020-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Waumini Ni Kama Jengo Hutiliana Nguvu

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 20

 Waumini Ni Kama Jengo Hutiliana Nguvu

www.alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) قال: قال رَسُولُ الله (صلى الله عليه و آله وسلم): ((الْمُؤْمِنَ لِلْمُؤْمِنِ كَالْبُنْيَانِ يَشُدُّ بَعْضُهُ بَعْضاً)) وَشَبَّكَ أَصَابِعَهُ - متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsa (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Muumin kwa Muumin mwenziwe ni kama jengo, baadhi yake hutilia nguvu baadhi nyingine)) Akaviumanisha vidole vyake. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Waumini wa kweli ni wenye kuungana katika kila jambo lao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ

Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao  [At-Tawbah (9: 71)]

 

 

2. Waumini ni ndugu, hivyo inawapasa kutilia nguvu umoja wao. Rejea: [Aal-‘Imraan (3: 200).

 

 

3. Umoja unatia nguvu kama jengo linavyokuwa imara, na hakuna faida kutengana, kwani jengo halitokuwa na faida pindi linapokosa kushikana. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)

 

 إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِهِ صَفًّا كَأَنَّهُم بُنْيَانٌ مَّرْصُوصٌ﴿٤﴾

Hakika Allaah Anapenda wale wanaopigana katika njia Yake safusafu kama kwamba wao ni jengo lililoshikamana barabara. [Asw-Swaff: 4]

 

 

 

4. Umoja unasababisha mapenzi baina ya Waislamu na kupendeleana kheri za kila aina.

 

Rejea Hadiyth namba (21), (22), (23, (42), (43).

 

 

Na kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

“Mfano wa Waumini katika kupendana na kurehemeana kwao na kuhurumiana kwao ni sawa na mwili mmoja, kikishtakia kiungo kimoja basi mwili mzima utakosa usingizi na kushikwa na homa” [Al-Bukhaariy].

 

 

5. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni mwalimu bora kabisa kwa kutoa mifano mizuri ya hikma na busara katika kuonyesha au kuelezea jambo.

 

Rejea: Al-Ahzaab (33: 21).

 

 

6. Ni mbinu nzuri ya Da‘wah au ufundishaji kwa Daa‘iyyah (mlinganiaji) au mwalimu kwa kuonyesha kitu kwa vitendo. Na kufanya hivyo kunamfanya msikilizaji kuelewa na kufahamu zaidi

 

Share