Kushika Na Kusoma Qur-aan Katika Hedhi, Nifaas Na Janaba

 

Kushika Na Kusoma Qur-aan Katika Hedhi, Nifaas Na Janaba

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Jee mtu anapokua na hedhi, nifasi au Janaba anaweza kusoma Qur-an bila ya kuishika, na nini sheria yake katika hayo?? 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Suala la mwenye Hedhi kusoma Qur-aan ni suala ambalo 'ulamaa wametofautiana hukmu yake lakini ni suala lisilo na makatazo yaliyothibiti kishari'ah katika Hadiyth Sahihi. Na waliopinga mwanamke kusoma wametoa zaidi dalili ya Hadiyth inayosema: (("Hasomi mwenye janaba au mwenye hedhi chochote katika Qur-aan"))  Imesimuliwa na Abu Dawud, At Tirmidhy na Ibn Maajah. Lakini Hadiyth hii ni DHAIFU kwa mujibu wa wanachuoni wa Hadiyth na wengineo akiwemo Imam Al-Bukhaariy, Ahmad bin Hanbali, Al-Bayhaqiy, Ibn Taymiyah, Ash-Shawkaaniy, Al-Albaaniy na wengineo.

 

Na pia waliopinga pamoja na wengi miongoni mwao kukubali kuwa mwanamke anaweza kusoma kimoyomoyo, au hata kwa sauti kwa mujibu wa wengine, lakini wamepinga kuishika hiyo Qur-aan na wametoa hoja ya kuwa mwanamke katika hali hiyo si msafi kuweza kushika Qur-aan kwa kutoa ushahidi wa aya isemayo:

 

لاَ يَمَسُّهُ إِلاَّ الْمُطَهَّرُونَ  

Haigusi isipokuwa waliotakaswa kabisa. [Al-Waaqi'ah: 79]

 

Lakini pamoja na baadhi ya Maulamaa kusema kuwa aya hiyo imekusudiwa watu wote, ila kauli iliyo sahihi ya wafasiri, ni kuwa makusudio ya 'Al Mutwahharuun' katika aya hiyo ni Malaika na si wanaadam na isiyoguswa hapo si hii Misaahafu yetu tuliyonayo, bali ni Allawhul Mahfuwdh na aya za nyuma yake za 77 na 78 zinaonyesha kuwa ni Qur-aan tukufu katika Kitabu kilichohifadhiwa ambacho kiko mbinguni  zinathibitisha hilo.

 

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ ﴿٧٧﴾فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ ﴿٧٨﴾

Hakika hii bila shaka ni Qur-aan tukufu. Katika Kitabu kilichohifadhiwa. [Al-Waqi'ah 77-78]

 

Na 'ulamaa na wema waliopita wanasema kuwa waliotakaswa ni Malaika na si wanaadam. Tazama pia tafsiri ya Ibn Kathiyr.

 

Kwa hiyo, maadam aayah hiyo haiwakusudii wanaadam, na Hadiyth iliyotajwa mbeleni ya makatazo ya kusoma Qur-aan mwenye hedhi si sahihi, basi suala hili labaki kuwa lafaa hadi pawepo makatazo yaliyothibiti.

 

Na hoja nyingine ya kuonyesha kuwa jambo hilo halina makatazo, ni Hadiyth ((iliyosimuliwa na Jaabir bin 'Abdillaah kuwa katika tarehe nane ya mwezi wa Dhul Hijjah siku ijulikanayo kuwa ni ya 'Tarwiyah' walipokuwa wakielekea Minaa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wakaleta talbiya ya Hijjah, kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaenda kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) akamkuta analia, akamuuliza: ''una nini?'' akajibu ('Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anha)) ''Nimepatwa na hedhi na watu wamehirimia na wamefanya twawaaf nami sijafanya vyote hivyo! Na watu wanaelekea kuhiji hivi sasa!!'' Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Hili ni jambo Aliloliandika Allaah kwa wanawake (wanaadam), basi nenda kaoge halafu kahirimie kisha Hiji na fanya yale anayofanya Mwenye kuhiji isipokuwa usitufu na kuswali". 'Aaishah akafanya matendo yote ya Hajj isipokuwa kufanya Twawaaf na Swalah.))

 

Hadiyth hii ya Jaabir inatuonyesha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu kufanya yote afanyayo mwenye kuhiji kwenda Minaa kulala, kwenda 'Arafah, kutupa mawe na hata kwenda 'Swafaa wal Marwaa' ambako hapo kunasomwa aya isemayo:

 

 إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾   

Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya khayr basi hakika Allaah ni Mwenye kupokea shukurani, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 158]

 

Kwa hiyo hapa tunaona kuwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliruhusiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya hata hayo ya Swafaa wal Marwaa ya kusoma Qur-aan, kwa kauli ya ((Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) "Fanya yote afanyayo mwenye kuhiji isipokuwa Twawaaf na Swalah")). Na ndio moja ya hoja ya 'Ulamaa wanaoona kuwa hakatazwi mwenye hedhi kusoma Qur-aan.

 

Pia tunaona kuna mgawanyiko wa makundi matatu kuhusu kusomwa Qur-aan na Mwenye Hedhi, Mwenye Nifaas na Mwenye Janaba;

 

Kundi la kwanza linasema wanaweza kusoma Qur-aan nalo ni Swahaba Mtukufu Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu), Imaam Al-Bukhaariy, Ibn Mundhir na wengineo katika wema waliotangulia.

 

Kundi la pili ni la watu wa zama za Imaam Ahmad wanaojulikana Ahlul Hadiyth wao wanasema inajuzu kusoma lakini makruhu.

 

Kundi la tatu ni la ma-Imaam wa madhehebu ya ki- Shafi'i, Hanafi n.k. hayo yanapinga kabisa kusoma Qur-aan kwa watu wa hali hizo juu.

 

Kwa kufupisha, tunaona kwamba hakuna makatazo sahihi thabiti yenye kukataza mwanamke mwenye hedhi kusoma Qur-aan wala mwenye Nifaas na hata mwenye Janaba ingawa kwa maoni ya wengi miongoni mwa 'Ulamaa wanaonelea kuwa mwenye janaba inachukiza kwake kusoma kwa sababu hali yake inaweza kubadilika mara moja kwa kuoga janaba, yaani ni jambo ana khiyari nalo huyo mwenye janaba. Ila hali inakuwa tofauti kwa mwenye hedhi na nifaas kwa sababu wao hawana khiyari yoyote kwa hali hiyo iwapatayo ya kimaumbile.

 

Na mwanamke mwenye hedhi kushika Qur-aan, waliolikubali wamesema ni vizuri kushika kwa kitu glavu, au kuweka kizuizi chochote katika mkono. Lakini wanachuoni wote wamekubaliana ni rukhsa kushika Qur-aan ya Tafsiri na magazeti au vitabu vyovyote vyenye Qur-aan ndani yake isipokuwa Msahafu.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share