003-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Akimtakia Khayr Mja Humpa Mtihani Duniani

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 3

Allaah Akimtakia Khayr Mja Humpa Mtihani Duniani

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَا عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبلآءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلاَهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake khayr, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari, Humzuilia dhambi zake mpaka Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtihani mkubwa, na hakika Allaah Anapowapenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika, atapata Radhi [za Allaah] na atakayechukia, atapata hasira. [za Allaah])) [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa pamoja na anayesibiwa na mitihani akasubiri, na juu ya hivyo, ni alama ya mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:

 

وَكَأَيِّن مِّن نَّبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٦﴾

Na wangapi katika Nabiy alipigana vita, na pamoja naye (walipigana) Wanachuoni waswalihina, basi hawakulegea kwa yaliyowasibu katika njia ya Allaah, wala hawakudhoofika na wala hawakunyong’onyea. Na Allaah Anapenda wanaosubiri.  [Aal-‘Imraan 3: 146]

 

Rejea: Al-Baqarah (2: 153), Al-Anfaal (8: 46).

 

 

2. Alama za kufutiwa dhambi Muislamu pindi anapokuwa na subra katika mitihani.

 

 

3. Watu hupewa mitihani kulingana na taqwa na Iymaan zao.

 

 

4. Mwenye kuwa na subra katika mitihani ndiye atakayepata khayr za Siku ya Qiyaamah na malipo mema kabisa, kinyume na atakayeshindwa kuwa na subra:  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar 39: 10]

 

 

5. Muumin inampasa awe radhi kwa mitihani inayomfikia wala asikate tamaa au kuchukia bali ashukuru, na hii ndio sifa mojawapo ya Muumini wa kweli kama ilivyotajwa katika Hadiyth:

 

عن أبي يحيى صهيب بن سنانٍ رضي الله عنه، قَالَ: قَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((عَجَبًا لأمْرِ المُؤمنِ إنَّ أمْرَهُ كُلَّهُ لَهُ خيرٌ ولَيسَ ذلِكَ لأَحَدٍ إلا للمُؤْمِن: إنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكانَ خَيرًا لَهُ، وإنْ أصَابَتْهُ ضرَاءُ صَبَرَ فَكانَ خَيْرًا لَهُ)). رواه مسلم

Kutoka kwa Abuu Yahyaa, Swuhayb bin Sinaan  (رضي الله عنه)    amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Ajabu kwa jambo la Muumin; hakika mambo yake ni khayr, wala hakuna anayepata hilo isipokuwa Muumin pekee; akipatwa na furaha hushukuru basi huwa ni khayr kwake, na akipatwa na madhara husubiri basi huwa khayr kwake.” [Muslim]

 

 

6. Jannah si wepesi kuipata ila baada ya kuwa na taqwa, kutenda ‘amali njema na kuwa na subira katika mitihani.

 

Rejea: Al-Baqarah (2: 214).

 

 

7. Kuipita mitihani ni thibitisho kuwa mtu huyo yuwapendwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

8. Fadhila tele za subira katika mitihani zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah, miongoni mwazo ni kauli za Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾  

na wanaosubiri katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah: 177].

 

Na pia:

إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ﴿١١﴾

Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema hao watapata maghfirah na ujira mkubwa. [Huwd: 11]

 

Na pia:

 

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾

Jannaat za kudumu milele wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao. Na Malaika wanawaingilia katika kila milango.

 

سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾

 “Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu) kwa yale mliyosubiri.” Basi uzuri ulioje hatima njema ya makazi ya Aakhirah. [Ar-Ra’d: 23-24]

 

Na Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( مَا يَزَالُ الْبَلاَءُ بِالْمُؤْمِنِ وَالْمُؤْمِنَةِ فِي نَفْسِهِ وَوَلَدِهِ وَمَالِهِ حَتَّى يَلْقَى اللَّهَ وَمَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ)) الترمذي وقال حديث حسن صحيح

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Mtihani utaendelea kumpata Muumini mwanamume na Muumini mwanamke katika nafsi yake na watoto wake, na mali yake mpaka akutane na Allaah akiwa hana dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما)  عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلاَ وَصَبٍ وَلاَ هَمٍّ وَلاَ حُزْنٍ وَلاَ أَذًى وىَ غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ))

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abuu Hurayrah  (رضي الله عنهما)    kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Muislamu hatopatwa na tabu, wala maradhi, wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu [sononeko] hata mwiba unaodunga isipokuwa Allaah Humfutia madhambi yake kwa sababu ya hayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((مَثَلُ الْمُؤْمِنِ كَمَثَلِ الزَّرْعِ لاَ تَزَالُ الرِّيحُ تُمِيلُهُ وَلاَ يَزَالُ الْمُؤْمِنُ يُصِيبُهُ الْبَلاَءُ. وَمَثَلُ الْمُنَافِقِ كَمَثَلِ شَجَرَةِ االأرْزِ لاَ تَهْتَزُّ حَتَّى تَسْتَحْصِدَ)) متفق عليه

Kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)   kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)    amesema: ((Mfano wa Muumini ni kama mti ulio na rutuba, upepo unaupiga huku na kule, na ataendelea Muumini kufikwa na mitihani. Na mfano wa mnafiki ni kama mti wa seda [aina ya mti wa mbao ya mkangazi], hautikisiki hadi ung’olewe wote mara moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share