Biashara Ya Vitu Vilivyokatazwa Na Serikali Japo Dini Haikuharamisha

SWALI:

 

Asalamu aleykum sheikh. Swali yangu ni kuhusu haramu na halali. nauliza hivi hapa nchini kwetu kuna vitu serikali imeharamisha, hata kama haijatajwa kwa quran. kwa mfano kufanya biashara juu ya wanyama wa porini kwa minajili ya pembe zao, ngozi n.k. Ni halali ama ni haramu kuchuma mali kwa njia hii ama ni haramu.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu biashara zilizokatazwa na serikali.

Huenda kukawa na biashara ambazo Kiislamu ni halali, lakini zikapigwa marufuku na serikali. Hilo ni jambo linaonekana katika nchi kadhaa ulimwenguni kwa sababu wanazodai wao kuwa ni za maslahi ya wanaadamu wenyewe.

Kufanya shughuli kama hizo ni halali kishari’ah kufanywa, hata hivyo kwa kufanya hilo huenda mtu akaingia katika matatizo na serikali. Hakika ni kuwa serikali inapopiga marufuku jambo huwa mwenye kufanya hana budi kufanya kwa siri na anapogunduliwa basi huwa kuna adhabu ambayo atapatiwa – ima kufungwa, kutozwa faini au adhabu nyengine yoyote ile.

 

Kwa minajili hiyo kwa nini Muislamu ajiingize katika matatizo kwa kufanya biashara hizo ambazo atakuwa anazifanya kwa siri na huenda zikampelekea katika madhambi makubwa kama kutoa hongo (rushwa) na mengineyo. Ni bora Muislamu kuacha biashara hizo hadi waweze kuzungumza na kuelewana na serikali kuihalalisha.

 

Uislamu unazingatia kuwa wanyama wana haki ya kuishi kama wanaadamu na wanauliwa tu kwa maslahi ya wanaadamu kama kula nyama yao au kutodhurika nao.

 

Kwa ajili hiyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa ruhusa hata kwa muhrim kuwaua wanayama wa tano lakini wote hawa hawana maslahi na wanaadamu. Nao ni nnge, panya, mbwa mwenye kichaa, kunguru na kipanga (al-Bukhaariy).

 

Ama kumuua tu mnyama kwa sababu ya ngozi, pembe au kimchezo ni jambo ambalo halifai isipokuwa anapoleta maafa kwa wanaadamu. Hivyo, ni afadhali uachane na biashara hiyo na uanze kufanya nyingine njema isiyo na utata.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share