017-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kukatazwa Kutoroka Katika Nyumba Ya Mume

 

KUKATAZWA KUTOROKA KATIKA NYUMBA YA MUME

 

Huenda mume akatofautiana na mke (jambo hili ni la kawaida na hutokea mara kwa mara) lakini huenda tatizo hili wakati mwingine likawa kubwa kidogo na hivyo mke kughadhibika na kupandwa na Shaytwaan katika akili yake, jambo la kwanza siku zote analofikiria ni kukusanya nguo zake na kurudi kwao.

Kwa hakika hili ni kosa analofanya mke na mara nyingi wanakuwa ni wale walioolewa hivi karibuni, kwa kufanya hivyo mwanamke yule anakuwa amefanya makosa manne na sio moja tu:

1.     Kosa la Kishari’ah: nalo ni lile la kutoka nje ya nyumba bila ya ruhusa ya mume (hakuna sababu yoyote ya kujitetea, eti ‘ulikuwa na ghadhabu’);

2.     Kuweka mazingira yasiyokuwa mazuri katika nyumba anayokwenda, yaani nyumba ya wazazi wake;

3.     Kuenea kwa habari na watu wengine wa nje kujua siri za familia;

4.     Kulifanya tatizo dogo lililotokea kuwa kubwa na kuongeza ugumu katika maisha ya ndoa.

 

Kwa hakika suala la kuhama nyumba yako wewe dada yangu wa Kiislamu si suluhisho la tatizo lililopo, huku ni kuongeza tatizo. Hata hivyo jitahidi kusuluhisha matatizo yako na mume wako vizuri kwa utulivu na muombe Mola wako msamaha. Ikiwa mume wako ameghadhibika muache na mambo yake hadi atakapotulia, kisha mkurubie, na hata ikiwa mkosa ni mume wako katika kutekeleza majukumu yake kwako basi amini ya kuwa utakapomtendea mema na kuwa na subira juu yake basi atakusamehe pindi utakapokuwa mkweli kwa matendo yako yote.

 

Share