032-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutoa Sadaka Na Kukinai Badala Ya Kuombaomba

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 32

 

Kutoa Sadaka Na Kukinai Badala Ya Kuombaomba

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((الْيَدُ الْعُلْيَا خَيْرٌ مِنْ الْيَدِ السُّفْلَى وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ.  وَخَيْرُ الصَّدَقَةِ عَنْ ظَهْرِ غِنًى وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللَّهُ وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللَّهُ)) البخاري

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Anza kwa unayemlisha. Sadaka bora ni inayotolewa baada ya kubakisha kitu. Anayejizuia [kutokuomba] Allaah Humtosheleza, na mwenye kukinai Allaah Humkinaisha)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Mafunzo na Mwongozo:

 

 

1. Uislamu unapendekeza kutoa zaidi kuliko kuombaomba. Allaah (سبحانه وتعالى) Amewasifia aina ya watu kama hao, Anasema:

 

 لِلْفُقَرَاءِ الَّذِينَ أُحْصِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ ضَرْبًا فِي الْأَرْضِ يَحْسَبُهُمُ الْجَاهِلُ أَغْنِيَاءَ مِنَ التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا ۗ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٢٧٣﴾

(Swadaqah ni) Kwa ajili ya mafakiri waliozuilika katika njia ya Allaah hawawezi kwenda huku na kule katika ardhi (kutafuta rizki); asiyewajua huwadhania kuwa ni matajiri kutokana na staha ya kujizua kwao, unawatambua kwa alama zao, hawaombi watu kwa ung’ang’anizi. Na chochote mtoacho katika kheri basi Allaah kwacho ni Mjuzi. [Al-Baqarah (2: 273)]

 

 

2. Aina ya mkono na daraja zake katika mas-alah ya sadaka ni nne: (i) Wa juu kabisa ni mtoaji (ii) Unaojizuia kuchukua (iii) Unaochukua bila kuomba (iv) Unaoomba.

 

 

3. Anayejizuia kuomba kitu Allaah (سبحانه وتعالى) Humkidhia na Humuruzuku kukinai.

 

 

4. Kujizuia kuomba ni kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) katika mas-alah ya rizki na ni miongoni mwa sifa za Muumin.

 

Rejea: Al-Anfaal (8: 2), An-Nahl (16: 42) Al-‘Ankabuwt (29: 59), Ash-Shuwraa (42: 36), At-Twalaaq (65: 2-3).

 

 

5. Sadaka bora ni ile anayoitoa mtu katika mali yake baada ya kujitosheleza mwenyewe na ahli zake.

 

 

6. Uislamu umesisitiza kutoa sadaka kwa kuanzia kwa ahli kama ilivyotajwa ((…anza kwa unayemlisha)).  

 

 

7. Fadhila za kutoa sadaka zimetajwa tele katika Qur-aan.

 

Rejea [Al-Baqarah (2: 245, 261), Al-Hadiyd (57: 11), Sabaa (34: 39)].

 

Rejea pia Hadiyth namba (31), (62),   

 

 

 

Share