Ramadhwaan: Zakaah Lazima Itolewe Ramadhaan?

SWALI:

Assalaam alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Shaikh naomba unipe jibu la Suali langu.

1.     Ikiwa nataka kutoa Zakaah ya mali kabla ya kufika   

       mwezi wa Ramadhani itafaa? Au itahesabiwa ni Sadaqa?

2.     Hii Zakah ya mali ni lazima itolewe mwezi wa Ramadhani

       tu? Na ikipita au ikiwa kabla ya Ramadhani itahesabiwa  

        kua ni Sadaqa?

Basi Shaikh ntashukuru kama utanipatia jibu Inshallah.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunamshukuru Allah Aliyetupatia neema nyingi ambazo hatuwezi kuzihesabu. Na shukrani kwa kaka na dada zetu ambao wanauliza maswali yenye kutufaidisha sote.

1.     Hakika ni kuwa Zakah ya mali inaweza kutolewa wakati wowote na si lazima itolewe wakati wa Ramadhan. Kila ‘Ibadah ina masharti yake na sharti la kutoa Zakah ni kuwa ni lazima mwanamme au mwanamke awe amefikisha nisaab (kiwango cha chini cha mali nayo ni takriban thamani ya gramu 82.5 ya dhahabu) katika mali yake ya akiba. Na hela hii ikae bila ya kupungua kwa hawli nzima (yaani mwaka) kufuata kalenda ya Kiislamu. Sasa hela kama hiyo ikipitiwa na mwaka itabidi mtu huyo aitolee Zakah nayo ni kutoa asilimia 2.5 (2 ½ %) na hela hiyo inatakiwa ipatiwe watu wanane waliotajwa katika aya ifuatayo:

{{Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima}} (9: 60).

 

2. Tofauti ya Zakah na Sadaqah ni kuwa Zakah inatolewa kufuata masharti ambayo tumeyataja katika jibu la swali la kwanza na Sadaqah inatolewa wakati wowote na hata kama hujafikisha kiwango cha nisaab. Watu wengi huanza kalenda yao ya kuhesabu kuanzia mwezi wa Ramadhan na hivyo Zakah zao wanatoa kila mwezi huo Mtukufu ili wapate thawabu na ujira mkubwa zaidi. Lakini inatakiwa ikiwa nisaab yako imeanza mwezi wa Swafar kwa mfano hivyo ikifika mwezi kama huo mwaka unaofuata inatakiwa utoe Zakah.

 

Kwa manufaa zaidi tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Zakaah

Zakaah Na Viwango Vyake

Kutoa Zakaah

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

Share