009-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Neema Mbili Watu Wengi Wameghilibika Nazo; Siha Na Faragha

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 9

Neema Mbili Watu Wengi Wameghilibika Nazo; Siha Na Faragha

www.alhidaaya.com

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((نِعْمَتَانِ مَغْبُونٌ فِيهِمَا كَثِيرٌ مِنْ النَّاسِ: الصِّحَّةُ وَالْفَرَاغُ))  رواه  البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu wengi wameghilibika katika neema mbili; siha na faragha [wasaa])).[Al-Bukhaariy.]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) hata wakati wa faragha kama Anavyosema:

 

 فَإِذَا فَرَغْتَ فَانصَبْ ﴿٧﴾

Basi utakapopata faragha fanya juhudi katika ‘ibaadah.

 

وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَب ﴿٨﴾

Na kwa Rabb wako elemea kwa raghba (kutakabaliwa).  [Ash-Sharh (94: 7-8)]

 

 

2. Siha na faragha yaani kuwa na wasaa (nafasi) ni raasilmali ya mtu, basi atakayetumia raasilmali yake vyema atapata faida, na atakayeipoteza atakhasirika na kujuta, na pindi yatakapomfika mauti  atatamani arudishwe duniani ili atumie vizuri neema hizi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾

Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: “Rabb wangu! Nirejeshe (duniani).”

 

 

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾

 “Ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.” (Ataambiwa) “Laa hasha!” Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu.  Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa.  [Al-Muuminuwn (23: 99-110)]

 

 

3. Umuhimu wa kunufaika kwa siha na faragha kabla ya kutoweka kwake, kwa kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kujitendea ‘amali njema. Hadiyth:

 

 

قال رسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم لرجلٍ وهو يَعِظُه: ((اغتنِمْ خمسًا قبل خمسٍ : شبابَك قبل هِرَمِك، وصِحَّتَك قبل سِقَمِك، وغناك قبل فقرِك، وفراغَك قبل شُغلِك، وحياتَك قبل موتِك))

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia mtu katika kumuwaidhi: ((Nufaika kwa mambo matano kabla ya matano; ujana wako kabla ya uzee wako, siha yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, wakati wako wa faragha kabla ya kushughulishwa kwako, na uhai wako kabla ya mauti yako))  [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1077), Swahiyh At-Targhiyb (3355)]

 

Rejea Hadiyth namba (58).

 

 

4. Watu wengi hawathamini neema mbili hizi. Kuna ambao wanaopoteza muda wao kwa mambo yasiyowanufaisha katika Aakhirah, na wanaharibu miili yao na hali Uislamu umesisitiza kuchunga wakati na viwiliwili.

 

 

5. Muumin atumie wakati wake wote kwa kutenda mema na kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ili ajiepushe na upuuzi na aweze kupata sifa miongoni mwa sifa za Waumini watakaopata Jannah ya Al-Firdaws.

 

Rejea: Al-Muuminuwn (23: 1-11).

 

 

 

6. Kutotumia neema alizopatiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) ni kukhasirika kwa mja duniani na Aakhirah.

 

Rejea:  Al-‘Aswr (103: 1-2).

 

Rejea pia Hadiyth namba (7), (45), (54), (61).
 

7. Kutokutumia vizuri neema mbili hizo za Allaah (سبحانه وتعالى) na nyenginezo nyingi ni kukosa shukurani. Kinyume chake ni kumshukuru Allaah (عزّ وجلّ) na hapo faida inamrudia mtu mwenyewe kwa kuzidishiwa neema kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu); na mkikufuru, basi hakika adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14: 7)]

 

 

 

Share