Kuna Miezi Maalum Ya Kuoa Na Kuolewa?

SWALI:

 

Assalaamu ‘alaykum. Mm nina swala langu ni hivi Nataka harusi (kuowa) yangu ifanyeke June lkn kuna watu wananiyambia mtu haowe June je ni kweli au ni itikati za watu, na kuna miezi maalum ya kuowa au kuleowa naomba msaada wako. Natumai swala langu kwa mara ya tatu sasa lkn naona apate jibu naomba msada wenu.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wakati maalumu wa kufunga ndoa. Hakika ni kuwa katika Dini yetu hakuna wakati maalumu wa kufunga ndoa. Unaweza kufunga wakati na mwezi wowote ambao umeafikiana na mkeo mtarajiwa au ambao ni muafaka familia mbili hizo. Ama kuwa katika baadhi ya jamii zetu hufanya ushirikina kwa kwenda kwa wachawi na wapigaji ramli ili wawaeleze wakati na tarehe ya kuoa. Kufanya hivyo ni dhambi kubwa sana katika Uislamu. Hakika ni kuwa Allaah Anatueleza kuwa shirki ni dhambi ambayo haisamehewi na Allaah kabisa (Suratun-Nisaa (4): Aayah ya 48 na 116). Na amali ya mwenye kumshirikisha Allaah yote hupomoka na akaruka patupu.

 

Ni nasaha yetu kuwa wewe usifuate ada na desturi zinazokwenda kinyume na Uislamu bali kuwa imara katika Uislamu wako na Allaah Aliyetukuka Atakupatia tawfiki.

 

Tukitizama historia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utakuta kuwa alioa katika tarehe na miezi tofauti. Hebu tazama mifano ifuatayo ya ndoa zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

1.      Sawdah bint Zam‘ah, ‘Aaishah bint Abu Bakr, Hafswah bint ‘Umar, Umm Salamah Hind bint Abi Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anhum) aliwaoa Shawwaal (Mfungo Mosi).

 

2.      Juwayriyyah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha) – Sha‘abaan.

 

3.      Umm Habiybah Ramlah bint Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anha) – Muharram (Mfungo Nne).

 

4.      Maymunah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha) – Dhul-Qa‘dah (Mfungo Pili).

 

Hii ni ishara ya wazi kuwa ndoa inaweza kufungwa wakati wowote kwa mujibu wa ndoa za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Ikiwa utaoa kwa miezi ya Kirumi/ Kilatini kama ni Juni au mwezi wowote ule hakuna kipingamizi wala tatizo lolote lile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share