Kufunga Mikono Katika Swalah

Kufunga Mikono Katika Swalaah

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Kufunga mikono katika Swalaah ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni jambo alilolisisitiza sana katika Swalaah na hata kuwasahihisha wale waliokuwa wakikosea kufunga mikono yao ndani ya Swalaah. Isitoshe ni Sunnah sahihi iliyothibiti hata kwa Manabii  waliotangulia kama anavyotujulisha mwenyewe Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika Hadiyth zifuatazo.  

 

Hakuna ushahidi wala dalili wala mapokezi sahihi yoyote yanayoonyesha kinyume na kufunga mikono kwenye Swalaah kutoka kwake yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wala Maswahaba zake.

 

 

Hadiyth Za Kufunga Mikono

 

Ama Hadiyth zinazoeleza juu ya Kufunga mikono ni nyingi sana na zinapatikana katika kitabu Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam). cha Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) kilichopo ndani ya ALHIDAAYA kwa lugha ya Kiswahili Na pia ndani ya kitabu cha 'Al-Qawl Al-Mubiyn fiy Akhtwaa Al-Muswalliyn) kilichoandikwa na Shaykh Mash-huwr Hasan Salmaan na pia ndani ya kitabu cha Fiqhus Sunnah cha Sayyid Saabiq na kwenye kitabu cha Swahiyhu Fiqhus Sunnah cha Abu Maalik Kamaal kilichopo ALHIDAAYA Swahiyh Fiqhus Sunnah na ndani ya vitabu vingi sana vya Fiqh na vya Hadiyth sahihi.

 

 

Anasema 'Bahari ya elimu' Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kuwa;
"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;
"Sisi Manabii tumeamrishwa kuharakisha kula futari zetu na kuchelewesha kula daku letu, na kuweka mikono yetu ya kulia juu ya kushoto ndani ya Swalaah."
[At-Twabaraaniy na Ibn Hibbaan]

 

 

Na katika Sunan za Abu Daawuwd Hadiyth iliyosahihishwa na Ibn Khuzaymah inasema;

 

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto."

 

Imepokelewa pia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona mtu mmoja akiswali huku ameweka mkono wake wa kushoto juu ya mkono wa kulia, akauondoa na kuuweka wa kulia juu ya kushoto." [Ahmad na Abu Daawuud].

 

Na imepokelewa kutoka kwa Swahaba Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa katika Swalaah ya maiti Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alinyanyua mikono yake juu akasema “Allahu Akbar:”, kisha akauweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto." [At-Tirmidhiy katika ‘Baab maa jaa fiy raf’il yadayni.]

 

 

Imepokelewa katika Swahiyh Muslim na kutoka kwa Imam Ahmad na At-Twabaraaniy kuwa:

"Na alikuwa akiuweka mkono wake wa kulia juu ya sehemu ya nyuma (mgongo) ya mkono wa kushoto."

 

Katika mlango huu zimepokelewa Hadiyth zaidi ya ishirini kutoka kwa Maswahaba kumi na nane pamoja na waliowafuatilia (Taabi’iyn), zote hizo zikitoka moja kwa moja  kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Kutoka kwa Swahaba Waail bin Hujr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema;

"Kama kwamba namtazama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) namna alivyokuwa akiswali", akasema:
"Nikamtazama! akatoa takbiyr, kisha akanyanyua mikono yake mpaka ikakaribia masikio yake, kisha akauweka wa kulia juu ya upande wa nyuma wa mkono wa kushoto."
[Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake na An-Nasaaiy na Abu Daawuwd katika Sunan yake na Ahmad katika Musnad yake 4/318 na Ibn Maajah katika Sunan yake 1/266 na Ad-Daarimiy katika Sunan yake 1/314 na Ibnul Jaruud katika Al-Muntaqaa Hadiyth nambari 208 na katika vitabu vingi vingine"].

 

 

Anasema Imaam Maalik (Allaah Amrehemu) katika kitabu cha Al-Muwattwaa, na huyu ni Imaam wa watu wa Madiynah mji alioishi na kuswali ndani yake Mtume wa Allaah zaidi ya miaka kumi, na Maswahaba wake watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wakaendelea kuswali hapo miaka mingi iliyofuata.

 

 

Katika ukurasa wa 122 na 123 mlango wa "Mwenye kuswali aweke mkono mmoja juu ya mwengine",  imeandikwa katika kitabu hicho cha Imaam Maalik katika Hadiyth nambari 133 kama ifuatavyo:

 

"Katika maneno ya Manabii ni kuwa usipokuwa na haya basi fanya utakalo, na pia (katika maneno ya Mitume) ni kuweka mkono mmoja juu ya mwengine katika Swalaah."

