Nguo Ikiingia Pombe Ni Najisi? Akishika Pombe Kwa Bahati Mbaya Wudhuu Unatenguka?

SWALI:

 

Napenda kuuliza tena kuhusu suali la tohara. Ikiwa nguo ya Muislamu imemwagikiwa na Pombe. Inatoharika vipi au yaweza kusalia nayo? Na kama mkono wa Muislamu umeshika pombe japo kwa bahati mbaya. Kunawa na kuendelea kuswali kunafaa? Na kama mtu anao udhu na akagusa pombe. Jee udhu umetenguka?

 

Ahsanteni sana Mwenye ez Mungu akuzidishieni kila la kheri amin.


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu utwahara au unajisi wa pombe. Hakika ipo tofauti baina ya wanazuoni kuhusu utwhara au unajisi wa pombe. Wapo wanaosema kuwa ni najisi na wapo wenye kusema kuwa ni twahara. Hata kwa wale wenye kusema kuwa ni najisi, unajisi wake haufikii ule wa mbwa. Hivyo, ikiwa itakuwa pombe imeingia kwenye nguo utapatia maji pale penye pombe na kisha utaswalia nguo hiyo hiyo. Ama ikiwa umeshika pombe kwa bahati mbaya au kwa kusudi utauosha mkono wako na huna haja ya kutawadha tena. Kwa hiyo, unaweza kuswali Swalah bila ya shida au tatizo.

 

Wudhuu hautenguki kwa kushika pombe, japokuwa si vyema kabisa kukishika kinywaji hicho cha haraam. Wanachuoni wengine wanaonelea kuwa pombe si najisi na hivyo hata ikikuingia kwenye nguo basi mtu anaweza kuswali nayo ingawa haipendezi kuswali na harufu hiyo huku umesimama mbele ya unayemuomba (Allaah), kama ambavyo vilevile haipendezi kusimama ukiwa na nguo yenye uchafu wa aina nyingine yoyote kama matope, vumbi, girisi na oili za gari kwa wale watengenezaji magari ambao wanakimbilia kuswali na nguo zao chafu, au wauza samaki na nguo zao zinukazo shombo n.k. Ingawa kulinganisha na hizo, uchafu wa pombe na harufu yake ni mbaya zaidi na inayokirihi na pia kutatiza wenzako wanaoweza kukushuku kuwa umeinywa kutokana na harufu hiyo. Hivyo pamoja na kuwa si najisi kwa kauli yenye nguvu, lakini ni bora usimame mbele ya Allaah kwenye Swalah ukiwa nadhifu, msafi na mwenye kunukia harufu nzuri.

Kwa faida zaidi soma maudhui ya unajisi au utwahara wa pombe kwa kirefu hapa:

005 Je, Pombe Ni Katika Vitu Najisi?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share