015-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kitendo Cha Bid’ah Hakikubaliwi Katika Dini Yetu

 

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 15   

 

Kitendo Cha Bid’ah Hakikubaliwi Katika Dini Yetu

 

 

 

 

عَنْ عَائِشَة (رضي الله عنها)  قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم:  ((مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدّ)) رواه  مسلم

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwenye kuzua katika hili jambo [Dini] letu lisilokuwemo humo, litakataliwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Hadiyth hii ni asili ya Dini na nguzo kati ya nguzo kama alivyosema Imaam An-Nawawiy (رحمه الله). Hivyo basi, kuna umuhimu mkubwa wa kumtii Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani hivyo ni kumtii Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ  

 Atakayemtii Rasuli basi kwa yakini amemtii Allaah [An-Nisaa 4: 80].

 

 

 

 

2. Dini ya Kiislamu ni Dini ya kufuata maamrisho na si ya kuongeza mambo na kuzusha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚوَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Hashr 59: 7]

 

 

3. Jambo lolote linalotendwa kama ni ‘Ibaadah ya kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى) ambalo halimo katika Qur-aan na Sunnah ni bid’ah (uzushi) litakataliwa, na mzushi au mtendaji uzushi hatopata thawabu yoyote, hata ikiwa kwa niyyah safi, na itakuwa ni kupoteza juhudi zake na mali yake kwa jambo lisilo na thamani mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan (25: 23)]

 

Rejea pia: Al-Kahf (18: 103-104).

 

 

4. Dini ya Kiislamu hairuhusu bid’ah yoyote bali inatilia nguvu kushikamana na Qur-aan na Sunnah, na hiyo ndio njia iliyonyooka ipasayo kufuatwa kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam (6: 153)]

 

Rejea pia: Yuwsuf (12: 108)

 

 

5. Hili ni onyo kwa Muislamu kutozua jambo lolote katika Dini kwani tayari Dini imekamilika kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.   [Al-Maa’idah (5: 3)]

 

 

Share