12-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Hatari Ya Bid’ah (Uzushi)

 

Hatari Ya Bid’ah (Uzushi)

 

‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

”Yeyote atakayeanzisha kitu katika jambo  (Dini) letu hili ambalo halimo, basi litakataliwa (litarejeshwa).”[1]

 

Na katika Hadiyth ya Muslim,

“Anayefanya ‘amali ambayo si katika jambo (Dini) letu, basi itarejeshwa.” [2]

                           

Ni desturi ya hatari sana kutafuta ukuruba wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) bila kufuata Qur-aan, Sunnah, na njia ya watakatifu (wacha-Mungu) waliotutangulia. Aidha kutowafuata wao inaonesha ujasiri wa kijuvi, pupa na kuchupa mipaka ya Allaah.

 

Kama fahamu za mtu zinamruhusu kuiba dola moja au dola kumi, atakuwa hana kipingamizi cha kuiba dola elfu moja. Ni sawa na kadhia ya mzushi: akiridhika kuchepuka kutoka Sunnah za Mtume, wakati huo akiridhika na bid’ah moja, bid’ah kubwa na pengine hata shirk itakuwa sahala (nyepesi) kwake. Hatua hiyo ya kwanza ya kuridhia kukengeuka na bid’ah inarahisisha hatua za mbele zinazopelekea kwa kila aina ya upotovu. Hii ndio ilikuwa hali ya watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam), ambao walifanya masanamu ya baadhi ya watukufu wao kuwa miungu baada ya wao kufariki dunia.

 

Mwanzoni, walipokufa tu, Shaytwaan aliwashawishi watu wajenge masanamu baada yao, ili wawakumbuke na waige ‘amali zao njema. Kisha, baada ya kupita karne kwa karne, watu waliposahau lengo la awali la masanamu hayo, Shaytwaan aliwashauri kuabudu masanamu badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), akiwadanganya na madai potofu ya kuwa baba yao ndiye aliyekuwa akiyaabudu.

 

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema,

“Masanamu kutoka kwa watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam) yalishuka miongoni mwa Waarabu baadaye. Ama Wudd (jina la moja ya masanamu), alikuwa wa Kalb katika Dawmat Al-Jandal; Suwa’ alikuwa wa Hudhayl; Yaghuuth alikuwa wa Murad; Thamma alikuwa wa Bani Ghalif huko Jurf, akiwa na Saba; Ya’uuq alikuwa wa Hamdaan; na Nasr wa Hamayr; kwa ukoo wa Kila’. Wao (masanamu) ni majina ya wacha-Mungu miongoni mwa watu wa Nuuh (‘Alayhis Salaam). Walipofariki dunia, Shaytwaan aliwashawishi wasimamishe (wajenge) masanamu ya hao, walipokuwa wakikusanyika na waliyapa majina yao. Walijenga masanamu lakini hawakuyaabudu.

Kizazi hiki kilipopotea na elimu ilipofutika, masanamu yalifanywa vitu vya kuabudiwa.” [3]

 

Hivyo ndivyo Shaytwaan alivyowaghilibu taratibu, kwanza kuzua na kisha kufanya shrik na kukufuru. Endapo wangekata uhusiano kati yao na Shaytwaan kutokea mwanzo, kama wangeminya tatizo katika tumba lake, wasingeanguka kwenye lindi la uovu na ukafiri.

 

Sawa na hilo lilitokea kwa bahati mbaya kwa makundi ya Ummah wetu; mfano mmoja ni kundi moja lililokuwa likikusanyika ndani ya Msikiti. Kwa kila mkusanyiko alikuwepo kiongozi, na kila mshiriki alikuwa na vijiwe mkononi. Kiongozi alisema, “Semeni Takbiyr (Allaahu Akbar) Allaah Mkubwa mara 100, na kila aliyekuwepo alisema mara 100. Waliendelea kufanya hivyo kwa Tahliyl (wakisema, Hapana apasaye kuabudiwa ila Allaah) na kwa Tasbiyh (wakisema, Ametakasika Allaah!) ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwalaani kwa matendo yao.

 

Katika Hadiyth Swahiyh, al-Hakam bin al-Mubaarak alipokea kutoka kwa ‘Umar Bin Yahya, aliyesema, “Nilimsikia baba yangu akisimulia ya kuwa alimsikia baba yake akisema,

Tulikuwa tukikaa kwenye mlango wa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kabla ya Swalah ya Alfajiri, na alipotoka nje, tulikwenda naye Msikitini.

