Mume Hajali Ndoa Yake, Anafanya Maasi Ya Zinaa, Hafanyi ‘Ibaadah Yoyote, Nifanyeje?

SWALI:

 

mimi nimeolewa mume wangu hashuhuliki na ndoa hii haswali yeye yupo na anasa za dunia anabadilisha w/wke kila aina hii r'dhani analala na w/wke nje na hafungi na humu ndani halali na haya mambo tushayapeleka mpaka kwa wazazi lakini hasikii na nimeshachukua hatua tele kutaka abadilike lakini habadiliki, swala langu linauliza jee kwa sheriya ya kiislam nahitajika mimi nifanye nini juu ya m/mme huyu?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume wako aliye ‘aswi na asiyetekeleza wajibu wake kwa Allaah Aliyetukuka wala mkewe.

Hakika twakupongeza dada yetu kwa kuchukua hatua zote ulizozichukua juu ya kutaka mumeo abadilike. Juhudi hiyo haitaruka patupu bali una ujira mzuri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Ufahamu kuwa kwa sasa wewe hufai kukaa na mume kama huyo kwani anaweza kukuharibu na kukuharibia Dini yako. La kufanya sasa ni wewe kujaribu kuzungumza naye tena. Ikiwa hakusikia mpeleke mbele tena kwa wazazi na hapo waombe wamkanye na kumtaka arudi katika njia ya sawa. Ikiwa katika hilo hukufaulu basi itabidi umpeke kwa Qaadhi ambako kwa makosa aliyo nayo mumeo ni wewe kupewa talaka. Lau kabla ya kufika kwa Qaadhi unaweza ukazungumza na mumeo akupe talaka au ukawashilikia wazazi katika kikao chenu wamwambie mume atoe talaka itakuwa sawa. Ikiwa amekataa itabidi uende kwa Qaadhi ambako utapata talaka hiyo.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe istiqaamah na uweze kupita mtihani huu mgumu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share