000-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Utangulizi

 

 

 

 

Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake

 

 

 

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحِيم

 

 

Utangulizi:

 

 

Himdi Anastahiki Allaah (سبحانه وتعالى) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimfikie Nabiy Muhammad (صلى الله عليه  وآله وسلم ) na jamaa zake, na Swahaba zake (رضي الله عنهم)  na wote waliotangulia kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Imekuwa ni waajib wa kila Muislamu kufikisha ujumbe kwa kuamrishana mema na kukatazana maovu kama Anavyoamrisha Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾

Na watokeze kutoka kwenu umati wa watu unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu. [Aal-‘Imraan: 104]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah [Aal-‘Imraan 110]

 

 

Waajib huo wa kuamrishana mema na kukatazana maovu umetiliwa nguvu mno na jambo hili kuwa adhimu hadi kwamba baadhi ya 'Ulamaa wameona waongezee katika nguzo za kiislamu [Wujuwb Al-Amr Bil Ma’ruwf  Wan-Nahy ‘Anil-Munkari - Shaykh Swaalih Al-Fawzaan].  Wengineo wakanukuu dalili kadhaa, miongoni mwazo ni kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) zilotangulia za Suwratul-‘Imraan.

 

Makemeo makali yametolewa na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutokukatazana maovu kama vile  Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyowalaani waliopewa vitabu nyuma yetu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿٧٨﴾

Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israaiyl kwa lisani  ya Daawuwd na ‘Iysaa mwana wa Maryam. Hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakitaadi.

 

كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٧٩﴾

Walikuwa hawakatazani munkari waliyofanya. Uovu ulioje waliyokuwa wakiyafanya. [Al-Maaidah: 78-79]

 

 

Bali kuna onyo kali la kuteremshiwa adhabu kwa kutokutekeleza amri hii na juu ya hivyo, ni sababu mojawapo ya kutokutakabaliwa du’aa zetu kama ilivyothibiti katika usimulizi ufuatao:

 

عن حُذيفةَ بنِ اليَمانِ عن النَّبيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلِيهِ وسَلَّم قال: ((والَّذي نَفْسي بيدهِ لتأمرُنَّ بالمعروفِ ولتَنهوُنَّ عن المنكرِ وليوشِكَنَّ اللهُ أنْ يبعثَ عليكُمْ عقاباً منهُ فتدعونَهُ فلا يَستجيبُ لكُمْ)) الترمذي وصححه الألباني

Imepokelewa toka kwa Hudhayfah bin al-Yamaani  (رضي الله عنه) kutoka kwa Nabiy kwamba amesema: ((Naapa kwa Yule nafsi yangu ipo mikononi mwake, mtaamrishana ma’ruwf [mema] na kukatazana munkari [maovu] ama Atawaunganishia kwa kuwapa mfano wake Allaah na kuwateremshia nyinyi adhabu itokayo Kwake, kisha mumuombe Yeye na Asiwajibu du’aa zenu)) [At-Tirmidhiy na akaisahihisha Al-Albaaniy]

 

 

Zimethibiti pia Hadiyth nyinginezo za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) zinazotoa maonyo zaidi ya hayo na zinazobashiria fadhila tukufu za kuamrishana mema na kukatazana maovu. Na hii ilikuwa ndio kazi ya Rusuli wote kuwalingania watu wao waachane na maovu na washikamane na yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى). Na kutokana na umuhimu wake, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametuamrisha tufikishe ujumbe japo kwa Aayah moja kama alivyosema:

 

((بَلِّغُوا عَنِّي وَلَوْ آيَةً))

((Fikisheni kutoka kwangu [ujumbe] japo Aayah moja)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Kitabu hiki kwa tawfiyq ya Allaah (سبحانه وتعالى), kitamsaidia yeyote anayetaka kufuata amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه  وآله وسلم ), kwani Hadiyth moja itamtosheleza kabisa mtu kulingania kutokana na maamrisho na makatazo yake.

 

 

Hadiyth zote (isipokuwa ya Hitimisho) nimezitoa katika kitabu cha Riyaadhus-Swaalihiyn kwa kuingia katika Milango yake na kutoa Hadiyth moja au zaidi yake ambazo nimehisi kuwa zina mafunzo muhimu kwa Muislamu na jamii kwa ujumla.

 

 

Nimejaribu kutoa ‘Mafunzo Na Mwongozo’ katika kila Hadiyth kwa kuweka nukta za maelezo mafupi.  Pia nimetaja Aayah za Qur-aan zinazohusiana na baadhi ya nukta nilizozitaja kwa kuona kuwa zitamsaidia mtu kuisherehi zaidi Hadiyth moja ikawa ni darsa kamili la kumtosheleza na kuwatosheleza anaowalingania. Kitabu hiki kinaweza pia kuwa ni mazoezi kwa mtu ikawa ni chanzo cha kutoa darsa kwa wenziwe.

 

Tanbihi: Baadhi ya nukta nimenukuu  kutoka :Nuzhatul-Muttaqiyn

 

 

Namshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) Kuniwezesha kuandika Kitabu hiki cha Lu-ulu-um-Manthuwrun (Lulu Zilizotawanywa) kwani hakuna Awezeshaye ila Yeye tu:

 

 

وَمَا تَوْفِيقِي إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ ﴿٨٨﴾

Na sipati tawfiyq (ya kuyawezesha haya) ila kwa Allaah. Kwake natawakali na Kwake narejea

 

 

Shukurani zangu za dhati kwa al-Akh Abu ‘Abdillaah Muhammad Baawaziyr, al-Akh Sa’iyd Baawaziyr, al-Akh Muhammad ‘Abdallah Al-Ma’awiy na al-Akh ‘Abdallah Mu’aawiyah kwa juhudi zao za kukipitia kitabu hiki, namuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Awalipe malipo mema yawe mazito katika mizani zao za mambo mema Siku ya Qiyaamah. Aaamiyn.

 

 

Na namuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Ajaalie kazi hii iwe kwa ajili ya kupata Radhi Zake Pekee na Ajaalie iwe yenye manufaa kwa ndugu zetu wa Kiislamu na namuomba Atughufurie na Atusamehe kwa makosa yoyote yatakayokuwemo. 

 

 

Wa-Swalla-Allaahu ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa aalihi wa Swahbihi wa sallam.

 

 

Ummu Iyyaad

14 Dhul-Qa’dah, 1432– 12 Oktoba 2011M

Kimehaririwa  Swafar 1439 H

 

 

 

 

Share