Hadiyth Kuhusu Kuomba Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah Ni Swahiyh Au Dhaifu?

 

Hadiyth Kuhusu Kuomba Du’aa Pamoja Baada Ya Swalaah Ni Swahiyh Au Dhaifu?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Assalam alaikum

 

Ipo Hadithi ya mtume swalla Allaahu alayhi wa sallam, ambayo imesimuliwa na Abuu Umama Radhiya Allahu anhu amabyo ni hii hapa. Asema Mtume Swalla Allahu alayhi wasallama" halikusanyiki kundi la watu; wakaomba dua miongoni mwao na wengine wakaitikia aamiin; ila Allah atawajibu.”  Amepokea Twabrani, Baihaqiy, Hakim kutoka kwa Habibi Ibn Salamatal Fihryyah; Allaah Awe radhi nao wote hao.

 

Hii ndio Hadithi ninayotaka kujuwa usahihi wake na kama ni Sahihi ukiunganisha na ya Abuu Umama itakuwa ni sahihi kuomba dua kwa pamoja baada ya swala ya fardhi? Kwani imethibiti dua ya pamoja na pia imethibiti dua baada ya swala. Yaani moja ya sehemu inayo kubalika dua ni baada ya swala ya faradh na kama alivyosema imamu Tirmidhy (Allah amrehemu) kuwa ni Hadiythi hasan. Je? Hadiythi hii inafaa kuwa ni hoja madhubuti kwamba kuomba dua baada ya swala ya fardh ni sunnah na imethibiti kwa mtume Swalla Allaahu alayhi wa sallam na ni muhimu sana kwa mtu kuomba dua baada ya swala ya fardhi kwani ni moja ya sehemu inayokubaliwa dua

 

 

Maelezo mengineyo ya muulizaji kuhusiana na swali lake:

 

 

Assalam alaikum,

Hadiythi ya Abuu Umama niloisema yazungumzia dua baada ya swala ni hii hapa kama alivyo inukuu Imamu Shaukani ktk Nailu L’autwar. Pia Hadiythi hii inapatikana ktk Riyadh swallihina Hadithi ya 1,500. Pia nime attach hadithi nilo andika kwa mkono, hii nimeikuta ktk vitabu hivi vya dua vidogovidogo, sijaiona ktk vitabu vya hadithi nimeikopi pamoja na muhtasari wa takhrij yake, sina hakika na usahihi wa Hadithi hii

 

1.     Swali la kwanza, naomba mnifahamishwe usahihi wa Hadithi nilo andika kwa mkono (attachment number one) ama umadhubuti wake kama inafaa kufanyia kazi

 

2.     Maelezo kwa ufupi: Hadithi ya Abuu Umama; Ibn Hajar ktk Fathu lbar juzu ya 11 ukurasa 153 (toleo la mwaka 2003) Kitabu da’awa (dua’u ba’ada swalat)  ameinukuu na akaunganisha na Hadiythi ya Twabari kutoka kwa jaafar isemayo” dua baada ya swala ya fardh ni bora kuliko dua baada ya swala ya sunnat kama ilivyo kuwa ubora wa swala ya fardh kwa swala ya sunnat” pia akanukuu manenoya Watu wa Hanbal kuhusu kauli ya Ibn Lqaiym ktk kitabu chake cha Zadu l’ma’aad (alipo sema hakuna Hadithi Sahihi inayo thibitisha  dua baada ya swala)

 

3.     Swali la pili, Ikiwa Hadithi ya Abuu Umama na maelezo ya Ibn Hajar na Hadith ya Twabari ni sahihi Je kuomba dua baada ya swala ya Fardh ni Sunnat?

