047-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kila Mmoja Atakuwa Analo La Kumshughulisha Siku Ya Qiyaamah

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 47

 

Kila Mmoja Atakuwa Analo La Kumshughulisha Siku Ya Qiyaamah

 

 

 

 

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها)  قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلا)) قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ، النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟  قَالَ: ((يَا عَائِشَةُ! الأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ  يُهِمَّهُم ذلِكَ))

 

وَفِي رِواية: ((ألأَمْرُ أَهَمُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ)) متفق عليه

                                                                                                                                             Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Watu watafufuliwa Siku ya Qiyaamah ilhali hawana viatu, wako uchi, ni mazunga [hawakutahiriwa])). Nikamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Wanaume na wanawake wote watatazamana? Akasema: ((Ee ‘Aaishah! Hali itakuwa ngumu sana hata hawatoweza kushughulika na jambo hilo!))

 

Katika riwaayah nyingine imesema: ((Hali itakuwa ngumu mno hawatoweza kutazamana)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Hadiyth inaashiria kama taswira hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah. [Rejeja Al-Infitwaar (82: 17-19), Al-Hajj (22: 1-2)].

 

 

2. Kila mmoja atakuwa na la kumshughulisha hata asijali aliyekuweko mbele yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾

Siku mtu atakapomkimbia ndugu yake.

 

وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾

Na mama yake na baba yake.

 

وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾

Na mkewe na wanawe.

 

لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾

Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza. [‘Abasa (80: 34-37)]

 

Rejea pia: [Al-Ma’aarij  (70: 10-14)].

 

3.  Watu watafufuliwa Siku ya Qiyaamah wakiwa pekee, watupu, hawana mtu wala chochote, kila walichomiliki wamekiacha duniani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَقَدْ جِئْتُمُونَا فُرَادَىٰ كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَتَرَكْتُم مَّا خَوَّلْنَاكُمْ وَرَاءَ ظُهُورِكُمْ ۖ  

  Na kwa yakini mmetujia mmoja mmoja kama Tulivyokuumbeni mara ya kwanza; na mmeyaacha nyuma yenu yote Tuliyokuruzukuni.  [Al-An’aam (6: 94]

 

Na rejea pia:  [Al-Kahf (18: 48),  Maryam (19: 93-95)].

 

 

4. Khofu ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kujisitiri hata Siku ya Qiyaamah.

 

 

5. Dalili ya sitara ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) dhidi ya yale walivyomzulia wanafiki katika kisa cha Ifk [An-Nuwr (24: 11-26)] na yale wanayomzulia Mashia mpaka sasa.  

 

 

6. Kila mmoja atakuwa anaitizama na kuijali nafsi yake tu. [Hadiyth ndefu ya kuhusu Shafaa’ah (Uombezi) ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pindi Nabiy Aadam, Nuwh, Muwsaa na Iysaa (عليهم السلام) watakapokataa kuwaombea watu Ash-Shafaa’ah watasema kila mmoja wao: “Nafsi yangu! Nafsi yangu! Nafsi yangu.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Share