Shia Anauliza Ikiwa Swahaba Walikimbia Vita Vya Hunayn, Iweje Wanatukuzwa?

SWALI:

 

Assalamu Aleikum warahmatullahi wabarakatuhu, sifa Bismillahi Rahmanir Rahim, Sifa njema zote ni stahiki ya Mwenyezi Mungu (S.W) na Rehma na Amani zimiminike juu ya Mjumbe wake Mtukufu Sayyidna Muhammad (S.A.W.W). 

Ama baada ya hayo yaliyotangulia mimi ninapenda kuuliza kuwa kwa nini baadhi ya maswahaba ambao wamekemewa katika Surati-Tawbah kuhusu kukimbia katika vita vya Hunayn kama Umar ibni Khatabi na Uthman ibn Affaan, tunawaadhimisha sana, na kuwanyanyua vyeo kwa hadithi ambazo zilitungwa na watu wa bani Ummayah ili kuficha uovu wao (ikiwemo kukimbia siku ya vta vya Hunayn, jambo ambalo ni miongoni mwa madhambi makubwa) na kuwatakia radhi za Mwenyezi Mungu wakati Mungu Mwenyewe Amebainisha kuwachukia ndani ya Surati-Tawbah? Hilo ndilo swali langu, Wabillahi Tawfiq.


 

JIBU: 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) kukimbia katika vita vya Hunayn.

 

Muulizaji ili afahamu vyema kuhusu suala hilo na ikiwa kweli anataka kufahamu haki, basi anaweza kutazama Suratut Tawbah, Aayah 25 inayotupatia muhtasari kuhusu jambo hilo. 

Kisha tungemuomba kila Muislamu mwenye kutumia akili yake na sio ufuataji wa itikadi potofu ambao wametiwa chuki juu ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) arudi kwa Tafsiyr Ibn Kathiyr atazame majina ya wale waliobaki pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao hawajakimbia. Miongoni mwa waliobakia pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Lazima tufahamu kuwa Ibn Kathiyr si Banu Umayyah na hivyo hiyo tuhuma ya Mashia kuwa walihongwa, wasije wakamtupia na Ibn Kathiyr vilevile. 

Kisha Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wametukuzwa na Allaah Aliyetukuka katika Kitabu Chake cha Qur-aan.

 

Sijui pia kama kuna mwenye akili zake timamu anaweza kusema kuwa Qur-aan nayo imeandikwa na Banu Umayyah?

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Kwa hakika Allaah Amewapa radhi Waumini walipofungamana nawe chini ya mti, na Alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi Akateremsha utulivu juu yao, na Akawalipa kwa Ushindi wa karibu” [Al-Fath 48: 18].

 

Miongoni mwa waliokula kiapo chini ya mti cha kuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ilhali ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa amezuiliwa na makafiri wa Makkah mpaka ukatoka uvumi kuwa ameuliwa ndio mafungamano haya yakafanyika kulipiza kisasi cha kifo hicho.

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaendelea,

Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Allaah. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu.” [Al-Fath 48: 29].

 

Na Akaeleza tena:

Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Muhaajiriyn na Answaar, na waliowafuata kwa wema, Allaah Ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na Amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa” [At-Tawbah 9: 100]. 

 

Allaah Aliyetukuka Anasema Anawafahamu vyema na Anajua yaliyo ndani ya nyoyo zao. Sisi sijui ni kina nani kusema kuwa si hivyo Alivyosema Allaah Aliyetukuka. 

 

Rudi tena tazama katika Hadiyth unazosema ni za kutungwa hakuna Banu Umayyah aliyetunga au kuandika Hadiyth za Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kinyume na hivyo utakuta wakusanyaji Hadiyth wengi wala hawakuwa Waarabu kama Imaam al-Bukhaariy licha ya kuwa ni Banu Umayyah. 

 

Kinyume chake Mashia ndio wenye kutunga Hadiyth. Ukitazama vitabu vyao vya Hadiyth kama Al-Kaafiy vimejaa Hadiyth mbovu za ajabu na zingine zenye kufru za wazi kabisa kama zile za kuwatukuza Maimaam wao na kudai kuwa wanajua Ghayb na wanajua lini watakufa na wana ubora kuliko hata Mitume wote isipokuwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Na sifa ya uongo huwezi kuipata isipokuwa kwa Mashia, na sifa ya kutunga Hadiyth imejaa kwa Mashia na kwenye vitabu vyao vya Hadiyth. 

 

Nasaha zetu kwa ndugu muulizaji na wote wenye kulaghaika na Mashia, warudi wasome na watafute elimu kwa Niyah safi na kumuomba Allaah Mtukufu Awaongoze kwenye njia ya Haki na Awaepushe na dini hiyo yenye kukufurisha Maswahaba na Waislamu, dini iliyojaa kufru, chuki, uadui na visasi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share