011-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mkutano Wenye Mafanikio Ndio Dawa Yenye Kuokoa

 

MKUTANO WENYE MAFANIKIO NDIO DAWA YENYE KUOKOA

 

Katika jambo muhimu sana katika mahusiano ya ndoa na yenye nafasi kubwa kayafanya yawepo na kudumu ni makutano ya kijinsi kati ya wanandoa wawili. Kwa hakika hii ndio dawa ya matatizo yanayozikuta maisha ya ndoa, matatizo mengi katika jumla ya matatizo ya ndoa ni kufeli katika mkutano huu wa ndoa au kuchelewa kwake kutokana na upande mmoja kutohisi chochote.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza kutumia dawa hiii, kujamiiana na kuingiliana. Mwenyezi Mungu Amelifanya jambo hili lipendwe na watu na Anawalipa watu thawabu kwa kulifanya na ni sadaka na ujira wa ayafanyaye (kwa wanandoa)’[1]. Hapa ndipo panapopatikana ukamilifu wa ladha na kumfanyia hisani mpenzi wako na kulipwa ujira kwa ajili ya hilo, thawabu na sadaka na furaha ya nafsi naye kuweza kuondokana na fikra potofu, hii ni ladha isiyolingana na ladha nyingine yoyote na haswa inapopatikana ukamilifu wake, kila sehemu katika mwili inapopata sehemu ya ladha, basi ndipo ukamilifu wa shughuli hiyo inapofikiwa. Macho yanapomwangalia mke, masikio katika kusikia maneno yake, pua kunusa harufu nzuri na mdomo kubusu na mkono kushika, kila kiungo kinashiriki katika kupata ladha katika ladha kuu inayopata kiwiliwili chake na hii ndio sababu ya mwanamke kuitwa sakan yaani utulivu yaani inatuliza nafsi,

 

“Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu (sakan) kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. ” (30:21)[2]

 

“Kwa hakika maingiliano baina  ya mume na mazungumzo ya faragha baina yao yakifanyika kwa njia sahihi na nzuri humuongezea mwanamme na mwanamke ukaribu wa kimapenzi na huruma ya kiroho baina yao, huwasaidia na hupumzisha miili yao na huwasahaulisha humumi na matatizo ya kidunia hata ikiwa jambo lenyewe ni la muda mfupi tu. Kadhalika huwapa usingizi mzuri, utulivu, ambao hupatikana kupitia maingiliano haya. Wewe kama mwanandoa una mchango wako katika kufanikisha ukamilishaji na kufikia upeo wa juu katika mafanikio haya, muwafaka wa pamoja kati ya mume na mke ni muhimu katika maingiliano haya muhimu, ni juu yako kama mke kujitahidi kwa kadiri ya hali ya juu kufanikisha jambo hili muhimu, ambalo hupatikana kwa njia ya kuwa wawazi na ushirikiano wa pamoja na mume wako”[3]

 

Uislamu umempa nafasi mwanamme haki ya kuomba unyumba kwa mke wake na ukamhimiza mwanamke kukubali kwa haraka maombi ya mume wake na ukamhadharisha na adhabu mbaya kwa mwenye kukhalifu.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Mwanamme atakapomtaka mkewe kwa haja yake basi na ampatie na kumfuata hata akiwa jikoni au kwenye tanuri la mkate”[4]

 

Katika Hadiyth nyingine amesema,

“Naapa kwa yule ambaye Nafsi yangu iko mikononi mwake, hakuna mwanamme yeyote atakayemuita mke wake katika kitanda chake na mwanamke yule akakataa, na mwanamme akalala huku akiwa amekasirika basi Malaika watamlaani mwanamke yule hadi kupambazuke”[5]

 

Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemkataza mwanamke kufunga Swawm ya Sunnah bila idhini ya mume wake kwa Hadiyth yake,

“Haiwi Halali kwa mwanamke kufunga sunna na mumewe yupo, isipokuwa kwa idhini yake, wala hatoki nyumbani kwake isipokuwa kwa idhini ya mume wake”[6]

 

Ni vizuri kwa mwanamke kujua kuwa haja ya mume ya kujamiiana nae inaweza kupita haja yake mwanamke kwa mumewe, kwa kuwa vishawishi kwa mwanamme ni vingi sana, mara nyingi fitna hutokea anaponyimwa mume unyumba, bila ya kuwepo kwa udhuru wa kishari’ah na hivyo kusababisha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwake.

 

Mume asiwe ni mfujaji wa tendo la ndoa bali jambo zuri ambalo dini hii imelingania ni hali ya wastani kwa kila jambo. Kujichosha sana na kuzidisha sana katika kujamiiana ni jambo ambalo halimsaidii mume katika kuwa na siha nzuri. Wanandoa wafahamu ya kuwa jambo ambalo linafanikisha mkutano huu kukua ni kuwepo kwa hamu ya jambo hilo kwa wote wawili, na utangulizi mzuri unatakiwa utoke kwa mume kabla ya jambo lenyewe kuanza, kadhalika kuwekeana wazi na kila mmoja ajue jinsi ya kumuweka sawa mwenzake hadi wafikie kilele cha jambo lenyewe. Katika maingiliano haya ya faragha kati ya mume na mke wasisahau Niyah, na Niyah yenyewe ni, kuwa kila mmoja kumfurahisha mwenzake na kutekeleza haki zake kwake, na yote hayo huwa ni ujira wa sadaka aliyoitaja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake tuliyoitaja hapo nyuma.

 

 

[1] Hii inaashiria ile Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema, “…na mtu kumuingilia mke wake kuna sadaka. Maswahaba wakamuuliza, iweje ewe Mtume wa Allaah, ‘Mtu anastarehe na haja zake na anapata thawabu kwa hilo?’ Mtume akawajibu, ‘Je mnaonaje kama mtu Yule angelifanya kwa haramu je kungekuwa na ubaya?’ Maswahaba wakajibu, ‘Ndio.’ Mtume akasema, ‘vivyo hivyo atakapoweka katika halali atakuwa na ujira’” (Muslim na wengineo)

[2] Angalia kitabu, ‘Rawdhatul Muhibiyn’ cha Ibn Al-Qayyim

[3]Imechukuliwa kutoka katika kitabu, ‘Tuhfatul ‘Aruus’ cha Al-Istanbuliy

[4] Imepokewa na Ahmad

[5] Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim

[6] Al-Bukhaariy na Muslim

Share