Ufafanuzi Wa Aayah Kuhusu Malaika Haaruwt Na Maaruwt Na Shaytwaan

 

Ufafanuzi Wa Aayah Kuhusu Malaika Haaruwt Na Maaruwt Na Shaytwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Salam alaykum

Kwanza nitangulize dua na pongezi kwa kazi ngumu munayoifanya katika kuendeleza kazi hii ya da'wa. Suali langu lipo kwenye Surat baqara aya ya 102 (02: 102) aya ni refu na sitairudia isipokua nitauliza vipengele viliomo kwenye aya hii.

 

a) Haruta na maruta. Je ni malaika? Manake wametoka nje ya sifa za kimalaika. Kuna mashekhe wengine wanasema hao ni watu walioshiba elimu, kwa uchambuzi wa kilugha ya kiarabu. Na kama ni malaika wakiwasiliana vipi na hao binadamu wakati huo.

 

b) Qur-aani inasema, shetani akawafunza watu uchawi na YALE YALIOTEREMSHWA KWA MALAIKA WAWILI huko Babylon. Sasa ni nini hichi waliokuja nacho au kuteremshiwa haruta na maruta?

 

c) Na hao haruta na maruta hawamfundishi mtu mpaka wampe onyo. Kuwa sie ni mtihani tuu musikufuru. Sasa je ndio tuseme hawa malaika wametumwa kutoka mbinguni kuleta balaa hili la uchawi na kufundisha watu? Wasalam alaykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ni muhimu kabla ya kuingia katika kujibu vipengele vya swali lenyewe tutoe tarjama ya Aayah hiyo kwa ukamilifu wake. Aayah yenyewe ni kama ifuatayo:

 

وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿١٠٢﴾

 Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 102]

 

Ama tukianza na kipengele (a), ni kuwa Malaika hao hawajatoka katika sifa za kimalaika kwani Malaika sifa yao imetajwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliposema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym 6]

 

Kwa hiyo, sifa kuu ya Malaika kufuata maagizo ya Muumba wao. Ama mawasiliano ni kawaida kabisa kwani Qur-aan inatufahamisha katika Suwrah nyingine na Sunnah pia nazo zimejikita katika kutueleza vipi Malaika walikuwa wakiwasiliana na wana Aadam kwa amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); mfano jinsi Jibriyl (‘Alayhis-salaam) alivyowasiliana na Maryam. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Anasema:  

 

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا ﴿١٦﴾فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا ﴿١٧﴾قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا ﴿١٨﴾قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا ﴿١٩﴾قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا ﴿٢٠﴾قَالَ كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ ۖ وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِّلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِّنَّا ۚ وَكَانَ أَمْرًا مَّقْضِيًّا ﴿٢١﴾

Na mtaje katika Kitabu Maryam alipojiondosha kutoka kwa ahli zake, mahali pa Mashariki.Akafanya pazia kujitenga nao, Tukampelekea Ruwh Wetu (Jibriyl عليه السلام) akajimithilisha kwake kama bin Aadam timamu.  (Maryam) Akasema: Najikinga kwa Ar-Rahmaan dhidi yako ukiwa ni mwenye taqwa. (Jibriyl عليه السلام) Akasema: Hakika mimi ni Mjumbe wa Rabb wako ili nikubashirie tunu ya ghulamu aliyetakasika. (Maryam) Akasema: Itakuwaje niwe na ghulamu na hali hakunigusa mtu yeyote, na wala mimi si kahaba? (Jibriyl) Akasema: Ni hivyo hivyo (lakini) Rabb wako Amesema. Haya ni sahali Kwangu! Na ili Tumfanye awe Aayah (muujiza, ishara) kwa watu na rahmah kutoka Kwetu, na likawa jambo lililokwisha hukumiwa. [Maryam: 16-21]

 

Ama katika Hadiyth tunapata ile ya 60 katika Riyaadhw Asw-Swaalihiyn cha Imaam an-Nawawiy kutoka kwa ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye anatufahamisha jinsi gani alikuja wakiwa hawamjui na wala haonekani na athari ya safari. Mgeni huyo alikuja mpaka akawa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuanza kumuuliza maswali kuhusu Uislamu, Iymaan, Ihsaan na alama za Qiyaamah. Alipoondoka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kama anamjua mgeni huyo, naye akajibu kuwa Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi. Naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Huyo ni Jibriyl amekuja kuwafundisha Dini yenu [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy]

 

Hizi ni dalili kuonyesha ni katika sifa ya Malaika kuwasiliana na wanaadamu wanapoamriwa hivyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

 

 

Tukija katika kipengele (b), Aayah inatueleza kuwa,

 

lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. 

 

 

Ibn Kathiyr amesema: “Wengi miongoni mwa Salaf walisema kuwa Haaruwt na Maaruwt walikuwa Malaika ambao walishuka duniani kutoka mbinguni na wakafanya waliyofanya kama Aayah inavyosema. Maoni haya yanalingana na ukweli kuwa Malaika wamehifadhika na makosa. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alisema: ‘Mtu alipowajia Malaika kujifunza uchawi, walimkataza sana na kumwambia, ‘Sisi ni mtihani, tahadharini na kukufuru’. Walikuwa wanajua lipi ni jema na lipi ni uovu na mambo yenye kupelekea kwenye Iymaan na ukafiri na hivyo walijua kuwa uchawi ni aina ya ukafiri. Wakati mtu alipokuja kujifunza uchawi, walisisitiza kujifunza, walimuamuru kwenda sehemu fulani, na alipokwenda Shaytwaan alimpokea na kumfundisha uchawi. Baada ya mtu huyu kujifunza uchawi, nuru (imani) itamkimbia, na ataiona inameremeta (na inapaa) kwenda angani. Kisha atatangaza, ‘Oh huzuni! Ole wangu! Nitafanyaje?”

 

 

Hasan al-Baswriy alisema kuwa Aayah hii maana yake: “Malaika walitumwa wakiwa na uchawi, hivyo watu ambao Allaah Aliridhia wajaribiwe na watahiniwe. Allaah Aliwafanya waahidi mtihani, basi usikufuru”.

 

Pia Qataadah alisema: “Allaah Alichukua ahadi yao ya kutomfundisha uchawi mtu yeyote mpaka wamwambie, ‘Sisi ni mtihani, kwa hiyo usikufuru”.

 

Mitihani ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  huwapatia waja Wake ni aina nyingi na inaonekana huu ndio mtihani waliopatiwa watu baada ya kuaga dunia kwa Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis Salaam). Mtihani ilikuwa ni kuwatazama kama watabaki katika Iymaan au watakengeuka na maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Hilo ni onyo tulilolielezea hapo juu kulingana na wanachuoni ni yale maagizo waliyopatiwa hao Malaika na Muumba wao, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Baada ya agizo hilo, mtu mwenyewe anaachwa achague lile alitakalo. Na hili si balaa, kwani watu hawakulazimishwa kabisa katika kufanya huo uchawi. Pia Malaika hao hawakuwafunza watu bali walikuwa wanawaelekeza sehemu wanayotakiwa kwenda. Na hapo ndio walikuwa wanafundishwa hayo ya uchawi na Shaytwaan mwenyewe. Hata kama walikuwa wanawafunza ingekuwa ni ule mtihani waliopatiwa kupitia kwao tu, nao wakafeli mtihani huo. Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema:

 

“na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua.”

 

  

Na tufahamu kuwa uchawi haumdhuru mtu ila kwa idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

 

“Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah”

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share