Vipi Nihesabu Eda Yangu Ya Talaka

 

SWALI:

Asalaam aleikum,

Mie nimeachika lakini mume hataki kutoa talaka na mie na yeye tupo mbali mbali (nchi tofauti) sasa sijui nifanye nini.

Suala jengini Huko mume wangu alipokuwa ananitangazia mambo nilokuwa sijayafanya mabaya kwa jamaa zake na watu wake wakati mie huku ni mwanamke nilokuwa nimetulia na dini yangu sijashughulishwa na dunia. Sasa sijui nifanye nini kwa sababu maneno yashakuwa mengi. Ahsante

Swali linaendelea  

Assalaam aleikum

Mie nakaa nchi tofauti na mume wangu lakini kila baada ya muda tunaonana. Hivi karibuni ameniacha kupitia njia ya simu bila ya sababu ya msingi na sasa nipo kwenye edda.

Suala langu edda ya talaka rejea ni miezi mitatu lakini mie nimepata siku zangu mara mbili na bado siku kumi kupata mara ya tatu lakini ukifanya kwa ujumla haijatimia miezi mitatu bali ni miwili kasoro kidogo (period tatu) sasa nataka kujua nihesabu miezi au siku zangu. Ahsante.

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako hili zuri na kwa hakika maswali yanayohusiana na ndoa, talaka na mas-ala mengine ya kijamii ni mengi sana. Haya yanatuonyesha ya kwamba sisi tuna matatizo mengi ambayo yanaturudisha sisi nyuma. Kuhusu mas-ala ya eda ni kuwa unahesabu tohara na ada au kwa miezi ikiwa aliyeachwa ni mdogo na hajawahi kupata damu ya mwezi au akiwa mkongwe na damu ya mwezi imekatika.

 Sasa kuhusu kadhiya yako ni kuwa mume anafaa kukuacha katika kipindi cha tohara ambacho hajakuingilia kwayo. Sasa ikiwa ulikuwa katika tohara na baadae ukapata ada yako ya mwezi na kujitoharisha, hivyo hii ni Quruu’ moja. Tohara hii itafuatiwa na ada ya mwezi kisha tohara, na hii itakuwa ni Quruu’ ya pili. Tohara hii nayo itafuatiwa na ada ya mwezi kisha tohara, na hii itakuwa ni Quruu’ ya tatu na hivyo eda yako imekwisha. Ni hakika kuwa ikiwa umeachwa katikati ya tohara yako siku zitakuwa kidogo zaidi kuliko miezi mitatu.

 Maadamu amekupatia talaka ya mdomo bila ya kuandika tayari hiyo inahesabika ni talaka, hivyo eda yako inapomalizika unaweza kuolewa na mume mwengine bila ya matatizo yoyote isipokuwa anapokurudia kabla ya eda kumalizika au kuleta posa mpya na wewe kukubali posa hiyo baada ya eda. Kwa hiyo, huna haja kuwa na wasiwasi wowote katika suala hilo.

 Hili la kumtangazia mwenzako kwa jambo ambalo hajafanya ni katika kosa kubwa na dhambi kubwa na mwenye kufanya hivyo na adhabu kali Allah Anasema: “Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walioamini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui” (24: 19).

 Kwa hivyo dada yetu jambo hilo linauma lakini usihuzunike kwani kwa kusubiri Allah Atakuletea faraji. Allah Anasema tena: “Hakika wanaowasingizia wanawake, wanaojihishimu, walioghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa” (24: 23). Hii ni jazaa kwa wanaowasingizia Waumini kwa mambo ambao hawajayafanya, hasa tena wakiwa wanawake. Lau kama kungekuwa na dola ya Kiislamu basi ungeweza kushitaki kwa hilo na mume huyo angepigwa viboko themanini (80).

 Kitu ambacho unaweza kufanya mwanzo ni kusubiri katika haya maudhi ambayo unayapata na ujira wako utakuwa kwa Allah. Jambo la pili ni kusamehe kwani Allah Amewasifu watu ambao wanasamehe pindi wanapokosewa. Tafadhali tusome pamoja aya zifuatazo:

Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allaah Huwapenda wafanyao wema” (3: 134), na:

Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo” (3: 159), na:

Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Allaah Akusameheni? Na Allah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu” (24: 22).

 Kitu ambacho unaweza kufanya pia ni kuweza kuzungumza na wazazi au jamaa wa mtalaka wako ikiwa wapo karibu na uwaelezee tatizo hilo na hivyo wazungumze na mtoto wao na wamkanye. Au pia wazazi wako wanaweza kuzungumza na wazazi wake kuhusu hilo. Ikiwa wapo watu wengine ambao wanaweza kutumiwa katika hilo pia itakuwa kheri.

 Tunakuombea tatizo hili liondoke kwako na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akupatie subira ya kuweza kuupita mtihani huu.

 Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share