Wanandoa Waliopeana Talaka Kukutana Mara kwa Mara

SWALI: 

Assalam Aleikum, 

Nigependa kutoa shukurani zangu za dhati kwa juhudi zenu juu ya kutuelimisha sisi waislamu. Nimejaribu kutafuta jawabu juu ya swala la mawasiliano baina ya mke na mume ambao wametalikiana na wanaishi mbalimbali.

Kwa kirefu ni kwamba mume aliyekua amemua mwanamke na akaishi nae ambapo maisha hayakua yakuelewana na akampa talaka. Katika ndoa yao wameruzukiwa na mtoto moja. Mume huyu akaoa mke mwengine, lakini kila siku watalaka hawa wawili wanazungumza kwa simu, saa nyingine huonana na kuzungumza kuhusu mambo ya mtoto na hata maisha yao. Mwanamume huyu hujitolea hata kumuangalia kwa matumizi huyu mwanamke na mambo mengine. Na watalaka hawa hufanya mambo kama ambae wako pamoja. Huyu Mke wa sasa amemsihi mumewe basi kama hali iko hivi akaombwa amrudie, lakini husema hataki, wala hana haja nae.

Swali langu ni Jee yafaa watalaka kuonana na kuzungumza saa zote, ama kuna taratibu ambazo wataka wafuaate? Kama haifai nini hukmu yake ama malipo yake.


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wanawake waliotalikiwa na mume kukutana mara kwa mara.

Hakika Uislamu ni kama alivyotuambia Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Tangamana na watu kwa wema na uzuri” (at-Tirmidhiy).

Hivyo, kunaruhusiwa wanandoa walioachana kukutana kwa malengo hayo ya kumuona mtoto na kujadili yanayomhusu huyo mtoto mfano wa mahitaji yake, masomo yake, matibabu, na maangalizi mengine. Wanaruhusiwa kwa dharura kuzungumza kwenye simu kuhusiana na mas-alah kama hayo. Lakini kukutana kwao au kuzungumza kwao ikibidi, lazima kuwe na mipaka ya kishariy'ah na kwa dharura tu ihusuyo mtoto na si kwa mengine kwani hao kwa wakati huu si Mahram.

Pindi wanapokutana ni vizuri kuwepo mtu wa tatu au kusiwe ni faragha peke yao. Kukutana faragha ni khatari na kunaweza kuingia fitnah katikati.

Kuna mifano mingi ya matukio ya watu walioachana kisha wakawa wanakutana kwa ajili ya mtoto au watoto na matokeo yake kwa kukosekana mipaka baina yao, wakawa wametumbikia katika zinaa.

Vilevile kuepukwe kukutana bila sababu kama hizo au mawasiliano ya mara kwa mara kwa simu na kuongea mengine yasiyohusiana na hayo yenye kuwaunganisha -ambayo ni mtoto wao- basi shari'ah hairuhusu mahusiano kama hayo kwani wao si Mahram na huenda mawasiliano hayo yakawa ni katika kukurubia Zinaa kulikokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Hivyo, nasaha tunazotoa kwa watalaka hao na haswa mume, ni kujiepusha na mawasiliano ya karibu na ya mara kwa mara na mtalaka wake, na mazungumzo mengi na kukutana mara kwa mara bila mipaka na bila kuwepo mtu wa tatu, Shaytwaan atakuwa wa tatu wao na atawachezea na kuwashawishi waingie kwenye Haraam.

Ushauri aliopewa na mke wake wa sasa wa kumrudia huyo mke wake wa zamani, ni ushauri mzuri sana wa busara, na isitoshe angemshukuru sana mke wake wa sasa kwa kumrahisishia jambo hilo ambalo ni gumu kwa wake wengi kukubali mas-ala ya uke wenza.

Mume huyo anahitaji kuzidi kupewa nasaha na kukumbushwa makatazo ya Diyn ya maingiliano yasiyo na mpaka na mtu asiye Mahram wake, na kadhalika ikiwa hajui, afahamishwe misingi ya Shariy'ah na mipaka yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share