 

Haya ni maneno ya Imaam Maalik ndani ya kitabu chake cha Al-Muwattwaa.
 

Na katika kitabu hicho hicho cha Al-Muwattwaa Imaam Maalik ameandika Hadiyth kutoka kwa Sahl bin Sa’ad Al Saa’idiy kuwa:

“Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Swalaah."

 

Anasema Abu Haazim;

"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". [Al-Bukhaariy Juz. 1 ukurasa wa 397 Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa na Imaam Ahmad katika Musnad.]

 

Na katika kuisherehesha Hadiyth hiyo amesema Imaam Maalik (Allaah Amrehemu);

"Kuweka (mkono) wa kulia juu ya kushoto na kuharakisha futari na kuchelewesha daku."

Haya ameyasema katika kuisherehesha Hadiyth iliyotangulia ya Abul Mukhariq.

 

Baadhi ya watu wakasema kuwa katika Hadiyth iliyomo ndani ya Al-Muwattwaa yumo Abul Mukhariq na huyu anajulikana kuwa ni dhaifu katika elimu ya Hadiyth, lakini inaeleweka pia katika elimu ya Hadiyth kuwa udhaifu wa wapokezi unakhitalifiana darja, na kwamba daraja inayokubalika Hadiyth zao katika madhaifu ni wale waliodhoofishwa kwa ajili ya udhaifu wao wa kuhifadhi ikiwa wao si watu waongo wala si wenye kupenda kuongeza maneno.

 

Madhaifu wa aina hii anasema Dr. Muhammad Ajjaaj Al-Khatwiyb katika kitabu chake cha 'Al-Mukhtasar Al-Wajiyz fiy Uluwm Al-Hadiyth kuwa;

"Mtu aliyedhoofishwa kwa ajili ya kuhifadhi kwake, au kwa ajili ya kutoweza kudhibiti maneno vizuri, ikiwa hatuhumiwa kwa ila nyingine, na ikiwa zitapokewa Hadiyth zake kwa njia nyingi, basi Hadiyth itapanda na kufikia darja ya Hadiyth 'Hasan', na kwa ajili hiyo udhaifu wake unatoweka kwa kupokelewa Hadiyth kwa njia nyingine."

Anasema Imaam Muhammad bin Al Hassan Al Shaybaniy kuwa;

"Anatuhumiwa Abul Mukhariq kwa udhaifu wake wa kuhifadhi tu."

 

Isitoshe ndani ya kitabu hicho cha Al-Muwattwaa ipo pia Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) na kunukuliwa pia na Maimaam Ahmad na Al-Bukhaariy na wengineo, inayosema;

"Watu (wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) walikuwa wakiamrishwa kuweka mikono yao ya kulia juu ya kushoto katika Swalaah."

 

 

 

Je, Imaam Maalik Alikuwa Akiaachia Mikono Na Alisema Watu Waachie Mikono Kwenye Swalaah?

 

Yaliyoandikwa ndani ya kitabu cha Bidaayatul Mujtahid si kukanusha kufunga mikono bali ni kuthibitisha, isipokuwa tu imenukuliwa ndani ya kitabu hicho kuwa Imaam Maalik amejuzisha kufunga katika Swalaah ya Sunnah na hakujuzisha katika Swalah ya fardhi akihofia watu wasiwe wanafunga kwa ajili ya kujipumzisha tu na wasidhani kuwa ni nguzo mojawapo ya Swalaah na kwamba Swalaah inabatilika iwapo mtu atafanya kinyume cha hivyo (hii ikiwa kweli imethibiti kuwa Imaam Maalik amesema hayo), lakini yaliyomo ndani ya kitabu chake cha Al-Muwattwaa ni kinyume na hayo yaliyoelezwa.

 

Na yanayofanywa na baadhi ya wafuasi wa Imaam Maalik wanaoachia mikono kwenye Swalah zao kama wafanyavyo baadhi ya watu wenye itikadi zisizo za Ahlus Sunnah wal Jama’ah, ni jambo ambalo halina dalili kwenye Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wala Maswahaba zake wala hata Imaam Maalik mwenyewe.

 

Hivyo, tumeona kuwa hapana Hadiyth Swahiyh hata moja kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema watu waachie mikono katika Swalaah au kuonyesha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya kinyume na kufunga mikono kwenye Swalaah, na hii ni kauli ya wengi sana katika Maswahaba na Taabi’iyna (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na haya ndiyo aliyonukuu Imaam Maalik katika Al-Muwattwaa.

 

Na Allaah Ni Mjuzi Zaidi

 

 

 

Share