 

Asubuhi moja, Abu Muusa Al-Ash’aariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitujia na kusema, “Je, Abu ‘Abdir-Rahmaan (‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameshatoka nje? Tulijibu, “Hapana” na hivyo Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikaa nasi mpaka alipotoka. Alipotoka, Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan! Nimeona jambo Msikitini nililolizuia, hata hivyo – AlhamduliLlaah – kila nilichokiona ni kizuri. ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliuliza, na kilikuwa kitu gani? Alijibu, “Iwapo utaishi (kwa kitambo kidogo) utakiona. Niliona makundi katika mduara, walikaa wakisubiri Swalah. Katika kila duara alikuwepo mtu (kiongozi), na wote walikuwa na kokoto mikononi mwao.

Kiongozi alisema: fanyeni Takbiyr mara 100, nao walifanya Takbiyr mara 100. Kisha alisema, fanyeni Tahliyl mara 100 na wakafanya Tahliyl mara 100.

Na kisha aliposema Tasbiyh mara 100, na wakafanya ‘Tasbiyh mara 100. Na uliwaambia nini?  Aliuliza ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu). Sikusema lolote, kwani nilisubiri kujua rai yako kwanza kuhusu suala hili au nipokee amri yako! Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu), Ni wewe uliowataka wahesabu madhambi yao…”

Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikwenda tukimsindikiza mpaka alipokuta waliokusanyika ‘Abdullaah bin Mas’uud aliwasimamia na kusema, “Ni jambo gani hili mlifanyalo?” Walijibu, ‘Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan (yaani ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) tumetumia hizi kokoto kuhesabu idadi ya Takbiyr, Tahliyl na Tasbiyh tunazofanya.

”Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Basi hesabuni madhambi yenu… Mlaaniwe, Enyi Ummah wa Muhammad, vipi maangamifu yamewafika mapema! Hawa ndiyo Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika idadi yenye kutosheleza hii ni nguo ambayo ilikuwa bado imetatuka na hii ni sahani yake bado haijavunjika (yaani, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia hivi karibuni na tayari mmepotoka). Naapa kwa Yule ambaye Roho yangu iko mikononi Mwake, ama mpo kwenye Dini yenye mwongozo kuliko Dini ya Muhammad, au ni wafunguzi wa mlango wa upotofu.”

Walisema, “WaLlaahi, Ewe Abu ‘Abdir-Rahmaan, tulikusudia kufanya mema, lakini hatukufikia lengo!

 

Kwa hakika, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizungumza nasi, akisema kikundi cha watu walikuwa wakisoma Qur-aan, hata hivyo haipitii mitulinga yao.

WaLlaahi, sijui lakini pengine wengi wao ni miongoni mwenu. Kisha aligeuka na kuondoka.

 

‘Amr Bin Salamah alisema, “Tuliwaona washiriki wengi wa mikusanyiko (hiyo) wakipigana dhidi yetu siku ya An-Nahrawaan wakiwa upande wa Khawaarij.”[4]

Kilichoonekana ni kitu kidogo japo ni kikubwa si kwa sababu walikuwa wakimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika njia ambayo haikuamriwa kwenye Qur-aan au Sunnah, na hivyo waliongozwa kwenye uovu. Kama vile, waliishia kuwapiga Waislamu katika Siku ya Nahrawan wakishirikiana na Khaawarij. Hivyo waliacha njia ya Waumini, mwanzoni walifanyaje At-Tasbiyh, At-Tahliyl na At-Takbiyr –huku wakidai ya kuwa walichokuwa wakikitaka ni kutenda mema na baadaye kupigana dhidi ya Waislamu – na pengine walitatizika na kufikiria ya kuwa walikuwa wakitenda mema.

 

 [1] Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[2] Muslim (1718).

[3]Ilisimuliwa na Al-Bukhaariy (4920), na Al-Haafidh alitaja ya kuwa Hadiyth hii haikuungana japokuwa ni Swahiyh kwa sababu ya Silsilah nyingine yenye nguvu kutoka kwa Ibn ‘Abbaas na ilishuhudiwa na mwanafunzi wake, ‘Ikrimah katika Tafsiri ya At-Twabariy. Shaykh wetu (Allaah Amuwie radhi) alitufahamisha hivyo, na taarifa hii aliiweka katika toleo la Pili lililopitiwa la “Tahdhiyr al-Masaajid Fiyttikhaadh Al-Qubuur Masaajid.”

[4] Alisimulia Ad-Daarimiy (1/68) na Silsilah yake ni Swahiyh, kwani wasimulizi wake wote ni waaminifu. Rejea Ar-Radd ‘Alaa at-Ta’aqqub al-Hathiyth (uk. 47) kilichoandikwa na Shaykh, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi).

Share