 

4.     Swali la tatu, ikiwa Hadithi nilo andika kwa mkono (Swali la kwanza) ni sahihi ama ni madhubuti na inafaa kufanyia kazi, na kwa kuwa baada ya swala kuna kundi la watu, hivyo wakaamuwa miongoni mwao mmoja aombe dua na wengine waitikie wakaifanyia kazi Hadithi (kwani ni sababu ya kujibiwa dua kama hadithi inavyo jieleza) na kwa kuwa kuomba dua baada ya swala ni Sahihi ikiwa Swali la pili  yaani Hadithi ya Abuu Umama  ni madhubuti, Je, kuomba dua kwa pamoja baada ya swala (yaani kufanyia kazi Hadithi nilo andika kwa mkono na ya Abuu Umama kwa pamoja) itakuwa ni sunnat ama bid’a (ukizingatia sunnah inaweza kuwa Mtume Swalla Allaahu alaihi wa sallam amesema (sio lazima afanye), ama amefanya, amekubali jambo moja ktk ya haya matatu yaweza kuwa sunnat)

 

Wabillah taufi

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

In Shaa Allaah tutajaribu kujibu nukta baada ya nukta kuhusu Hadiyth zilizotajwa hapo juu katika swali hilo.

 

 

Mwanzo tunatakiwa tufahamu kuwa du’aa ni jambo ambalo linahitajika kwa Muislamu. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufahamisha kuwa du’aa ni silaha ya Muumini. Kwa hiyo, baada ya kila ‘Ibaadah, Allaah ('Azza wa Jalla) Akatuwekea du’aa. Na ‘Ibaadah ya Swalaah si tofauti, kwani Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema:

 

 فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu. [An-Nisaa: 103]

 

Na Anasema pia Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿١٠﴾

Na inapomalizika Swalaah, tawanyikeni katika ardhi, na tafuteni katika fadhila za Allaah, na mdhukuruni Allaah sana ili mpate kufaulu. [Al-Jumu’ah: 10]

 

 

Hata hivyo, inatakiwa tuilete hiyo du’aa kwa njia ambayo tumefundishwa katika Shariy’ah sio tunavyotaka sisi.

 

Tukianza na Hadiyth ya Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Nadhani itakuwa bora mwanzo tuanze na kuifasiri kwa ukamilifu wake ili ifahamike vizuri.

 

 

Imepokewa kwa Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Aliulizwa Rasuli wa  Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni du’aa gani yenye kusikilizwa zaidi (inayokubaliwa)?” Akasema: “Sehemu ya mwisho ya usiku na baada ya kila Swalaah ya faradhi” [at-Tirmidhiy ambaye amesema ni Hasan].

 

Hivyo ndivyo ilivyonukuliwa na Imaam An-Nawawiy. Labda tuitazame msimamo wa Wanachuoni kuhusu Hadiyth hiyo.

 

 

Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy ameiweka Hadiyth kuwa ni ya (1508), naye amesema Hadiyth hii ni Swahiyh. Hata hivyo, Shaykh Shu‘ayb Al-Arna’ut amesema Hadiyth hii ni dhaifu kwa sababu ya Isnadi yake lakini inatiliwa nguvu na Hadiyth nyingine ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mja anakuwa karibu zaidi katika du’aa zake wakati wa usiku wa mwisho” [at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy, na Isnadi yake ni Swahiyh]

 

Hata hivyo, tukichukulia kuwa Hadiyth hii ni Swahiyh kabisa kama alivyosema Sh. Muhammad Naaswir ad-Diyn al-Albaaniy haimaanishi kuwa adhkaar na du’aa zinazoletwa baada ya Swalaah ni kwa pamoja. Zipo Hadiyth nyingi Swahiyh zinazotufundisha adhkaar na du’aa kwa mpangilo maalumu baada ya Swalaah ya faradhi. Na kufanya hivyo kunampatia mwenye kutekeleza ujira na thawabu nyingi. Kwa hiyo, ni muhimu kuhifadhi du’aa hizo na kuzileta kwa njia inayotakiwa na Shariy’ah. Pia tunatakiwa tulete baada ya Swalaah tu na kabla ya kuinuka latika sehemu aliyoswali Muislamu. Utaratibu wenyewe ni kama ufuatao:

 

 

1-Kusema

 

أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ، وَمِـنْكَ السَّلام، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام

 [Muslim]

 

 

2-Kisha ni kusema:

 

لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُـلْكُ ولهُ الحَمْد، وهوَ على كلّ شَيءٍ قَدير، اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد

 [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

 

3-Baada ya hapo:

 

لا إلهَ إلاّ اللّه وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ الملكُ ولهُ الحَمد، وهوَ على كلّ شيءٍ قدير، لا حَـوْلَ وَلا قـوَّةَ إِلاّ بِاللهِ، لا إلهَ إلاّ اللّـه، وَلا نَعْـبُـدُ إِلاّ إيّـاه، لَهُ النِّعْـمَةُ وَلَهُ الفَضْل وَلَهُ الثَّـناءُ الحَـسَن، لا إلهَ إلاّ اللّهُ مخْلِصـينَ لَـهُ الدِّينَ وَلَوْ كَـرِهَ الكـافِرون

[Muslim].

 

 

 

4-Kisha utaleta mara 33 kila moja ya:

 

 سُـبْحانَ الله 

الحَمْـدُ لله 

واللهُ أكْـبَر

5-Kisha utasoma mara moja

لا إلهَ إلاّ اللّهُ وَحْـدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ الملكُ ولهُ الحَمْد، وهُوَ على كُلّ شَيءٍ قَـدير

 [Muslim]

 

 

 

6-Kusoma Ayaatul Kursiy

 

(2: 255) [An-Nasaa’iy, atw-Twabaraaniy na Ibn Sunniy]

 

 

 

7-Kusoma Suwratul Ikhlasw, al-Falaq na an-Naas ([Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

 

 

Shaykh Swaalih Fawzaan bin ‘Abdillaah al-Fawzaan katika kitabu chake: Al-Mulakhkhaswu al-Fiqhiyy amesema: “Na inapendeza kujihirisha Tahliyl, Tasbiyh, Tahmiyd na Takbiyr baada ya kila Swalaah lakini isiwe kwa sauti ya pamoja. Kila mmoja anasome peke yake. Baada ya kumaliza adhkaar hizi, kila mmoja anaomba kwa siri kile  anachotaka. Hakika ni kuwa du’aa baada ya ‘Ibaadah na hizi adhkaar tukufu inaleta uwezekano mkubwa zaidi wa kujibiwa. Haifai kudhihirisha du’aa bali anaifanya kwa sauti ndogo, kwani kufanya hivyo ni karibu zaidi na ikhlaasw na unyenyekevu na mbali zaidi na riyaa. Ama kwa yale yanayofanywa na baadhi ya watu katika baadhi ya nchi kwa kuleta du’aa ya pamoja baada ya Swalaah kwa sauti kubwa au Imaam aombe na maamuma waitikie “Aamiyn”, hii ni bid‘ah inayochukiza kwani haijapokewa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa anaposwalisha watu na baada ya kumaliza Swalaah akiomba kwa njia hii. Hakufanya hivyo katika Swalaah ya Alfajiri, wala Alasiri, wala Swalaah nyinginezo, wala hakupendeza hilo yeyote miongoni mwa Maimamu” [Mj. 1, uk. 154 – 160].

 

 

Ama tukija katika Fat-hul Baariy nimeipitia Hadiythi hizo ulizozitaja katika Mj. 11, uk. 159, chapa ya Daar as-Salaam, chapa ya tatu ya mwaka 1421 H/2001 M. Imaam al-Bukhaariy ana mlango wa 18: Baab ad-Du’aa’i ba‘da asw-Swalaah (Mlango wa Du’aa baada ya Swalaah). Imaam al-Bukhaariy ameweka Hadiyth mbili zilizoshereheshwa na Ibn Hajar, nazo ni kama zifuatazo:

 

1-Imepokewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika wametangulia wenye mali kwa daraja na neema za kuendelea. Akasema: “Itakuwaje hivyo?” Akasema: Wanaswali kama tunavyoswali, wanapigana Jihaad kama tunavyopigana, na wanatoa katika fadhila za mali zao, nasi hatuna cha kutoa. Akasema: “Je, niwajulishe jambo ambalo mkifanya mtawafikia waliokuwa kabla yenu na kuwashinda wanaokuja baada yenu, wala hatofikia yeyote kwa mlioleta ila atakayeleta mfano wake? Leteni Tasbiyh baada ya kila Swalaah mara kumi, Tahmiyd kumi na Takbiyr kumi”

