni hukumu za talaka kwani wengine wanasema sio talaka bali ni mtengano (fas-kh).

 

Kufanya kazi kwa mwanamke ni katika mambo yaliyoleta mgawanyiko baina ya Maulamaa; Maulamaa wametofautisha na kuweka wazi kuhusiana na kazi ya mwanamke; wamesema kuwa ikiwa kazi yenyewe itapelekea kusababisha kutotimiza haki za mumewe basi kazi hiyo haitofaa kufanywa na mke huyo na hasa ikiwa hakuna sababu ya lazima kwa mwanamke huyo kufanya kazi; kama iko sababu yenye kukubalika (sio tu kwa sababu mume hampi pesa au kipato chao ni kidogo au anataka kwenda holiday) au kuna ulazima basi atakubalika kwa vidhibiti na masharti maalum kama ilivyoashiria Qur-aan kwa kusema kuwa sababu iliyowapelekea kwenda kufanya kazi ya kunywesheleza wanyama hali ya kuwa wao ni wanawake ni kwa kuwa baba yao alikuwa hawezi tena kazi hiyo kwa uzee wake hivvyo walilazimika kuifanya kazi kwa kuhitajika kuwepo mnyeweshezaji wa wanyama wao,

“…Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi –hawa walikuwa wanawake- mpaka wamalize hao wachunga -wanaume- Na baba yetu ni mzee sana Al-Qaswas: 23.

Mke anataka lazima akafanye kazi iwe moja kati ya kazi ambazo kimaumbile ni katika kazi anazotarajiwa na kutegemewa kuzifanya mwanamke ni kama vile Waislamu wanahitaji Madaktari wa kike wauguzi wa kike, walimu wa kike na katika kila sehemu ambazo pakiwepo mwanamke kama ndie mhudumu mkuu huwa ni bora na italazimu kwa mwanamke au wanawake wa Kiislamu kufanya kazi katika sehemu hizo ili kuwahudumia wanawake wenzao wa Kiislamu, na hata kama mume anamuhudumia ipasavyo huwa hapa anayo haki ya kufanya kazi hiyo na huenda ikawa ni faradhi kama hakuna wengine wa kuifanya. Juu ya hivyo haki za mume hazitosameheka na juu ya kufanya kazi kwake mume bado ni jukumu lake kumhudumia mkewe hata kama kipato cha mke kwa kufanya kazi ni kikubwa kuliko cha mume; mume huwa hana haki ya kuchukua kipato cha mke kwa kisingizio kuwa kilichompelekea amemruhusu kufanya kazi ni apate kuchangia huduma za nyumba; hivyo yeye atalipa kodi ya nyumba na mke atalipa umeme, maji, simu na kadhalika.

Juu ya kuwepo ruhusa ya kufanya kazi kwa mwanamke hata hivyo panahitajika ieleweke kuwa sehemu ya kufanyia kazi isiwe sehemu ya mchanganyiko baina ya wanawake na wanaume kadiri ya uwezekano kama ilivyoashiria Qur-aan kwa kusema:

“Na alipoyafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu (wanaume) wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga (wanaume) Na baba yetu ni mzee sana” Al-Qaswas: 23.

Kinachokatazwa kwa mwanamke huyo ikiwa atafanya kazi zinazoruhusika ni kuzungumza na wanaume tu bila ya kuwepo haja au ulazima wowote wa kuzungumza nao; kwani anatakiwa awe anajiheshimu, anajilinda, anaamrisha mema na kukataza mabaya hapo kazini na kujitanda bali kuvaa vazi linalokubalika katika Uislamu ambalo ni Hijaab itayofunika kichwa chake kamili na shingo yake mpaka kushuka kufunika kifua chake na nguo zenye kufunika mwili wake zisizoonyesha umbo lake na kadhalika wala havai nguo zenye kuonyesha kuwa anafanana na wanaume kama kuvaa suruali na nguo zinazoeleweka kuwa ni za kuime.

Kumhudumia mke ni jukumu la mume iwe mke anafanya kazi au hafanyi anafanya kwa ridhaa ya mumewe au bila ya ridhaa ya mumewe bado litabakia jukumu pale pale hata kama mke atajilazimisha kwenda kufanya kazi, mume atatakiwa bado aendelee kumuhudumia, na kwa kulazimisha mke kufanya kazi au mke kufanya lolote lile ambalo mume halitaki lifanywe na mkewe ikiwemo kumuingiza ndani ya nyumba yao hata kama nyumba ni ya mke hukumu ni ile ile mtu asiyetakiwa na mumewe aingizwe bila ya ruhusa au ridhaa ya mume mke huyo huwa anakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu kwani mke katika mafundisho aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa anatakiwa amtii mumewe na kufanya hivyo ni kujitengenezea Pepo yake kinyume cha hivyo kijikosesha radhi za Mola wake kama ilivyothibiti katika Hadiyth nyingi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share