 

2-Mughiyrah bin Shu‘bah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuandikia Mu‘aawiyah bin Abi Sufyaan (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema baada ya kila Swalaah baada ya salaam:

 

لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُـلْكُ ولهُ الحَمْد، وهوَ على كلّ شَيءٍ قَدير، اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد

 

Kauli yake: “Mlango wa Du’aa baada ya Swalaah”, yaani baada ya Swalaah za faradhi. Hadiyth hizo mbili zilizo hapo juu zinatufahamisha kuwa ipo du’aa baada ya Swalaah, du’aa ambazo ni makhsusi kama alizotufundisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, hizo Hadiyth hazionyeshi kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba na Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wakiitikia ”Aamiyn.”

 

 

Ama tukija katika Hadiyth ulizozitaja kwa mukhtasari ambazo amezitaja Ibn Hajr Al-Asqalaaniy, na pia kuna nyingine umeziacha zote hazina dalili ya kuomba du’aa kwa pamoja baada ya Swalaah. Na hivyo akamuusia Mu‘aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) asiache kuomba du’aa baada ya Swalaah, du’aa maalumu [Abuu Daawuwd, an-Nasaa’iy, al-Haakim na Ibn Hibbaan].

 

 

Pia Hadiyth ya Abuu Bakrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa kauli:

 

  اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ مِنَ الْكُـفر، وَالفَـقْر، وَأَعـوذُبِكَ مِنْ عَذابِ القَـبْر،

 

“Ee Allaah! Najilinda Kwako kutokana na ukafiri, ufakiri na adhabu ya kaburi.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba kwayo baada ya kila Swalah [Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, na imesahihishwa na al-Haakim].

 

Na pia Hadiyth ya Sa‘d, Zayd bin al-Arqam, Swuhayb na Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) zatuonyesha du’aa za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya Swalaah kwa njia ya siri ila kwa wakati mwengine alikuwa akinyanyua sauti ili wafuasi wake wapate kujifunza kwa njia sahali na rahisi.

 

 

Na maelezo yote hayo yanaweza kufupishwa kwa kauli ya Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 

 وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ ﴿٢٠٥﴾

Na mdhukuru Rabb wako katika nafsi yako kwa unyenyekevu na kwa khofu na si kwa jahara katika kauli asubuhi na jioni; na wala usiwe miongoni mwa walioghafilika.  [Al-A’raaf: 205]

 

 

Imaam ash-Shawkaaniy amesema kuieleza Aayah hii katika tafsiri yake Fat-hul Qadiyr kuwa, “Hiyo ni kuisikilizisha nafsi yake bila kutoa sauti, yaani kwa unyenyekevu na kwa khofu na kuzungumza kwa mazungumzo chini ya kujihirisha.”

 

 

Na Ibn Kathiyr naye amesema katika tafsiri yake, Tafsiyr Al-Qur-aanil ‘Adhwiym: “Mtaje Rabb wako kwa matumaini na khofu na kwa kimoyomoyo, si kwa jahara. Na hivi ndivyo Dhikru-Allaah  inavyopendekezwa iwe, si kwa sauti ya juu wala kwa jahara.”

 

Na Aayah hii inafafanuliwa na Hadiyth iliyowazi kabisa kutoka kwa Abuu Muwsaa al-Ash‘ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema:

 

Watu walinyanyua sauti zao katika du’aa wakati wa baadhi ya safari, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ‘Enyi watu! Jifanyieni wepesi katika nafsi zenu, kwani mnayemwomba si kiziwi wala si wa kughibu. Kwa hakika mnayemwomba ni Mwenye kusikia, wa karibu, yu karibu zaidi ya mmoja wenu kuliko shingo ya mnyama wake.” [al-Bukhaariy na Muslim]. 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share